Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
DAKTARI wa timu ya Simba, Yasin Gembe, amesema mshambuliaji wao
Khamis Tambwe, amepata mvurugiko wa tumbo hivyo kukosa kufanya mazoezi ya asubuhi na wenzake.
Muda wote wa mazoezi, Tambwe alikuwa nje ya uwanja, hivyo kuzua
hofu kwa wadau na mashabiki wa timu ya Simba wanaokoshwa na kasi ya
mshambuliaji huo ndani ya uwanja.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Gembe alisema kuwa
mshambuliaji wao Tambwe aliamka vibaya kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya
ghafla ya tumbo.
Alisema hata hivyo maradhi hayo si tatizo la kumfanya asiwe mzima
kwa siku mbili na kuongeza kuwa afya yake itatengemaa haraka kwa ajili ya
kuwapo uwanjani mwishoni mwa wiki pale timu yake itakapovaana na Ruvu Shooting,
Jumamosi, katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
“Tambwe anaendelea vizuri baada ya kupata tatizo la kuumwa tumbo,
ila hali yake haitampa wakati mgumu kuingia uwanjani kucheza na timu ya Ruvu
Shooting Jumamosi katika Uwanja wa Taifa.
“Mbali na Tambwe, pia majeruhi Henry Joseph na Issa Rashid wote
wamepona na wameanza mazoezi jana na wenzao, hivyo nadhani hii ni hatua nzuri
kwa Simba,” alisema.
Mechi ya Simba na Ruvu Shooting inasubiriwa kwa hamu na mashabiki
wa soka wa Simba, wenye hamu ya kuona timu yao inaendelea kufanya maajabu kwa
kushinda ili ijiweke katika nafasi nzuri kileleni.
No comments:
Post a Comment