Na Mwandishi Maalumu, Dar es Salaam
WAGOSI wa Kaya kutoka mjini Tanga, timu ya Coastal Union, imeendelea kufanya
vizuri kwenye michuano ya kuwania Kombe la Uhai inayoshirikisha wachezaji wenye
umri chini ya miaka 20 wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom baada ya jana kuifunga Toto Africans mabao 3-1.
Mabao ya Coastal katika mechi hiyo ya kundi A
iliyochezwa Uwanja wa Chamazi yalifungwa na Mohamed Miraji dakika ya 44, Abdul
Banda (dk. ya 62) na Ramadhan Shame (dk. ya 83). Toto Africans ndiyo iliyoanza
kupata bao dakika ya 30 lililofungwa na Severin Constantine.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Boniface Wambura, Coastal Union ilishinda mechi yake ya kwanza mabao 2-1
dhidi ya Tanzania
Prisons katika michuano hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa
kupitia maji Uhai.
Nayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya
African Lyon katika mechi ya kundi B iliyochezwa leo asubuhi (Desemba 12 mwaka
huu) Uwanja wa Karume. Miraji Athuman na Ramadhan Mzee ndiyo walioifungia Simba
dakika ya 15 na 47 wakati la African Lyon lilifungwa dakika ya 57 na Mbela
Kashakala.
Polisi Morogoro iliifunga Azam bao 1-0 kwenye Uwanja
wa Karume wakati katika Uwanja wa Azam, JKT Ruvu iliifunga Tanzania
Prisons bao 1-0 lililofungwa dakika ya 16 na Jacob Mambia. Yanga na Ruvu
Shooting zilitoka suluhu kwenye Uwanja wa Chamazi.
Katika mechi iliyochezwa leo asubuhi (Desemba 13 mwaka
huu) Uwanja wa Karume, Oljoro JKT imeizamisha Kagera Sugar mabao 3-0. Mabao
hayo yamefungwa na Hamis Saleh dakika ya 49 huku Shamir Mohamed akipachika
mawili dakika ya 52 na 55.
Michuano hiyo itaendelea kesho (Desemba 14 mwaka huu)
kwa michezo kati ya Mtibwa Sugar vs Toto Africans (asubuhi- Karume), Coastal
Union vs JKT Ruvu (mchana- Karume), Oljoro JKT vs Yanga (asubuhi- Chamazi),
Ruvu Shooting vs Kagera Sugar (mchana- Chamazi), Mgambo Shooting vs Simba
(asubuhi- Chamazi) na African Lyon vs Azam (jioni- Chamazi).
No comments:
Post a Comment