Na Oscar Assenga, Muheza
JAMII ya watanzania imehimizwa kujenga utamaduni wa kuchemsha maji ya kunywa na kuyatumia,matumizi ya dawa za kutibu maji ‘water guard’ na matumizi ya vyoo bora utaratibu ulioelezwa kuwa utawasaidia kujiepusha kupatwa na magonjwa ya mlipuko.
 
Meneja wa shirika la PSI mkoani Tanga,Geofrey Mwankenja alitoa rai hiyo juzi kwenye maadhimisho ya siku ya kunawa mikono duniani,utumiaji wa vyoo bora na uzinduzi wa kampeni ya usafi wa mazingira ambapo kimkoa ilikuwa kata ya Mhamba huko Muheza.
 
Akiwahutubia wakazi kata hiyo ya Mhamba,Mwankenja alisema ili watu wengi hususani wale wanaoishi maeneo ya vijijini kuweze kunusurika  kupata magonjwa ya mlipuko ni vyema wananchi wakachukua tahadhari kwa kuchemsha maji kabla ya kutaka kuyatumia.
Mwankenja alisema kuwa taratibu zote za kiafya zikizingatiwa ni dhahiri kuwa wananchi wengi wataepuka adui maradhi kama yale ya mlipuko ambapo aliwasisitiza wakazi wa Mhamba kunawa mikono kwa sabuni pindi wanapotoka maliwato kujisaidia hatua aliyoieleza kuwa itasaidia kuokoa maisha ya watanzania waliowengi hususani watoto.
Akizungumzia shughuli zilizofanywa na shirika la PSI kwenye maadhimisho hayo ya siku ya kunawa mikono,Mwankenja alisema wameweza kutoa elimu juu ya wananchi kutumia vyoo shughuli ambayo imefanyika kwa baadhi ya vijiji vya wilaya ya  Muheza.
 
Alisema kuwa pia elimu hiyo wameweza kuitoa kwa njia ya sinema,sanaa ya ngoma,matumizi ya mabango na hata matangazo kupitia vipaza sauti vilivyofungwa kwenye magari yao ambapo kata nane za wilaya ya Muheza ziliweza kuelimishwa.
 
Mbali na kueleza hayo Mwankenja pia alisema,PSI ambayo imekuwa ikifanya kazi ya kuisaidia serikali kupambana na majanga mbalimbali imesaidia kukabiliana na  ugonjwa wa Ukimwi,malaria,magonjwa ya mlipuko na kuelimisha jamii kuhusu uzazi wa mpango.
 
Katika hayo Mwankenja alitanabaisha kwamba wamefanikiwa kuwapatia dawa za kutibu maji ‘water guard’ bure waathirika wa VVU huku wananchi wengine wakielimishwa na kushauriwa kununua dawa hizo kwa bei nafuu ya Tsh 200/= ili kuboresha afya zao.
 
Awali akiMwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Tanga aliyekuwa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo Marcel Clemence alisema zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa wanaohudhuria vituo vya huduma za afya nchini wanaugua magonjwa yatokanayo na usafi wa mazingira na maji.
 
Clemence ambaye ni kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Tanga alisema takwimu hizo ni kwa mujibu wa wizara ya afya na ustawi wa jamii (WAUJ) ambapo magonjwa ya kuhara yanachangia zaidi ya asilimia 54 ya wagonjwa wote wanaohudhuria vituo vya huduma.
 
Aliendelea kusema kuwa taarifa za shirika la kuhudumia watoto la umoja wa mataifa UNICEF zinaonyesha kwamba ugonjwa wa kuhara kuwa miongoni mwa magonjwa matano yanayoongoza kwa kuua watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
 
Clemence alisema,wakati kauli mbiu ya maadhimisho hayo inasema ‘Usafi ni ustaarabu unaanza na sisi,tumia choo bora,nawa mikono kwa sabuni,okoa maisha ya watoto na jamii kwa ujumla’ taarifa zinasema mtoto mmoja hufariki dunia kila baada ya sekunde 20 kwa kukumbwa na magonjwa yatokanayo na mazingira machafu na ukosefu wa vyoo.