https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, December 24, 2012

DC Handeni akemea mkaa kupangwa barabarani


Mkuu wa wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu, akiangalia mkaa ulivyopangwa kando ya barabara ya Mkata Handeni.

Na Rahimu Kambi, Handeni
MKUU wa wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, amewataka watu kuacha kupanga mkaa barabarani ili waweze kuilinda barabara hiyo inayotoka Mkata kwenda Handeni.

Muhingo aliyesema hayo hivi karibuni aliposhuka kwa ajili ya kuwaelimisha wananchi hao wanaofanya biashara hiyo inayoweza kuhatarisha usalama wa barabara hiyo.

Akizungumza na Handeni Kwetu, alisema ingawa juu ya biashara ya mkaa ipo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini ofisi yake inaingilia kati kwa kuwataka watu hao kuacha kupanga bidhaa zao barabarani.

Alisema yeye kama Mkuu wa wilaya ya Handeni anazuia kupanga mkaa, maana unaongoza kuharibu kuta za barabara hiyo iliyojengwa kwa ajili ya kuharakisha maendeleo yao.

“Nawaomba jamani mnapokuwa kwenye biashara hii hakikisheni bidhaa zenu hazipo barabarani kwa ajili ya kuilinda barabara hii nzuri kwa ajili yetu.

“Tusipokuwa makini, barabara itaharibika mapema wakati hata kukabidhiwa bado, hivyo naomba tuelewane katika hili, japo najua mpo kimakosa mnapofanya biashara hii ya mkaa,” alisema Muhingo.

Kujengwa kwa barabara ya Mkata Handeni kumepokelewa kwa furaha na wakazi wengi wa Handeni, hasa wa maeneo korofi ya Kwachaga ambayo mvua inaponyesha kidogo tu, magari hukwama na kushindwa kuendelea na safari zake.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...