https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, December 17, 2012

Chipukizi wa Hip Hop mwenye ndoto lukuki




Felister Phillip Maginga-Lady Black

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KUTOKANA na mafanikio katika kona ya muziki wa kizazi kipya maarufu kama Bongo Fleva, vijana wengi wamekuwa wakijiingiza katika sanaa hiyo kwa ajili ya kujitafutia maisha yao.

Katika hilo, wapo wengi wanaofanikiwa kwa namna moja ama nyingine, jambo linalofanya wasanii wachanga kukimbilia kwa wingi katika tasnia hiyo ya muziki nchini.

Miongoni mwa wasanii hao wachanga ni Felister Phillip Maginga. Binti huyo mwenye asili ya Shinyanga, amepania vilivyo kuhakikisha kuwa anaweza kujipatia maisha yake kwa kupitia sanaa ya muziki wa kizazi kipya.

Ney wa Mitego, chaguo la kwanza la Lady Black

Dada huyo anajulikana kama Lady Black. Tayari amesharekodi wimbo wake unaopigwa katika baadhi ya vituo vya redio hapa nchini. Wimbo huo unaitwa Dis Me, aliyoimba kwa mtindo wa Hip Hop, muziki unaohitaji ubunifu mwingi.

Katika mazungumzo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, Lady Black, anasema kwamba ameamua kujiingiza katika muziki wa Hip Hop ili aboreshe kipaji chake na kutafuta maisha yake kwa kupitia muziki.

Anasema amezaliwa na kipaji cha muziki tangu akiwa na umri mdogo, hivyo kwa kitendo chake cha kuamua kushika kipaza sauti, ni kuweka mambo sawa na kufanikisha kutimiza moja ya malengo yake aliyojiwekea.

“Napenda sana kuimba tangu zamani hasa muziki wa Hip Hop hapa nchini, huku moja ya watu ninaotamani kufanya nao kazi ni Ney wa Mitego.

“Naamini haya yote yatafanikiwa kwasababu nimejipanga imara katika kuweka malengo yangu na jinsi gani ya kuanza vyema safari hii ninayoipenda na kuweka mikakati kabambe katika kuhakikisha kuwa natimiza malengo yangu,” alisema Lady Black.

Dada huyo anasema licha ya kuachia wimbo huo wa Dis Me, lakini unapigwa kidogo kidogo kutokana na ugeni wake katika ramani ya muziki wa Hip Hop nchini, huku akiamini kuwa nyimbo zitakazofuata mambo yatakuwa mazuri.

Anasema licha ya kuimba muziki wa Hip Hop, lakini kipaji chake kimekuzwa na muziki wa asili, akimpenda zaidi mwimbaji Saida Karoli aliyewahi kutamba ndani na nje ya nchi na nyimbo zake nyingi ukiwamo Chambua kama Karanga.

Lady Black anasema kwamba wimbo wake wa kwanza ameurekodi katika Studio za Ukombozi zilizopo Yombo, huku ukifanikiwa kumuweka katika ramani nzuri kutokana na ugeni wake katika tasnia ya muziki huo nchini.

Msanii huyo anasema kipaji chake kilizidi kushika kasi baada ya kutua jijini Dar es Salaam, akitokea kijiji kwao Ilola, kilichopo Shinyanga Vijijini mwaka 2002, ambapo pia safari yake ilitokana na wazazi wake kuhamia jijini humu.

Anasema kwamba baada ya kutua Dar es Salaam, alijiunga na vikundi mbalimbali kwa ajili ya kujiwekea mazingira mazuri ya kibiashara, akijua kuwa katika mtindo huo, vijana waliweza kustawisha vipaji vyao.

Mwanadada huyo mwenye mwonekano wa kisanaa anasema kwamba kwa sasa anachofanya ni kuweka mazingira mazuri ya kibiashara kwa kutunga na kurekodi nyimbo nzuri kwa ajili ya kumnemeesha zaidi.

“Huu ni wakati wangu wa kufanya kazi nzuri zaidi kwa ajili ya kuniweka katika nafasi nzuri, ukizingatia kwamba nimeamua kufanya kazi ya muziki, hivyo lazima nivumilie na kuweka mikakati kabambe nifikie malengo yangu.

“Naamini mambo yatakwenda sawa kwa kuhakikisha kuwa natunga nyimbo na kuwapelekea mashabiki wangu kazi nzuri zenye ujumbe na mtindo wa kuwafurahisha zaidi, ukizingatia kwamba nimeamua kuishi kisanaa,” alisema Lady Black.

Mwanadada huyo anasema kwamba kwa sasa anafanya kazi bila kuwa na kundi lolote, ingawa ana ukaribu na wasanii kadhaa akiwa na lengo la kufanya kazi kwa ushirikiano na wasanii waliotangulia na kusoma nyendo zao.

Binti huyo aliyezaliwa mwaka 1987, anasema kwamba anafanya kila awezalo kuhakikisha kuwa anafanikiwa kisanaa, bila kuangalia changamoto gani anakutana nazo katika tasnia ya muziki huo nchini na yenye mafanikio mengi.

Lady Black anasema kwamba maisha ya sanaa yanahitaji uvumilivu wa aina yake, ikiwamo wakati mwingine kuonekana muhuni kutoka kwa baadhi ya watu wanaoamini kuwa sanaa inatakiwa ifanywe na wanaume na si wanawake.

Licha ya kuanza zamani kupenda muziki, lakini mwaka 2008, kipaji chake kilizidi kushamiri pamoja na kupata hamu ya kufanya kazi ya muziki kwa mafanikio makubwa, akiwa na lengo la kuonyesha makali yake.

Anasema anashukuru kwa kuweka mkazo katika suala hilo, nyota yake imezidi kukua kiasi cha kuanza kuona dalili njema katika maisha yake ya sanaa, hasa kwa kufanikiwa kuingia studio na wimbo wake kupigwa katika vituo vya redio.

Dada huyo anasema kwamba muziki wa kizazi kipya unalipa hasa kwa wasanii wanaojitambua na wenye uwezo wa kufanya kazi kwa umakini, hivyo anaamini kwa upande wake atafikia malengo yake ya kuwa msanii nyota.

Anasema katika hilo anafanya kazi kubwa ya kuhakikisha anawaweka mashabiki wake katika mtego wa kuona hawawezi kuwa mbali na yeye, kutokana na utunzi wa nyimbo zake zote zitakazofuata.

“Muziki ni mzuri lakini ni ngumu sana kuendelea kuwa juu kama mtu anashindwa kutunga nyimbo nzuri, ndio maana kuchelewa kwangu kuibukia katika sanaa ya muziki wa kizazi kipya, nimejifunza mambo mengi mazuri kwa ajili ya sanaa yangu.

“Naamini katika hili mambo yatakuwa mazuri, maana kwa kutunga nyimbo nzuri pamoja na aina ya uimbaji wangu, wadau wataniunga mkono na kunifikisha mbali, ukizingatia kuwa msanii anahitaji mipango ya hali ya juu,” alisema.

Mwanadada huyo anasema kwamba licha ya kuweza kuimba kwa utundu na kughani mashairi yake, pia ana uwezo wa kucheza, akikumbukia wakati wa uwepo wa ma-camp  mengi na kutembelea kwa ajili ya kuonyesha makali yao.

Anasema kuingia kwake kwenye camp ni kutafuta namna ya kutoka kisanaa, akisema wakati huo kila camp lilikuwa likialikwa na wenzao pamoja na kutoa nafasi ya wasanii kupanda jukwaani kuonyesha cheche zao.

Lady Black anamalizia kwa kuwataka wadau na mashabiki wa muziki wa kizazi kipya hapa nchini kukaa makini na kusubiria nyimbo zake, akiamini kuwa ni nzuri zitakazowapatia shangwe na amani katika mioyo yao.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...