Katibu wa Mbunge wa Handeni, Salumu Masokola pichani
Na Rahimu Kambi, Handeni
KATIBU wa Mbunge wa Handeni, Salumu Masokola, amesema kwamba
mkakati uliopo sasa ni kuhakikisha kuwa wanaweka mipango madhubuti ya kuwapatia
maji wakazi na wananchi wa Handeni.
Masokola ambaye ni Katibu wa Abdallah Kigoda, mbunge wa
Handeni, alisema mikakati hiyo itakwenda sambamba na kupatikana visima 500
vitakavyochimbwa katika baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo.
Akizungumza na Handeni Kwetu mjini hapa, Masokola
alisema kwamba visima hivyo vitachimbwa, ikiwa ni mikakati ya kukabiriana na
shida ya maji inayoendelea kuwasumbua wakazi na wananchi wa Handeni.
Alisema mbunge wao anajua kuwa Handeni kuna matatizo ya maji
kutokana na kutokuwa na vyanzo vya maji vya uhakika, lakini kwa bidii yake
amekuwa akihangaikia suala hilo
kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu wa Handeni.
“Handeni ina kero kubwa ya maji kwasababu hakuna vyanzo vya
maji vya uhakika, ila kuna mpango wa kuchimba visima 500 vitakavyogawanywa kwa
kwa watu wa eneo la Handeni, hivyo kupunguza kama
sio kuimaliza kabisa shida ya maji.
“Tunaamini mpango huo ukifanikiwa, wananchi wa Handeni
wataishi maisha yenye amani, ukizingatia kwamba kwa sasa wimbo umekuwa ni shida
ya maji na watu wanahangaika sana,
hasa baada ya maji kupatikana kwa tabu,” alisema.
Kwa mujibu wa Masokola, endapo visima hivyo vitachimbwa haraka
iwezekanavyo, vitagawanywa katika maeneo ya Handeni pamoja na vijiji vyake,
ukiwa ni mpango utakaoleta amani kwa wakazi na wananchi wa Handeni.
No comments:
Post a Comment