https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, December 17, 2012

Badi Bakule ataka milioni saba za Muumini



Mwanamuziki Badi Bakule akiwa jukwaani
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MWANAMUZIKI mahiri wa muziki wa dansi wa The African Stars, Twanga Pepeta, Badi Bakule, amedaiwa kutaka milioni saba ili aweze kujiunga na bendi ya Victoria Sound ya Mwinjuma Muumini.

Hitaji la Bakule limejulikana muda mchache baada ya kutajwa kutakiwa na uongozi wa Victoria Sound kwa ajili ya kuiboresha zaidi bendi hiyo inayopigania umaarufu kwenye medani ya dansi nchini.

Habari kutoka kwa mtu wa karibu na bendi ya Victoria Sound zilisema kuwa awali waliketi na Badi kuzungumzia ujio wake kwenye bendi hiyo, lakini alitangaza dau lake la Milioni saba, kama ada ya uhamisho wa kutoka Twanga Pepeta.

Ada hiyo ilimshinda Muumini na kumuacha aendelee na maisha yake Twanga Pepeta, ingawa sauti na uwezo wa mwanamuziki huyo inahitajika katika bendi hiyo iliyoongezwa pia kwa mwimbaji mwenye sauti ya mvuto, Waziri Sonyo.

“Badi Bakule anataka fedha nyingi sana, milioni saba ndio aweze kujiunga na bendi yetu, hivyo hatuwezi kukubaliana naye zaidi ya kumuacha abaki kwenye bendi yake ya Twanga Pepeta, maana huwezi kumlazimisha mtu,” alisema mdau huyo wa Victoria Sound.

Alipoulizwa Badi juu ya ada hiyo alisema, “sijafanya mazungumzo yoyote na Muumini juu ya kutaka niende kwenye bendi hiyo, lakini mimi kazi yangu ni muziki sidhani kama nisingeweza kukutana nao kuangalia maslahi yangu,” alisema Badi.

Badi Bakule ni miongoni mwa wanamuziki wenye uwezo wa juu katika ramani ya muziki wa dansi hapa nchini, huku sauti yake ikipendeza zaidi anapofanya kazi pamoja na Mwinjuma Muuni, tangu enzi za Tam Tam.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...