https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, December 21, 2012

Nyuki inavyoweza kupunguza umasikini kwa Tanzania



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

Hiyo ndiyo inayoweza kuleta elimu ya dhati kwa raia wake, ili wajiingize kwenye sekta hiyo ya ufugaji nyuki na asali kwa ujumla, ikiwa ndio njia ya kuwapatia maisha bora kwa kila Mtanzania.
Mama Gladness Mkamba, kulia akiangalia nyuki wadogo wanavyotengeneza asali katika mzinga wao.

Ni kutokana na hilo, jamii inazidi kuelewa jinsi ya ufugaji nyuki. Baadhi yao wanajiingiza humo, wakiamini maisha yao yanaweza kuwa mazuri.

Hata hivyo, katika ufugaji wa nyuki, zipo dosari ama changamoto nyingi, ukizingatia kwamba wengi wao wanaogopa wadudu hao.

Katika muendelezo wa kutoa elimu kwa Watanzania, Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Ufugaji wa nyuki, kwa kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, Gladness Mkamba, anasema kwamba fursa ya uwekezaji katika ufugaji wa nyuki ni jambo la lazima ili zao hilo liwe na faida kwa jamii nzima.

Anasema uanzishwaji na usimamizi wa viwanda vinavyojikita katika shughuli za ufugaji nyuki na biashara ya mazao ya nyuki kunaweza kuiingizia nchi kipato kikubwa na kuondoka kwenye umasikini.

Nchini Tanzania kuna fursa nyingi sana za uwekezaji katika sekta ya ufugaji nyuki hasa katika nyanja zifuatazo ambazo ni viwanda vya kutengeneza vifaa vya ufugaji wa nyuki, ambavyo ni mizinga ya nyuki, mavazi ya kinga, mashine ya kukandamiza na ya kukamulia asali, vifaa vya kuhifadhia asali na vifaa vya kuchujia nta.

Pia alivitaja viwanda bidhaa zitokanazo n anta ambavyo vinajumuisha shughuli za biashara kama vile, utengezaji wa mishumaa, matumizi ya nta kama kiambato muhimu katika dawa, vipodozi, mafuta ya kulainishia mitambo, polishi na mengineyo.

“Pia viwanda vya bidhaa zitokanazo na asali kwa kutengeneza pombe, mvinyo, kiambato muhimu katika dawa, kikolezo kitamu katika maji matatu ya matunda/juisi, mikate, biskuti, na uhifadhi wa chakula.

“Aidha kuna uchavushwaji unaofanywa na nyuki na kuboresha mazao yatokanayo na mimea ya kupanda mashambani na mimea ya asili, ukizingatia kwamba nyuki ni wazuri katika uboreshaji wa wingi na ubora wa matunda na mbegu,” alisema Gladness.

Mkurugenzi huyo msaidizi wa nyuki anasema kwamba bidhaa hiyo pia hutumika kama pembejeo katika mashamba kwa kuongeza uchavushaji wa mimea ya asili na ya kupandwa mashambani.

Anatolea mfano jinsi makundi ya nyuki yanavyoweza kukodishwa na wakulima ili yachavushe mimea kama alizeti, machungwa, maharage, mabohora/mapesheni na mahindi.

Katika nchi zilizoendelea katika mifumo yao ya kilimo kama Marekani hutumia nyuki katika ushavushaji na huku mazao wanayopata yakiwa na thamani ya mara kumi ya thamani ya asali na nta.

Gladness anasema kwamba uanzishaji na uendelezaji wa Hifadhi za Nyuki kwa ajili ya utalii ikolojia na uhifadhi wa makundi ya nyuki, pamoja na mimea ya chakula chao na maabara za kupima viwango vya mazao ya Nyuki
Wawekezaji, wahisani, taasisi na mashirika mbalimbali wanahamasishwa kuwekeza katika kuanzisha maabara za kupima ubora wa asali na mazao mengine ya nyuki ili kudhibiti viwango vya ubora wa mazao hayo.

Aidha anasema kwamba ufugaji na uuzaji wa makundi ya nyuki hukamatwa na kuwekwa kwenye mzinga na kisha kuuzwa kwa wafugaji wa nyuki, huku bei ya makundi ya nyuki wanaouma ni kati ya shilingi 40,000 hadi 50,000 kutoka kwa mfugaji na wale wasiouma wakifikia Sh. 50,000 hadi 70,000.

Biashara hii imeweza kuwaongezea kipato wafugaji wengi hasa wale wanaouza makundi ya nyuki wasiouma, hivyo kuweza kujimudu kimaisha na kusogeza mbele uchumi wa Taifa.

Uendelezaji wa sekta ya ufugaji nyuki utaleta manufaa mengi wa kuongeza pato la Taifa, kuongeza ajira, na kipato kwa wananchi  kutokana na mazao ya nyuki na ya kilimo pia kuboresha mazingira.

Kwa mujibu wa Gladness, endapo kutakuwa na wafugaji 1,500,000 ambao watajiajiri kwenye ufugaji nyuki na kuwa angalau na mizinga 50 kila mmoja, mchango wa ufugaji nyuki unaweza kutambuliwa katika kuchangia na kupunguza umasikini kwa uchumi wa nchi.

Wakarti mchango wa asali ukiwa Sh. 1,250,000,000 kwa mwaka, mchanago w anta kwa wafugaji wa nyuki kinafikia 371,250,000; sawa na USD 247.50, hivyo basi jumla ya kipato cha mfugaji kwa mwaka kutokana na makundi 50 kikiwa Dola za Kimarekani 1,747.50.

“Tungeweza kuongeza kiasi cha asali tunachouza nchi za nje cha tani 379 za nta na tani 275 za asali  kuwa  tani  4,560 za nta zenye thamani ya Dola 15, 960, 000 na  tani 6,600 za asali zenye thamani ya  Dola 9, 900, 000, Taifa linaweza kupata kiasi cha Dola 25,860,000 kutokana na mauzo ya mazao ya nyuki nje ya nchi na kukuza uchumi wetu.

Changamoto tuliyonayo ni udhibiti wa ubora wa mazao ya nyuki na uzalishaji wa kibiashara, huku tukiwaomba Watanzania wajikite kwenye sekta hiyo ya ufugaji nyuki kwa faida yao pia,” alisema Gladness.
Anasema mazao ya nyuki nchini Tanzania huwa na ubora wa hali ya juu yanapokuwa hayajavunwa kutoka kwenye mzinga.

Kutokana na sababu hiyo, yanaweza kupata soko lenye bei ya juu kama ubora wake utadumishwa.

Hata hivyo wazalishaji bado hawajatilia maanani viwango vya ubora vinavyohitajika kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi na kusababisha mazao hayo kuuzwa kwa bei ndogo.

Kutokana na tatizo hilo, mwongozo  umetolewa na Idara ya Misitu na Nyuki kulingana na Sehemu ya III ya Kanuni za Jumla za Ufugaji Nyuki za 2005, ili kuelekeza uhakiki wa ubora wa mazao ya nyuki, lengo likiwa ni kuweka mpango madhubuti wa sekta hiyo ya asali na nyuki.

kambimbwana@yahoo.com
0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...