Picha juu na chini ni mwandishi wa habari za michezo wa gazeti la Bingwa, Dimba na
Mtanzania kutoka Kampuni ya New Habari 2006 Ltd, Sharifa Mmasi pichani
akisoma kitabu cha Dira na Tumaini Jipya Handeni kilichoandikwa na Kambi
Mbwana, ambaye ni Mratibu Mkuu wa Tamasha la Handeni Kwetu
linalofanyika kila mwisho wa mwaka wilayani Handeni, mkoani Tanga. Picha
na Mpigapicha wetu.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWANDISHI wa Habari za Michezo ambaye pia ni Mratibu Mkuu wa
Tamasha la Utamaduni la Handeni Kwetu, Kambi Mbwana, ameandika kitabu chake kinachojulikana
kama ‘Dira na Tumaini Jipya Handeni’, kilichoanza kupatikana mapema wiki hii jijini
Dar es Salaam na wilayani Handeni, mkoani Tanga.
Kitabu hicho kimeelezea kero na changamoto mbalimbali za
wananchi wa Handeni, kama vile shida ya maji, elimu na migogoro ya ardhi kwa
ajili ya kushirikisha mawazo ya viongozi wa serikali, wadau na wananchi ili kukabiliana
na tatizo hilo wilayani humo na mikoa ya jirani ambapo changamoto hizo
zinashabihiana kwa kiasi kikubwa.
Sharifa Mmasi akisoma kitabu cha Dira na Tumaini Jipya Handeni, kilichoandikwa na Kambi Mbwana.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mbwana alisema kwamba
kuandika kitabu hicho kuna lengo kubwa la kuelimisha jamii kwa ajili ya
kutafuta fursa ya kimaendeleo katika wakati huu ambao wananchi wengi wamekuwa
wakilia bila kupata msaada wowote.
“Naijua vizuri wilaya yangu ya Handeni na mkoa wa Tanga kwa
ujumla, hivyo nimeamua nitumie kipaji change katika kuandika kitabu hiki
ambacho kimeweza kuanika mambo mengi yenye tija kwa serikali na wananchi kwa
ujumla, hivyo naomba waniunge mkono kwa kuhakikisha kwamba wanapata kitabu hiki
popote kitakapokuwapo.
Kinapatikana kwa bei ndogo mno ya Sh 3500 kwa kuwa sikuwa na
lengo la kutajirika kwa kupitia kitabu hiki bali kutoa mawazo yangu na
kuelimisha jamii yangu inayonizunguuka, hivyo ni wakatai wa Watanzania wote,
bila kusahau wakazi na wananchi wa Handeni kupata nafasi ya kusoma mawazo yangu
kwa ajili ya kutafuta namna ya kufika mbali kiuchumi na kiutamaduni,
ukizingatia kuwa kitabu kimegusia mambo kadhaa ambayo ni muhimu,” alisema
Mbwana.
Kwa mujibu wa Mbwana, maeneo yanapopatikana kitabu hicho kwa
jijini Dar es Salaam ni pamoja na ambapo ni Kinondoni Kwa Manyanya, kwenye
kituo cha basi kwa muuza magazeti aliyekuwa pembeni ya ghorofa la Mwaulanga, Sinza
Kijiweni kwenye studio inayoangaliana na lango la New Habari 2006 Ltd, upande
wa wanaokwenda mjini, huku studio hiyo ikiwa karibu na duka la vifaa vya
ujenzi. Maeneo mengine ni muuza magazeti wa Kimara Mwisho kwenye kituo cha basi
cha wanaokwenda mjini, huku Buguruni kikipatikana katika studio ya upigaji wa
picha karibu na Hoteli ya New Popex, Buguruni, jijini Dar es Salaam.
Aidha Mbwana alisema kwa wanaotaka kuwasiliana naye juu ya
kitabu hicho cha Dira na Tumaini Jipya Handeni wanaweza kumpata kwa +255 712053949
au barua pepe; kambimbwana@yahoo.com.