SIWEZI KUVUMILIA
Mlinda mlango wa Simba, Juma Kaseja.
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WATANZANIA hatuwezi kuendelea kama hatutakuwa na mapenzi
mema na timu zetu zote na sio kuegemea zaidi kwa timu kongwe za Simba na Yanga.
Kauli hii naisema leo ambapo najua ligi hatua ya mzunguuko
wa pili imeanza, huku timu 14 zikiwania taji hilo linalodhaminiwa na Kampuni ya
Simu za Mikononi ya Vodacom Tanzania.
Ndio ukweli huu, maana nimeshindwa kuvumilia kuona baadhi ya
timu zetu zinazoshiriki ligi mara kadhaa kucheza na majukwaa, huku mashabiki
wakiangalia zaidi timu kongwe.
Hii sio njia nzuri, maana wakati mwingine zinawakosesha
mapato kwakuwa kabla ya mchezo husika, timu hizo hutumia gharama kubwa
kuwaandaa wachezaji wao.
Kama hivyo ndivyo, timu hiyo inayotegemea mapato ya
milangoni, zitajiendeshaje? Hii ni tofauti na nchi zilizoendelea. Huko kila
shabiki anakuwa kama kichaa kwa kuipenda zaidi timu yake sambamba mpira wa
miguu kwa ujumla.
Kuna watu ambao wanachoangalia wao ni Yanga na Simba tu.
Timu ya African Lyon yenye maskani yake jijini Dar es Salaam, haiwezi kuendelea
kwa kutunisha mfuko wao, hadi icheze na Yanga au Simba.
Timu ya Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Azam FC, Coastal Union
lazima ziungwe mkono zinapokutana zenyewe kwa kuhakikisha kuwa mashabiki
tunajaza viwanja.
Najua hali ni ngumu kwa kila mmoja wetu, lakini si sahihi
pia kujidanganya kwamba soka lipo kwa watani wa jadi, Simba na Yanga peke yao.
Huo ndio ukweli wa mambo, maana kadri siku zinavyozidi
kwenda mbele, mahitaji ya kuendeleza timu zetu za mpira wa miguu yanazidi kuwa
makubwa na magumu.
Michezo ni pesa inayolipa, lakini si kwa mtindo huu
unaoendelea wa Watanzania kuona ili nafsi zao zinakuwa na raha zaidi kwa
kuwaangalia watani wa jadi.
Sikatai, upenzi wa timu hizo hauwezi kufutika, ila shabiki
wa kweli wa soka hawezi kukosa uwanjani kwa namna moja ama nyingine. Watanzania
tujenge mapenzi na timu zetu.
Huko kuangalia Simba na Yanga, kumetupambaza kiasi kwamba
hatuangalii mafanikio ya Taifa. Katika mzunguuko wa kwanza wa ligi hiyo, kuna timu
zimegawana kiasi kisichozidi elfu 50,000 kama mapato ya uwanjani.
Angalia hasara hii. Fedha hizo zinaweza kweli kuwatoa Tanga,
kama ni Coastal Union na kuwapeleka Bukoba kucheza na Kagera Sugar, zaidi ya
kutafuta nauli kwa njia nyingine?
Tanzania ni yetu wote. Ili isonge mbele tunahitaji kuwa na
akili mpya, hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi,
kimichezo na kijamii.
Tukiangalia soka la Simba na Yanga pekee hatuwezi kwenda,
maana timu hizo zimekuwapo kwa miaka mingi na bado hakuna cha maana zaidi ya
kushuhudi migogoro, matusi, kejeli na fitina za kila aina zinaposukwa njama za
kila aina, iwe kuupinga uongozi uliokuwapo madarakani na mengineyo.
Tujaribu kuweka karata zetu kwa timu zote za Tanzania ili
zione tahamni ya Watanzania katika hali ya kufanya mapinduzi makubwa katika
sekta ya mpira wa miguu.
Wakati nasema hayo, nakumbuka kuwa Tanzania mwaka huu katika
mashindano ya Kombe la Shirikisho inashiriki timu ya Azam FC, ambayo kwa hakika
ina mipango kabambe ya kuweza kutangaza soka la nchi hii kwa waliopiga hatua.
Azam inashiriki mashindano hayo baada ya mwaka jana kushika
nafasi ya pili katika ligi ambayo Simba ilinyakua ubingwa huo, hivyo yenyewe
kupata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ni Azam hii ambayo baadhi yao wanaiangalia vibaya, wakiona
haina cha maana, hata pale wanapoangalia mafanikio yao waliyopata katika
kipindi kifupi mno.
Katika hilo, hakika siwezi kuvumilia, hivyo wadau wa
michezo, hasa wa mpira wa miguu tuna kila sababu ya kuangalia juhudi zetu
katika hali ya kukuza soka letu.
Sitaki kusema kwamba tusipende timu za Simba na Yanga, maana
wengineo ndio imani zao, lakini tupende michezo kwa ujumla, kwa kuingia
uwanjani kihalali ili mapato yaweze kuendesha timu hizo zinazotegemea mapato.
Vinginevyo, Simba na Yanga zetu, zitazidi kuathiri kiwango
cha mpira wa miguu, maana zenyewe zinajiweza kwakuwa na rasilimali fedha na
watu, hivyo kuweza kufanya lolote, ikiwamo kununua mechi kwa timu zinazopoteza
mwelekeo kwa kukosa bajeti.
0753 806087
No comments:
Post a Comment