Na Kambi
Mbwana, Dar es Salaam
HATA vitabu
vya dini vinatueleza binadamu tuzitii mamlaka halali tulizochagua wenyewe ili
zituongoze. Ndio, inapotokea mtu anakwenda kinyume na maandiko hayo, ni dhahiri hatufai, hastahili kuchekewa.
Kambi Mbwana, mwandishi wa makala haya.
Na kutii
huko hakupo kwa mwananchi wa kawaida tu. Maadamu ni mamlaka halali, hapana
shaka kila Mtanzania wa nchi yetu anapaswa kutii hilo bila kujali dini yake au
itikadi yake ya kisiasa. Kwa bahati
mbaya, tangu kuanzishwa kwa sheria ya vyama vingi, mwaka 1992, kumekuwa na
kasumba ya baadhi ya viongozi wa upinzani, kufanya mambo ambayo ni kinyume,
wakiwa na malengo yao binafsi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr John Pombe Magufuli pichani.
Malengo ya
kutafuta sifa ya kuungwa mkono na wafuasi wao bila kujali wanafanya kitu kizuri
au cha kijinga. Bahati mbaya mfumo huo kadri unavyozidi kupewa nafasi na
wapinzani hao, dalili za wazi za kutowesha amani ya nchi yetu inazidi kuonekana.
Kwanini isionekane? Utawekeje tone moja la damu kwenye nguo nyeupe na bado
ukajindanganya kwamba nguo hiyo itaendelea kuvutia? Pamoja na
dalili ya machafuko inayozidi kuonekana, bado hakuna juhudi zinazochukuliwa na
wanasiasa kutoka mlengo wa upinzani, wakiamini siasa za kumwaga damu za
wananchi wao ndizo zinazoweza kuwaweka juu.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe pichani.
Hili
haliwezi kukubalika. Watanzania
tusikubali. Tumeshahudia mara kadhaa damu za Watanzania wenzetu zikimwagika
bila soni wala haya. Machafuko ya kisiasa yanayoanzishwa na wanasiasa kama
Arusha, Morogoro na katika maeneo mengine yameendelea kuonekana, huku chanzo
chake kikiwa ni siasa chafu, nyepesi, zisizokuwa na tija kupewa nafasi hususan
na chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kwa mfano,
Chama Kikuu cha Upinzani Tanzania (Chadema), kwa kupitia mwenyekiti wao Freeman
Mbowe JUZI wametangaza kufanya maandamano na mikutano nchi nzima katika siku ya
Novemba Mosi. Na mikutano
hiyo itafanyika bila kuangalia imeruhusiwa na jeshi la Polisi au itazuiwa.
Inawezekana kuandamana ni halali kwa mujibu wa Katiba, lakini pia busara na
usalama lazima ziimarishwe kwa faida ya nchi yetu.
Kufanya
maandamano yenye viashiria vya uvunjifu wa amani hakuwezi kuruhusiwa hata kama yamewekwa
kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hii ni kwa
sababu si Watanzania wote wanapendezwa na siasa za upinzani. Wapo ambao
hawaungi mkono agizo lolote la upinzani. Na wengine si wafuasi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wala CUF. Isipokuwa wote ni Watanzania. Hivyo endapo hayo
maandamano yatafanyika bila kufuata sheria, kanuni na taratibu tulizojiwekea,
ni wazi kutakuwa ni kupoka haki ya kuishi na kulindwa kwa wengine watakaoathiliwa
na maandamano hayo yasiyokuwa na kichwa wala miguu, kama wanavyotaka kufanya
viongozi wa juu wa Chadema.
Ndio maana
kunakuwa na taratibu. Nani asiyejua kuwa siasa za namna hiyo zimepelekea kifo
cha Mtanzania mwenzetu, mwandishi wa habari Daud Mwangosi kule mkoani Iringa?
Ingawa
Chadema wanasema mauaji hayo yamesababishwa na Jeshi la Polisi, lakini chanzo
kikuu ni ghasia zilizoendeshwa na wao na wakiwa na nia waliyojua wenyewe,
ikiwamo hii ya kujulikana kwa lazima bila kujali athari kutoka kwa baadhi ya
Watanzania wasiokuwa na hatia. Licha ya kifo hicho au machafuko yaliyotokea
katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, wapinzani wameendelea kutembea katika
njia ile ile, wakiamini ndio mtaji wao wa kisiasa ulipo. Hii
haikubaliki. Watanzania tusikubali siasa za kumwaga damu zinazofanywa na
kuhubiriwa na wanasiasa wa upinzani kwa sababu hazina faida kwetu. Tunachafua
tunu ya Taifa letu.