https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Wednesday, December 26, 2012

MGODI UNAOTEMBEA




CCM Handeni isicheze na fikra za walalahoi
Mkuu wa Mkoa Tanga, Chiku Galawa
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI kawaida yangu sasa kila ninaposafiri kwenda mahali popote, ninaporejea huchukua walau muda mdogo kuandika changamoto zinazowasumbua Watanzania.

Katika kuandika kwangu, huwa pia siangalii chama wala taasisi yenye kushindwa kuwasimamia kikweli Watanzania, nikiamini dosari hizo zitaongeza umasikini wa raia wake.
Mkuu wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu
 
Ni kweli. Na katika hilo, baadhi ya wadau wameshindwa kunielewa mtazamo wangu mara moja, huku wakishindwa kuniweka katika kundi la chama Fulani.
Mwenyekiti wa CCM Handeni, Athumani Malunda
 
Kwa mfano, wapo wanaonisema wakidhani mimi ni shabiki wa chama Fulani, iwe Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama Cha Wananchi CUF, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo chadema na vinginevyo vinavyosajiliwa kila uchao.

Meseji zinazokosoa au kusifia nazipata kwa wingi, huku baadhi yao nikiwajibu kuwa, sioni sababu za kuweka chama changu mbele, hasa ninapojadili maslahi ya Watanzania.

Inaweza kuwa ni kweli mimi ni mfurukutwa kama wanavyosema baadhi yao, lakini sio tiketi ya kukiacha chama hicho kiende kama mbuzi waliopotea machungaji kwa kushindwa kuwakosoa viongozi waliokuwa kwenye uongozi.

Ingawa nitakuwa mwana CUF, Chadema au TLP. Lakini ninapoona mapungufu, sibaki nyuma kusema, ndipo hapo watu wanaposhindwa kuelewa nipo mlengo gani?

Sio lengo langu kuelezea aina ya maisha yangu na changamoto zangu, maana sijaandika makala haya kwa ajili hiyo.

Lengo langu ni kuutaka uongozi mzima wa CCM wilayani Handeni, mkoani Tanga na Tanzania kwa ujumla kuangalia sera na changamoto zinazoweza kuwapatia maisha bora.

Endapo maisha bora yatapatikana kwa wilaya hiyo, hakika hizi shangwe na majigambo kuwa CCM itaendelea kutawala milele wilayani humo zitafanikiwa.

Kwanini nasema hivi? Kwa miaka 51 sasa ya Uhuru Chama Cha Mapinduzi CCM kimekuwa imara kwa wilaya nzima ya Handeni, hasa kwa wananchi wake kukiweka madarakani.

Lakini, licha ya wananchi hao kuipa dhamana ya kuongoza katika chaguzi mbalimbali, lakini kuna njia nyingi zinazowapa ahueni CCM katika jimbo hilo linalotawaliwa na Mbunge wa Handeni, Abdallah Omari Kigoda.

Kwa sababu hiyo, nashawishika kusema kuwa bila mipango madhubuti kutoka kwa viongozi wa wilaya, mkoa na Taifa kwa ujumla, kuna siku CCM Italia kilio cha mbwa.

Nasema hivyo kwasababu  ni ngumu sana kumlinda mbwa mwenye njaa. Na hakika hakuna fundi wa aina hiyo. Mbwa mwenye njaa hawezi kutulia nyumbani kwao.

Ili akae nyumbani, lazima mfugaji amfunge nyororo mara kwa mara kwa kujua wakati wowote atakimbia. Huu ndio ukweli. Wanachama na Watanzania wanaoshi Handeni ni sawa na mbwa mwenye njaa.

Kukaa katika chama hicho miaka nenda rudi ni hadithi. Hatuwezi kuwalinda wananchi wasikipige chini chama hiki kikongwe kama hakuna juhudi za maisha yao kuwekwa sawa.

Viongozi wa Chama na serikali kwa pamoja wakae na kusikiliza malalamiko kutoka kwa wananchi wao. Matatizo ya uvamaizi wa mashamba yao yafanyiwe kazi.

Matatizo ya maji nayo yasipofanyiwa kazi hakika wananchi lazima waichukie CCM. Nasema hivyo kwasababu nimekuwa nikitembelea wilayani humo mara kwa mara.

Nashukuru, katika kutembea kwangu huko, sikuwa na lengo la kuangalia matatizo tu kwa ajili ya kuyaanisha kwa lengo tofuati kama inavyofikiriwa na baadhi yao.

Kutembea kwangu huko kuna lengo la kuangalia namna gani wananchi wa Handeni maisha yao yanakuwa mazuri kwa kupitia uongozi uliopo madarakani.

Nilipokuwa Handeni niliweza kufanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa chama na serikali.

Nashukuru, maana nilipewa nafasi ya kusikilizwa namna gani wananchi wanaweza kushirikiana na viongozi wao kwa ajili ya maendeleo ya Handeni.

Hata hivyo, mazungumzo hayo yamekuwa yakizungumzwa mara kwa mara, huku baadhi yao zikishindwa kufanyiwa kazi. Kama hivyo ndivyo, yoyote anayeishi maisha mazuri na familia yake huku raia wake wakilala njaa huyo anatia shaka.

Wimbo wa kero ya maji katika wilaya ya Handeni unaweza kuachwa kama sera na mipango itachukuliwa.

Ndio, baada ya kuhanagaika sana, hatimae miezi michache ijayo, wananchi wataweza kuzunguukwa na barabara ya lami.

Hadi sasa, ukitoka Dar es Salaam kwenda Handeni kwa kuingilia Mkata ni lami kwa lami.

Lakini pamoja na hayo, ile nyingine ya kotoka Korogwe kwenda Handeni nayo inaendelea kujengwa, jambo litakalokuwa na faida kubwa.

Tusiishie hapo. Tupige hatua ya mbele zaidi. Lazima tujuwe kuwa barabara hizo zinatumiwa kimaendeleo. Watu wa Handeni waishi kwa kufanya kazi ipasavyo ikiwamo wale wajasiriamali wanaoishi ndani na nje ya Handeni.

Serikali ya CCM ilijuwe hilo, maana mambo yasipoangaliwa kwa kina, watu kutoka nje wanaweza kunufaika na barabara hizo, huku wenyewe wakidoa macho.

Utashangaa kwanini nasema serikali. Hii ndio kila kitu. Hata kwa kupitia mfuko wa Jimbo, sehemu ya mfuko huo inaweza kutumika kuendeleza wakulima au wajasiriamali.

Kama hivyo sivyo, basi pia kuwe na mipango ya kuwasimamia watu na kuwaendeleza katika kilimo maana ndio uti wa mgongo. CCM isibaki kusema tu chama kitatawala milele kama alivyosema mwenyekiti wake wa wilaya, Athumani Malunda, alipozungumza na Mtanzania wilayani humo.

Kila mwana Handeni wakiwamo viongozi na wananchi wao wafanye kazi kwa ushirikiano kwa ajili ya watu wote.

Mwenyekiti wa wilaya na Katibu wake wawe wakali zaidi kusimamia watendaji, wakimpa ushirikiano Mkuu wao wa Wilaya, Muhingo Rweyemamu, aliyeingia Handeni kwa miguu yote.

Tusiwe watu wa kutangaza miradi ya maendeleo na kushindwa kuiendeleza. Wakati mwingine huwa nasema, sera za kwenye makaratasi ni tatizo kubwa.

Wengineo wamekuwa wakiumizwa sana na maneno yangu, lakini huo ndio ukweli wa mambo. Nausema kwakuwa tunafanya yale ya kuiendeleza nchi yetu.

Kama hatutaelezana ukweli, ina maana kupiga hatua ya mbele zaidi ni kujidanganya tu. Tufanye siasa lakini pia wakati mwingine tuwe na sera zinazotekelezeka.

Sio Handeni tu, bali pia wilaya zote zilizopata viongozi wao wa CCM wafanye kazi imara ya kuendeleza maendeleo yao.

Huo ndio ukweli. Lakini tusipofanya hivyo, kuwang’ang’ania wananchi waendelee kukiheshimu chama chao ni kumpigia mbuzi gitaa wakati tunajua hawezi kucheza.

Kwa Tanzania ya leo inayokua kidemokrasia na kukua kwa vyama vya siasa vya upinzani, kuna siku wananchi wake watajuwa kwanini chama tawala kinastahili kukaa pembeni.

Watafanya hivyo kwasababu tangu walipozaliwa, wameikuta CCM katika maeneeo yao, huku wakiendelea kubaki kama walivyo, wakati wenzao wanapiga hatua.

Wilaya hii ya Handeni kutokuwa na nguvu ya vyama vya upinzani sio matokeo mazuri kwao, maana wakishaelewa kuwapata ni kazi ngumu mno, hivyo CCM iliangalie hilo.

Nalisema hili kwasababu ndio maisha yangu ya kawaida kuhubiri ukweli, huku nikijweka kando na fitina kwa kusifia kila linalofanywa hata kama najua ni baya.

Na ikitokea wapinzani wanakuwa na sauti Handeni kama ilivyokuwa katika baadhi ya maeneo, viongozi waliopo wataonyesha udhaifu wao kwa kushindwa kuelewa kuwa siku zote mipango ya kushinda vita yoyote ni kumfuata adui mbele na sio kusubiri aje kukuvamia, maana atatuamia silaha zako mwenyewe kukumaliza.

0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...