Fatuma Rashidi, mkazi wa kijiji cha Komsala.
Na Rahimu Kambi, Handeni
WANANCHI wa kijiji cha Komsala,
wilayani Handeni, mkoani Tanga, wapo kwenye shida ya maji kwa wiki moja sasa,
baada ya miundo mbinu inayopeleka maji katika kijiji hicho na vinginevyo vya
Kata ya Kwamatuku, kubomolewa na mzinga wa baruti kutoka kwa Wachina
wanaotengeneza barabara ya kutoka Korogwe kwenda Handeni.
Mkuu wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu
Wachina hao ni wale walioweka
kambi katika mlima wa mawe wa kijiji cha Komsala, huku wakiendesha shughuli za
kuvunja mawe na kokoto kwa ajili ya kutengenezea barabara hiyo.
Akizungumza na Handeni Kwetu,
mkazi wa kijiji cha Komsala, ambaye pia anafanya biashara ya maji, Fatuma
Rashidi, alisema mara baada ya mzinga huo kusikika, maji yalikatika.
Alisema baada ya kufuatilia
nini tatizo, waligundua kuwa mabomba yanayosambaza maji yalipasuka, hivyo
kusababisha maji hayo kumwagika na kuleta shida ya maji.
“Tuna wiki sasa hatuna maji
katika kijiji chetu kutokana na matatizo hayo ya kiufundi, hivyo tunaomba
wahusika ambao ni (HTM), Idara ya Maji ya Korogwe waje kutatua tatizo hili.
“Inawezekana hawajui, lakini
hawa wenzetu wanaotengeneza barabara ndio wanaodaiwa kupasua mabomba maana
mzinga wao wanaopasua mawe huwa mkubwa mno,” alisema.
Juhudi za kupatikana kwa
msemaji wa Wachina hao zilishindikana, baada ya simu ya mkubwa wao
anayejulikana kwa jina la Lee kutopatikana.
Kijiji cha Komsala kinatumiwa
na Wachina kwa ajili ya kupatikana mawe kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya
kutengeneza barabara hiyo ya Korogwe Handeni, ujenzi unaoendelea hadi sasa.
No comments:
Post a Comment