https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543

Recent Post

Wednesday, October 02, 2013

MGODI UNAOTEMBEA: Chadema, leo mmeisahau ndoa ya CUF na CCM?Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WASWAHILI wana msemo wao, siku zote mla ndizi usahau, ila anayetupa maganda ni ngumu kusahau. Siku zote jambo hilo litakuwa kichwani mwake, akiwaza na kuwazua.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Huenda chuki ikawa ndani yake kwa kuangalia tukio hilo, ila yule aliyekula ndizi si ajabu akawa ameshasahau na kuendelea na maisha yake ya kila siku.

Nimejikuta nikianza hivi baada ya kuangalia muungano wa mashaka wa vyama vya upinzani Tanzania, kama vile Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama Cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi, inayoongozwa na James Mbatia.

Kabla sijaenda mbali zaidi, naomba niseme kuwa sina chuki na uamuzi wa muungano huo kwa wapinzani wala chuki ya viongozi wanaongoza vyama hivyo vya siasa vyenye hamu siku moja vishike dola.

Kwa wale wanaofuatilia siasa za Tanzania, watakumbuka jinsi CUF walivyotukanwa na kudhalilishwa na Chadema, ambao leo wamejirudi na kuunda muungano. Mara kadhaa CUF waliitwa sehemu ya CCM na kila walichohitaji kutenda, kilibezwa.

Mengi yalisemwa likiwamo hilo la CCM B ambapo tulishuhudia sumu hiyo ikienezwa kwa kasi katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani ili CUF ionekane si lolote kwa siasa za nchi hii.

Baada ya kuona haitoshi, Chadema bado wakaendeleza propaganda kwa wafuasi wao kwa kusema chama hicho kinachoongozwa na Profesa Ibrahimu Lipumba kuwa kinaongozwa na siasa za Liberal.

Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje, kwa kupitia chama hicho kinachoongozwa na Mwenyekiti wao Freeman Mbowe, alizusha mzozo mkubwa kwa kuwaambia CUF wana uhusiano na mashoga au wale wanaounga mkono ushoga na ndoa za jinsia moja ulimwenguni.

Jambo hilo lilisababisha mvurugano wa aina yake ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kiasi cha kuhofiwa ngumi kuzuka kutoka kwa baadhi ya wabunge hao.

Kwa wapenzi wa amani na waumini haswa wa siasa za kistaarabu, kauli ya Wenje ilikuwa ya kihemko zaidi. Ilikuja kwa nia ya kupata kuandikwa au kujulikana mtaani.

Kwa bahati mbaya, kauli hii na nyinginezo zote zilizokuwa zinatolewa kwa ajili ya kuwadhalilisha watu wa CCM na CUF, ziliishia hewani. Ni pale leo tunapoona Chadema wanakubali kuungana na CUF.

Je, Chadema ni lini wameikanusha ndoa ya CUF na CCM? Je, vyama hivi vinavyodaiwa ni ndugu vimewezaje tena kukubali undugu na Chadema? Ni ajabu mno.

Wahenga wanaendelea kusema, ukiwa mchoyo usiwe mroho. Hata hivyo haitoshi, wakasema tena, ukiwa muongo usiwe msahaulifu. Chadema ni wepesi kusahau mambo.

Suala hili litawatafuna hasa kama lengo lao ni kujenga propaganda hata zile zisizokuwa na mashiko kwao. Hii si haki. Najua Chadema na CUF wana malengo mazuri kwa ajili ya kuupitia vizuri suala la Rasimu ya Katiba inayotingisha kwa sasa.

Najua ndoa ya CCM kama kweli ilikuwapo, Chadema wao wameivunja na kufunga upya. Lakini ni rahisi kusema muungano wa CUF na Chadema ni mwepesi mno kuvunjika.

Hawa wote wanasumbuliwa na vita vya urais. Lakini pia sidhani kama kweli ndoa yao itashamiri kwa pande zote za Muungano.

Kwa mfano, Maalim Seif Shariff Hamad na Lipumba watawezaje kudumisha muungano wao kwa kusema kauli moja Visiwani Zanzibar?

Zanzibar imekuwa ikikiangalia vibaya Chadema na kusema ni chama cha Wakristo na hakina nafasi katika mioyo yao. Lakini hapo hapo, viongozi wao wanapanda tena jukwaani kuimba wimbo wa muungano ambao ukiangalia kwa kina unagundua umejaa utata.

Nasema haya kwasababu tunajua vyema mwenendo wa wanasiasa wa upinzani wa Tanzania na vyama vyao. Japo kwa sasa wanajiona wanaimba wimbo mmoja, lakini kiu ya madaraka kwao, wote wakiutaka kuunda serikali au kambi ya upinzani vinawasumbua.

Mara baada ya kuungana, eti wapinzani hao wakatinga katika ofisi za Msajili wa Vyama, Jaji Godfrey Mutungi, kwa nia ya kueleza dhamira yao ya kupinga Rais Jakaya Kikwete kuusaini Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Vyama hivyo vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi, vinavyounda ushirikiano wa kisiasa wa kupinga Rais kusaini muswada huo, vilimfafanulia Msajili huyo kilichotokea bungeni hivi karibuni, kwa wabunge wa upinzani nje ya ukumbi wa Bunge, wakati wale wa CCM wakipitisha muswada huo pamoja na marekebisho yake.

Kinachopiganiwa kwa sasa na hao wapinzani, ni kumtaka Rais Kikwete asisaini hadi kufanyika kwa maridhiano ya Kikatiba, huku Lipumba akisimama kama Mwenyekiti wa ushirikiano huo.

Katika mvutano huo, Lipumba anasema, “Tumefanya mazungumzo na Msajili, tulifika kumsabahi na kumweleza yaliyojiri bungeni kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na mchakato ulianzia tume mpaka kura ya maoni ya katiba, ila Zanzibar haikushirikishwa,” alisema Lipumba.

Kuonyesha kile walichokuwa wanakihitaji tangu awali, CUF na Chadema wanatangaza maandamano.  Ilikuwa lazima. Ni kawaida kwa maandamano kwa watu hawa.

Wanapohitaji lao hakuna wa kuwazuia. Na ndio maana tumeshuhudia watu wakipoteza maisha kutokana na wapinzani, hasa wanaotoka katika Chama cha Chadema kulazimisha hata pale wanapozuiwa au kushauriwa kwa vuzuri tu na jeshi la Polisi.

Naomba nieleweke. Nchi hii ni yetu wote. Tukisema tushiriki kwa pamoja kuibomoa, maisha yetu yatakuwa mashakani. Watanzania sasa katika nchi za Bara la Afrika hatuna marafiki wengi.

Hata wale tuliokuwa na uswahiba nao kama vile Rwanda tumeingia kwenye uhusiano mbovu. Nchi ya Kenya na Uganda pia hawa si wenzetu. Kama hivyo ndivyo, tukiibomoa Tanzania, tutaishi maisha ya kutanga tanga na huenda hawa wenzetu wakashindwa kutupokea.

Kuna kila sababu ya kuhakikisha nchi hii inaongozwa kwa ushirikiano na kusikilizana pia. Kila mmoja amuheshimu mwenzake. Hakuna sababu ya kuitana lugha za kuudhi.

Nitamshangaa Wenje na wengineo wanapozalisha siasa za chuki na uhasama bila sababu za msingi. Profesa Lipumba alisema Oktoba 10 mwaka huu ndio siku ya kitaifa ya kupinga kusainiwa kwa Sheria hiyo na kwamba maandamano yatakayofanyika yatakuwa ya amani.

Kuna mengi yanayohitaji kufanywa kwa ajili ya Tanzania inayokumbwa na matatizo ya kila aina. Kwa bahati mbaya, baadhi yao wanakosa uzalendo na kiu yao kubwa ni kujiwekea mazingira ya maisha yao.

Mbunge wa Ubungo kwa kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika yeye anasema kuwa ushirika wao utatumia njia za kidemokrasia kushinikiza Rais asisaini Sheria hiyo.

“Tutatumia njia za kidiplomasia kupinga na kuwaandaa wananchi kwa kutumia njia hizo, kwani jambo hili limekuja kwa muda muafaka kutokana na kauli zilizotolewa na viongozi wa masuala hayo, Jaji Joseph Warioba na Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe,” alisema Mnyika, ikiwa ni ishara ya kuutumikia muungano wao.

Muungano ambao bado una mashaka, ukizingatia kuwa wanasiasa wetu mara kadhaa wanachofanya wao ni kujiwekea mazingira ya kunufaika wenyewe.

Kwanza wenyewe siku zote hawapendani. Kinachofanywa kwa sasa ni kuzuga tu na ndio maana katika muungano huo bado kuna vyama ambavyo havijashirikishwa.

Chama kama NRA hiki licha ya kuwa na muda mrefu tangu kuasisiwa kwake, lakini muungano huo hawajashiriki, hivyo utashangaa wapinzani hawa wanazungumza ushirikiano upi wakati mara kwa mara wamezoea kutengana?

Nadhani huu ni wakati sasa wa kuangalia namna gani tunafanya siasa zenye kujenga jamii bora. Wapinzani kwa kupitia muungano huu wenye utata kwa CUF, Chadema na NCCR Mageuzi wanapaswa kufahamu umuhimu wa mchakato huo.

Hatuhitaji malalamiko yasiyokuwa na mashiko. Ni mara kadhaa wapinzani hasa Chadema wamekuwa wakilalamika lakini mwisho wa siku wanaacha kama ilivyo.

Mbaya zaidi, wakati mwingine ili wajionyeshe wao ni wenye huruma na Watanzania hufikia kutoka katika wakati mgumu, kama ule wa Bajeti ambayo matokeo yake hadi leo yanawatoa watu machozi.

Huu ni wakati wa kuangalia siasa zenye kujenga nchi na sio kubomoa, huku wanasiasa hao wakiacha hoja za mizaha kwa ajili ya kulinda majina yao bila sababu za msingi.

Mengi yanaweza kuja na kuondoka, lakini kumbukumbu mbaya za upinzani zitaendelea kuumiza kichwa hasa pale hoja nyepesi kuwa CUF wapo chini ya CCM.

Hata hivyo haitoshi, wakasimangwa tena kwa kuambiwa wana urafiki na chama kinachounga mkono ushoga, ingawa leo hoja hizo zimetiwa kapuni kwa zuga ya muungano usiokuwa na kichwa wala miguu.

Mwisho kabisa ni wakati wa vyama vya upinzani kuwa makini katika kujadili mambo ya Katiba ili waiache serikali na wale waliopewa jukumu hilo watupikie Katiba yetu kwa ajili ya Watanzania wote.

Hii ni kwasababu makundi yote yamefanikiwa kutoa maoni yao, wakiwamo wanasiasa na vyama vyao vya siasa, hivyo chokochoko zao hazina mashiko na zinaweza kuibua mtafaruku usiokuwa na kichwa wala miguu.
+255712053949

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...