https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Thursday, December 20, 2012

CCM: wapinzani wetu mlie tu wilayani Handeni



Na Kambi Mbwana, aliyekuwa Handeni
UKITAKA kuuliza wilaya gani ya Tanzania ambayo hadi leo haijaharibiwa na vyama vya siasa, hakika Handeni itashika nafasi ya kwanza kama sio ya mwisho. Wilaya hii yenye vijiji 112 kata 19 na tarafa saba CCM imekuwa ikifanya vizuri mno.

Sio kama hakuna vyama vya upinzani kwa wilaya hiyo yenye kabila la wazigua hakuna, vipo, ingawa havina nguvu wala mashiko. Vijiji vyote vya wilaya hiyo vinatawaliwa na CCM, huku wananchi mmoja mmoja wakishindwa kufanya mabadiliko ya aina yoyote.

 Mwenyekiti wa CCM wilayani Handeni, Athumani Malunda

Hali hii ni changamoto kwa CCM. Ni pale watakapoweza kukaa kimya na kushuhudia wapinzani wakishika wilaya hiyo hasa kwa kusimamisha wenyeviti wa vijiji, madiwani au wabunge, hivyo kuwa jambo baya kwao.

Kwanini nasema hivi? CCM kuendelea kutamba katika wilaya ya Handeni ni heshima kubwa kwa wananchi wao, wakiona chama hicho kinastahili kushika dola. Kwasababu hiyo, vitu kama vile shule za msingi na sekondari, vituo vya afya, kilimo na shida ya maji ni mambo yanayotakiwa yaangaliwe upya.

Katika mazungumzo yaliyofanyika wilayani Handeni hivi karibun, mwenyekiti wa CCM wilaya, Athumani Malunda, anasema kwamba kukubalika zaidi kwa chama chao Handeni ni silaha ya kuendeleza mazuri yanayowapa imani na moyo wananchi wao kwa ajili ya kuwa na imani nao zaidi.

Anasema moja ya mambo wanayofanya ni kuhakikisha kuwa wenyeviti wa vijiji vya wilaya hiyo wanafanya kazi zao kwa ushirikiano na wananchi wao, huku wakiwa wakali na wale wanaofanya kazi kwa matakwa yao.

Kwa wenyeviti na watendaji wengine wa vijiji ambao wamekuwa wakiogopwa kama simba, hao watakula nao sahani moja kwa kuhakikisha kuwa wanabadilisha mwenendo wao kwa ajili ya kufanikisha maisha bora kwa kila Mtanzania.

“Kwa mfano, kuna baadhi ya wenyeviti wa vijiji ambao sera zao zinashangaza na hakika hawapendwi na wananchi wao jambo linaloweza kukiangusha chama katika siku za usoni, hivyo nimepangana na wenzangu kulisimamia hilo.

“Jambo hili nililifanya mara baada ya kutangazwa kuwa mwenyekiti wa CCM Handeni, nikijua kuwa nitafanya kazi kwa moyo wote kwa kushirikiana na viongozi wenzangu wa wilaya, akiwamo Katibu wangu, Salehe Kikweo, bila kusahau viongozi kutoka ofisi za mkoa na Taifa kwa ujumla, chini ya mwenyekiti wetu, Jakaya Mrisho Kikwete,” alisema.

Malunda anasema katika wilaya yao kumekuwa na ajenda za siri zinazofanywa na baadhi ya watumishi wakifanya mambo kinyume ambayo wakati mwingine wanafanya kwa nia ya kukihujumu chama chao siku za usoni.

Baadhi ya watumishi wa umma katika wilaya hiyo wamekuwa wakishindwa kusimamia vyema miradi ya maendeleo ya serikali, yakiwamo matatizo ya maji yanayowakabiri watu wa Handeni na Vitongoji vyake.

Anasema wapo watu wanaokubali uchimbaji visima vya maji kwa madai kuwa vipimo vyao vimegundua uwepo wa maji katika eneo husika, lakini baada ya fedha kuwekwa kwa ajili ya kufanikisha suala hilo, hugundua kuwa mahala hapo hakuna maji.

Malunda anasema tabia hiyo inaongeza shida ya maji pamoja na kejeli kutoka kwa watu ambao daima malengo yao ni kuona serikali ya CCM inashindwa kuwapatia maisha bora Watanzania, licha ya kulipanga hilo katika ilani zake.

“Hatuwezi kuchekea matatizo ya aina hii, hivyo tutakwenda nao sambamba kwa ajili ya kuona watendaji hao wanafanya kazi zao kama inavyotakiwa, maana wapo chini ya serikali inayoongozwa na rais Jakaya Kikwete.

“Kama hawataki au siasa zinawabana kwenye majukumu yao waamuwe moja ili tukutane katika majukwaa ya siasa na sio kuwahujumu watu wa Handeni kwasababu ya kukipaka matope chama chetu kinachopendwa na kuheshimika Handeni nzima,” alisema Malunda.

Kama watendaji wote watafanya kazi kwa kufuata sheria na sera za CCM zinazotekelezeka, hakuna sababu ya wananchi wao kukiweka pembeni chama chao zaidi ya kukipa heshima zaidi.

Juu ya suala la ardhi inayoporwa kama njugu na watu kutoka nje ya Handeni, Malunda anasema wanafurahia uwepo wa Mkuu wa wilaya wao mpya, Muhingo Rweyemamu kwa kufanya kazi nzuri, ikiwamo kusimamia ardhi na elimu kwa watoto wa kike.

Mengine wanayofanya kwa ajili ya Handeni yenye maendeleo ni kuhakikisha kuwa wajumbe wote wa CCM Handeni wanafanya kazi za chama kama inavyotakiwa pamoja na kuvunja makundi yao.

Aidha Malunda anasema kwamba wenyeviti wao wote wamewaagisa kuongoza kwa kufuata weredi na ushirikiano wao, ukiwapo kufanya mikutano ya mara kwa mara na wananchi wao, hasa kwa kusoma mapato na matumizi.

Nafasi ya mwenyekiti wa CCM wilaya ni ngumu, huku akiamini peke yake hawezi kuifanikishia chama chao bila kupata ushirikiano kutoka kwa viongozi wengine wa chama wilaya, mkoa na Taifa.

Kitu kinachompa imani ya chama chao kuendelea kufanya vizuri katika wilaya yao ni kuona viongozi na wanachama wao wote wapo kitu kimoja, jambo linalomfanya aone mazuri yataendelea kupatikana.

Mwenyekiti huyo anasema amekulia katika mikoa ya CCM tangu utoto wake, hasa kwa kuwa kwenye skauti na kushiriki shughuli za kichama hadi anakuwa Mwenyekiti wa wilaya kwa kura nyingi.

Wapo watu walioshindwa kuelewa kuwa atafanikiwa kushika nafasi hiyo, huku kanuni zake za uzalendo, mapenzi na moyo wa kukitumikia chama akikiweka mbele, jambo linalomfanya afanye kazi ya chama wakati wowote.

Kuhusu maendeo ya pamoja ya wilaya ya Handeni, Malunda anasema kwamba huruma na moyo wa dhati wa Mbunge wao, Dk. Abdallah Omari Kigoda kunasababisha waone mazuri mengi, ikiwamo barabara za kuunganisha wilaya na mikoa, vituo vya afya, shule za msingi na sekondari zinazojengwa kila Kata.

Kwa wananchi na wadau wengine wa Handeni wanapaswa kumpa ushirikiano mbunge wao huyo aliyeoingoza Handeni kwa mafanikio makubwa, tangu alipopata nafasi hiyo miaka 15 iliyopita na kupendwa na kila mtu.

Wapo watu ambao kwa namna moja ama nyingine wanaweza kuiendeleza wilaya hiyo ya Handeni, lakini wanabaki kimya wakiwa na hamu ya kuona mabaya ya kukosoa, jambo linalostahili kupingwa na kila mtu.

“Handeni ni yetu wote hivyo yoyote mwenye mapenzi mema anapaswa kushirikiana na uongozi kwa kupitia sisi tuliopewa majukumu ya kichama, mbunge wetu Kigoda na ofisi za serikali zikiongozwa na Mkuu wa wilaya, Muhingo.

“Naamini tukifanya hivyo, neema itakuwa ya aina yake, hivyo kizazi chetu cha leo na kesho kuja kuishi mahali pazuri, hasa kwa kudhibiti kwa vitendo suala la ardhi, elimu kwa watoto wetu, kilimo bora na kukwepa uvunaji wa misitu ovyo,” alisema Malunda.

Bila shaka viongozi wa CCM na Taifa kwa ujumla wanapaswa pia kuitumia nafasi hiyo ya watu wa Handeni kuwapa nafasi za kuwaongoza, wafanye pia yale yanayoweza kulingana na fadhira za watu wao, ukizingatia kwamba wameendelea kuwaona wao ndio wanaostahili kuwapo madarakani kwa kupitia chama hicho kikongwe hapa nchini.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...