https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, December 28, 2012

Klabu 14 zatishia kugomea Ligi Kuu


Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SHIRIKISHO la Soka nchini (TFF), limesema kuwa klabu 14 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom zimesusia kucheza hatua ya pili ya Ligi hiyo itakayoanza Januari 26 mwakani hadi zitakaporejeshewa fedha zao zilizochukuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka kwenye moja ya akaunti za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage

Novemba 23 mwaka huu, TRA kwa uwezo ilionao kisheria iliielekeza benki ya NMB kuilipa fedha hizo (sh. 157,407,968) kutoka kwenye moja ya akaunti za TFF ikiwa ni Kodi ya Lipa Kama Unavyopata (PAYE) kutoka kwenye mishahara ya waliokuwa makocha wa timu za Taifa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotuma kwenye vyombo vya habari na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wamburaa, ilisema kuwa uamuzi wao huo unatokana na kujua kuwa Serikali ndiyo inayolipa mishahara ya makocha wa nje moja kwa moja kwenye akaunti zao, huku ikiacha kukata PAYE kwa mishahara hiyo na kufikia kufikia malimbikizo ya sh. 157,407,968.

TFF bado inaendelea na mazungumzo na pande husika (Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa upande mmoja na TRA kwa upande mwingine) ili fedha hizo zirejeshwe kwani zilitolewa na mdhamini wa Ligi Kuu (kampuni ya Vodacom) kwa ajili ya maandalizi ya timu hizo tayari kwa mzunguko wa pili wa Ligi hiyo.

Katika hatua nyingine, TFF imesema kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) litamtuma nchini ofisa wake Abbas Sendyowa kukagua viwanja na hoteli ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa utaratibu wa klabu kupata leseni zitakazoziwezesha kushiriki michuano inayoandaliwa na CAF katika ukanda wao.

Ofisa huyo kutoka Uganda atawasili nchini Januari 7 mwakani ambapo anatarajiwa kukamilisha kazi hiyo Januari 14 mwakani na baadaye kupeleka ripoti yake CAF.

Aidha, Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA) kumuondoa Nazarius Kilungeja kugombea uenyekiti katika uchaguzi wa chama hicho.

Kutokana na uamuzi huo, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeiagiza Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA kuendelea na mchakato wa uchaguzi huo kama ilivyopangwa awali.


No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...