https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, December 21, 2012

Mwakamele: Mnyika usinikimbie



Mbunge wa Ubungo, John Mnyika
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MOTO umeendelea kuwaka kati ya mmiliki wa Kampuni ya Mc Donald Live Line Technology Ltd, Mc Donald Mwakamele kwa kumtaka Mbunge wa Ubungo, kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, aache kumkimbia badala yake athibitishe hoja anazotoa.
Mc Donald Mwakamele

Kwa wiki kadhaa sasa, wawili hao wamekuwa wakirushiana makombora, baada ya Mnyika kusema kuwa Mwakamele ni fisadi aliyepewa tenda nyingi katika Shirika la Umeme la TANESCO, likiwa chini ya William Mhando.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mwakamele alisema anamshangaa Mnyika kuendelea kupiga kelele ili ajijenge kisiasa, huku akishindwa kuweka ushahidi mezani.
 
"Mnyika aache kunikimbia na kama kweli ana hoja za msingi basi atangaze, maana nilishamwambia kuwa akithibitisha ukweli wake huo, atampa Milioni 20, ingawa ameshindwa na kubaki kupiga kelele,” alisema.

Mkurugenzi huyo wa Mc Donald aliyefanya kazi katika Shirika la Umeme kwa zaidi ya miaka 20, alisema badala ya kuendelea kupiga porojo kumnufaisha kisiasa, akutane naye, kuzungumzia hilo ili ukweli ujulikane na iwe nafasi kwa mbunge huyo kuwatumikia vyema wananchi wa Ubungo waliyomuweka madarakani.

Alisema Mnyika hana uwezo wowote wa kupambanua mambo zaidi ya kupiga soga na kuwaweka kwenye wakati mgumu wananchi wake wanaoishi maisha magumu, huku mbunge wao akibwabwaja mitaani, ndio maana ameshindwa kujenga hata choo kwa ajili ya wananchi wake Ubungo, huku akipenda kuzungumza kwenye vyombo vya habari akiamini ni mtaji wake kisiasa.

“Inashangaza, maana huu ufisadi unaozungumzwa na Mnyika ulifanyiwa uchunguzi na serikali. Sasa labda Mnyika aseme anataka mimi mtuhumiwa nijitangaze mwenyewe wakati anajua fika mambo haya yana wazungumzaji wao.

“Harakati za Mnyika zinashangaza, hivyo labda aniambie kuwa madai yake nimwambie yeye kwa serikali gani aliyokuwa nayo? Ipo serikali yenye viongozi makini, akiwamo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, anayefanya fanya kazi kwa ajili ya Watanzania wote, hivyo Mnyika aache siasa uchwara kwa kupiga porojo akiamini kuwa Watanzania wanapenda maneno yake,” alisema.

Mwakamele alisema kutwa na refarii kwenye kazi zozote ni jambo la msingi, hivyo yeye haoni sababu kuwa na refa Mhando, hasa kwenye kazi za Kimataifa.
 
“Sio kila wakati tunakiwa tufanye siasa, maana haya madai ya Mnyika yameshawahi kutokea Tanesco kwa kusimamisha uchukuaji wa nguzo katika kampuni za Kitanzania, ikiwamo ya Saohill ya Mafinga hadi Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene kupiga marufu suala hili.

“Mbali na hilo, kama utakumbuka Tanesco pia iliingia kwenye utata wa Richmond kwa kusimamisha mradi wao ambao baadaye ukawa mzigo mkubwa kwa serikali, hivyo wanasiasa wanapovaa vibwaya katika suala la ufisadi wawe na uthibitisho badala ya kuzungumza kwa kujua vyombo vya habari vitanukuu,” alisema.

Alisema katika kuhakikisha kuwa Taifa linapiga hatua, ameweza kufungua Chuo cha Umeme bila kuzima, akiamini kuwa mabilioni ya shilingi yataokolewa endapo teknolojia hiyo itatumiwa na Tanzania nzima, ingawa mgogoro mkubwa umeibuka kutokana na baadhi ya mabosi wa Tanesco kuipiga vita na Tanesco mkoani Morogoro kuuzima umeme katika njia inayokwenda kwenye chuo chake, alipotembelewa na wageni kutoka nchi mbalimbali duniani waliokwenda kushuhudia teknolojia hiyo inayoendeshwa na Mtanzania.

Mwakamele alisema anashangaa mbunge huyo kwa kuwa mwepesi kwenye vyombo vya habari, wakati alimtaka waonane uso kwa uso na kukataa, hata pale alipotangaza ofa ya milioni 20 ili atangaze ufisadi huo.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...