https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Saturday, December 22, 2012

Dawa za kulevya ni tatizo kwa wasanii Tanzania



 Ray C ni mmoja wa waathirika wa dawa za kulevya
 Ray C

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
HARAKATI za kupambana na utumiaji wa dawa za kulevya ni ngumu sana katika vizazi vyetu vya leo, vinavyojumuisha pia wasanii nchini. Hawa ni watu makini, ila wameingia kwa kasi mno katika utumiaji wa dawa za kulevya.
Ramadhani Masanja (Banza Stone mwimbaji wa muziki wa dansi.
Nakumbuka miaka minne iliyopita, msanii ambaye pia ni mwanasiasa kutoka Chama Cha Wananchi (CUF), Kalapina, alitunga wimbo uliokwenda kwa jina la ‘Hip Hop bila Madawa’.

Wimbo huu ulifanya vizuri, maana ulijaribu kuelezea matatizo na wasanii wale waliojihusisha na utumiaji wa dawa za kulevya.

Sina uhakika kuwa kati ya wale waliotajwa kwenye wimbo huo ni kweli wanatumia dawa za kulevya ama walitajwa kama wawakilishi tu wa wasanii.

Sitaki kuwataja tena katika makala haya, maana kwa wasanii na wanaofuatilia kwa karibu sanaa, wimbo huo na watajwa wanawajua.

Hii ndio hoja yangu. Hoja ambayo inaelezea kwa kirefu kadhia ya wasanii wa Tanzania kujiingiza kwa kasi katika utumiaji wa dawa za kulevya.

Katika kuliangalia suala hilo, kama ilivyokuwa kwa sanaa hii mara nyingi kuigwa kutoka nje, wasanii wanaona kuna umuhimu wa kuiga kila kitu, ikiwamo utumiaji wa dawa za kulevya.

Haya ni matatizo makubwa. Kama wasanii wetu wanaotegemewa kuelimisha jamii nao wanakuwa waathirika wakubwa, Tanzania inaelekea wapi.

Mimi ni miongoni mwa Watanzania walioshtushwa na habari za msanii wa kike nchini, Rehema Chalamila, maarufu kama Ray C.

Nilishtushwa ndio, maana habari za yeye kutumia dawa za kulevya zilianza kuvuma zamani, hadi kusaidiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.

Pamoja na hayo, Ray C ni mmoja kati ya Watanzania wengi wanaoingia kwenye utumiaji wa dawa hizo. Wapo wengi wanaoingia kwenye matumizi hayo yasiyokuwa na faida yoyote ile.

Hii ni aibu kubwa. Hatuwezi kuvuna chochote kama wasanii pamoja na jamii yapo wataona starehe nzuri ni dawa za kulevya.

Nikiambiwa nielezee athari za dawa za kulevya, kwa msanii kama Ray C, naweza kusema kuwa matumizi hayo yamesababisha pia kutaifisha kipaji chake.

Ray C yule aliyekuwa anajituma jukwaani pamoja na kuachia nyimbo nzuri zilizotikisa katika vituo vya redio, si huyu wa leo anayeisubiri hisani ya raisi.

Haya ni matatizo makubwa. Nadhani kwa kulijua hilo, wasanii pamoja na jamii yao kwa ujumla wanatakiwa jiangalie mara mbili. Dawa za kulevya hazina faida zaidi ya kuwapa athari kimaisha.

Dawa za kulevya si tu ni hatari kwa afya za watumiaji, bali pia zinauzwa kwa bei ghari kupita kiasi. Mtumiaji kwa siku anatakiwa asiwe na kiasi kisichopungua 20,000 kwa watu wenye kipato cha chini.

Mbaya zaidi, kadri mtu anavyozea dawa hizo, gharama yake inazidi kupanda mara dufu, hivyo fedha zake nyingi kuingia katika starehe hizo zisizokuwa na mpango wowote kwa jamii yetu.

Ukiangalia kwa haraka, utagundua wasanii wengi wanaishiwa nguvu kwasababu ya janga hilo. Muda wao mwingi wanaitumia katika sterehe na kupoteza pia gharama zao.

Wengine sauti zao zinatoweka baada ya kujiingiza katika utumiaji huo wa dawa za kulevya. Ni hatari tupu. Nadhani wasanii wenyewe wanatakiwa wajiangalie kwa ajili ya kuboresha maisha yao.

Kila msanii lazima ajuwe kuwa utumiaji wa dawa za kulevya si ujanja bali ni ujinga na hasara kwa maisha yake ya sanaa. Hakuna cha maana anachoweza kukipata katika kuingia kwenye anasa hizo.

Kinyume cha hapo atapata hasara kubwa kifedha pamoja na kukosa mbinu za kujiendeleza kisanaa. Huo ndio ukweli.

Harakati za kupambana na dawa za kulevya ziendelezwe kwa kuwaelimisha jamii kwa kupitia wasanii wetu na sio kuanzia kwa waelimishaji wetu.

Sanaa ni kioo cha jamii. Lakini kwa bahati mbaya baadhi ya wasanii wamekuwa wakisumbuliwa na ujinga wa kuiga hata kula kinyesi. Huu ni ujinga wa karne. Wasanii wetu wajiepushe na matumizi haya mabaya na yanayoharibu vipaji vyao kwa namna moja ama nyingine.

Huu ndio ukweli. Tuukubali kwa ajili ya kuwa na kizazi chenye kujitegemea na mafanikio makubwa kutokana na kazi zao na sio kupoteza muda wao kutumia dawa za kulevya zinazonunuliwa kwa gharama kubwa mno.

0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...