Banza Stone anavyoonekana sasa Extra Bongo.
Huyu pia ni Banza Stone, alipotoka kuumwa.
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WADAU wa muziki wa dansi hapa nchini, wamepongeza maendeleo
ya afya ya mwanamuziki nguli, Ramadhani Masanja Banza Stone, anayefanya kazi na
swahiba wake, Ally Choki, katika bendi ya Extra Bongo, Next Level.
Banza Stone alikuwa kwenye matatizo mengi ya kiafya, hali
iliyowafanya baadhi ya watu wenye roho nyepesi kumzushia kifo kutokana na hali
yake.
Hata hivyo, baada ya kuitwa na Choki katika bendi hiyo,
Banza Stone amekuwa kwenye kipindi kizuri cha afya yake kuimarika, jambo
linaloleta tumaini kubwa.
Mtu wa karibu na bendi hiyo, aliiambia Handeni Kwetu juzi katika bonanza lao linalofanyika kila Jumapili, Magomeni kuwa
wamekuwa wakimshauri sana mwanamuziki huyo ajilinde na matumizi mabaya ya ulevi
hali itakayomuweka njia panda.
“Afya yake inachangiwa na ulinzi anaopewa pamoja na ushauri
hapa Extra Bongo, ukizingatia kwamba hapo kabla alikuwa kwenye wakati mgumu
kiasi cha kutabiriwa kifo.
“Hata yeye mwenyewe alishakata tama, lakini kwa mwendo huu
mambo ni mazuri, maana ana nguvu zake pamoja na uwezo wa kupaza sauti katika
shoo za Extra Bongo,” alisema mpashaji huyo.
Banza Stone anakumbukwa na uwezo wake wa utunzi na uimbaji,
huku wadau wakikumbuka jinsi alivyofanya mambo katika nyakati mbalimbali, hasa
kipindi cha kuwika kwa Choki, Mwinjuma Muumini nay eye mwenyewe.
Banza pia amewahi kuwika na bendi mbalimbali, kama vile The
African Stars, Twanga Pepeta, TOT na nyinginezo alizojiunga nazo katika kipindi
chote cha maisha yake ya muziki na kutoa vibao mbalimbali kama vile Mtu Pesa,
Kisa cha Mpemba, Majungu sio Mtaji na nyinginezo.
No comments:
Post a Comment