https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, September 21, 2012

Ukiona uchafu, huwezi kumuenzi mwenzi wako






MAMBO FULANI MUHIMU



Na Kambi Mbwana, Dodoma
MAPENZI ni jambo ambalo linaleta hisia mbili tofauti. Mosi; mapenzi yanaweza kukufanya uishi kwa raha kama mfalme. Pili, mapenzi hayo yakibadilika hukufanya uwe kama chizi.

Jambo hilo zuri linalofananishwa na sukari kwa yaliyowakalia vizuri, hubadilika na kuwafanya baadhi yao waone ugumu wa kuendelea kuishi, maana wanaowapenda wanawasumbua kwa kiasi kikubwa.

Ni kutokana na hilo, jamii inashauriwa kuwa makini katika suala hilo. Wasijaribu kukurupuka na kuchukua uamuzi wenye mashaka kwa namna moja ama nyingine, maana vinginevyo watatamani kujinyonga.

                                                     Kambi Mbwana


Hata hivyo, pamoja na yote hayo, lakini inajulikana wazi wazi kuwa dawa kubwa katika uhusiano wa kimapenzi ni kumfikisha mwenzako, kumuweka katika kilele cha ubora katika ulimwengu wa mapenzi.

Katu usiangalie umbo lako, sura yako katika kujigamba kwamba unaweza kupendwa na yoyote, wakati ni mzigo kitandani. Kama huna ujuzi katika suala la mapenzi, ondoa kupendwa, kuhitajiwa au kugandwa na yoyote.

Zaidi ya hapo, wachache wao watakupitia na kuchukua hamsini zao, maana huna ujanja wa kumuweka mwenzako katika furaha. Hivyo basi, ili jamii iwe kwenye ramani nzuri na furaha ya mapenzi, lazima tuwajulie watu wetu.

Tufahamu namna ya kuwachanganya kisaikolojia, bila kuangalia uzuri wetu, fedha zetu, maana hizo haziwezi kufanya penzi liwe na amani.

Wapo ambao wanaishi na wanaume wenye nazo kupita kiasi, lakini bado wake zao, wachumba zao au wapenzi wao wanajiingiza katika uhusiano na watu wa kawaida, wakiwamo wafanyakazi wa ndani.

Hata hivyo haitoshi, wapo pia wakina mama wenye nazo lakini wanachanganywa na wasichana wa kawaida, wenye sura za kawaida au hadhi za kawaida. Wenye mali zao wanalia na kusaga meno.

Wanasema“Hivi kwani mume wangu unatembea na yule mfanyakazi wa ndani wakati mimi nipo” Au sielewi unachofuata kwa yule kijana mchunga mbuzi wakati mimi nipo, tena mwenye fedha za kutosha tu”

Kama wewe ni miongoni mwa watu wenye mtazamo huo umeliwa. Fedha sio kila kitu katika mapenzi. Fedha zako usipoangalia zinaweza kuwanufaisha wapita njia, wajuzi wa mambo kwenye mambo fulani muhimu.

Huo ndio ukweli wa mambo. Mjuzi huyo hatafutwi ili mradi mtu ana mtu wa nje, ila umuhimu wake unakuja anapokuwa kwenye ulingo. Hayo lazima mimi na wewe tuyajuwe kwa ajili ya mapenzi yetu.

Unapokuwa na mpenzi wako, mume au mke wako lazima ujuwe yupo na wewe kwa ajili ya kujenga maisha ya wawili. Ili mwenzako afurahie uwepo wako, hakikisha kuwa walau unatumia muda wako hata kama kidogo kumridisha kimapenzi.

Kwa wale ambao kwa miaka mingi wameishi na wapenzi wao bila kutumia ujuzi wao, waanze leo. Na wale wanaoingia kwenye uhusiano leo, pia wawaangalie watu wao, namna gani walivyo na wanastahili aina gani ya mapenzi.

Ninaposema mapenzi, sio yale ya kukaa pamoja, kutembea pamoja au kumpigia simu kila baada ya dakika kumi. Mapenzi, tendo la ndoa lenye ujazo mkubwa linalostawisha uhusiano wa wawili wapendanao.

Hivyo basi tuwe makini katika kazi hiyo. Tukitaka kuwapa raha kweli wenzetu lazima tuache kazi na kufanya kazi. Tendo la ndoa sio mchezo mdogo. Sio kama kuwasha njiti ya kibiriti mahala palipotulia.

Inahitaji kusumbua akili na kusumbua pia mwili wako. Sina maana kama nataka muda wote muwe kwenye tendo la ndoa, ila mnapotaka kufunja amri hiyo ya sita, basi mfikishe mwenzako kileleni.

Usimchezee chezee tu ukamuacha. Nimeamua kuandika mada haya maana nimepata malalamiko mengi kutoka kwa wanawake. Baadhi ya wasomaji wangu, wamenipasha kwamba waume zao ni watu wa kwenda raundi moja halafu wanaangalia ukutani.

Kwa bahati mbaya, watu hao wanapolala uzungu wa nne, wanakuwa wanawanyanyasa wenzao, kama unavyojua tena gari linapowaka. Hali hiyo inakera kiasi cha kutamani wapiti njia.

Haya nayasema kwa uchungu, maana usaliti mwingi huibuka kama wawili wapendanao hawaridhishani. Kama unaona huna ujuzi wa kumuweka katika kilele mwenzako, tafuta msaada kwa watu.

Kabla ya kuendelea, niseme tu kutokana na aina ya gazeti lako la Mtanzania, tunashindwa kuandika kiundani zaidi mada za mapenzi, badala yake tunakuwa wepesi kujibu maswali yenu kwa kupitia simu au barua pepe.

Tunafanya hivyo baada ya kugundua kwamba watoto wengi nao hujifunza kinachoandikwa kwenye gazeti, jambo linalonifanya niandike kwa kuficha au yale yasiyokuwa ya ndani zaidi.

Tukutane wiki ijayo.

0712 053949
0753 806087

Mwisho


Fiesta ilivyowapagawisha Dodoma na Morogoro




                          FIESTA 2012 DODOMA NA MOROGORO

                                                       AT akiwajibika jukwaani
                                               Linah Sanga, akifanya mambo
                                          Shetta akifanya mambo jukwaaani.
 
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
MASHABIKI wa muziki wa mkoani Dodoma, Septemba 14, walipata burudani za aina yake katika Uwanja wa Jamhuri, lilipofanyika tamasha la Fiesta 2012, lilioanza kutimua vumbi mapema mwezi uliopita, mkoani Kilimanjaro.

Mbali na Dodoma, tamasha hilo pia liliendelea katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, Jumapili ya Septemba 16, huku mashabiki wao wakibaki na hara mtindo mmoja kutokana na tamasha hilo.

Wasanii ambao walitoa burudani katika tamasha la Dodoma na Morogoro ni pamoja na Recho, Dayna, Linah, Mwana FA, Godzilla, Shetta, Stamina, AT, Juma Nature, Diamond, Rich Mavoco na Ben Pol.

Mbali na wasanii hao wanaokubalika hapa nchini, pia wasanii wachanga kama kawaida walianza kutoa burudani katika uwanja huo wa Jamhuri Dodoma, ikiwa ni utangulizi wa tamasha hilo na kiu ya kuibua wasanii wapya.

Burudani hizo zilianza jioni kwa wasanii wachanga kupanda jukwaani kutangaza vipaji vyao katika tamasha linaloingiza watu wengi kwa wakati mmoja, jambo ambalo linasababisha uwanja kujaa pande zote.

Kila msanii mchanga wa Morogoro na Dodoma, walikuwa na shauku ya kufanya vyema kwa kuimba nyimbo moja nzuri, ikiwa ni dalili njema ya kutangaza cheche zao kwa wadau wao katika uwanja huo.

Mara baada ya kumaliza kwa taratibu za burudani za wasanii wachanga, moto ulianza kwa kuwapa nafasi washindi watatu wa Super Nyota, wakiongozwa na Young Killer, mwimbaji mdogo mwenye makali ya kutisha.

Wasanii hao wamewekwa katika tamasha hilo kama sehemu ya kuonyesha cheche zao, baada ya kupatikana katika shindano la kusaka vipaji, ikiwa pia ni utangulizi wa ufunguzi wa tamasha hilo la Fiesta.

Baada ya kumaliza kwa wasanii hao watatu wa Super Nyota, msanii aliyeibukia mkoani Morogoro na wimbo wake ‘Mafungu ya Nyanya’, Mwanaisha Said, maarufu kwa jina la ‘Dayna’ alipanda jukwaani akifanya vitu vya aina yake.

Dayna kwanza aliwatanguliza madansa wake walioingia jukwaani kwa mbwembwe za aina yake, wakicheza na kujipanga kishujaa na kupandisha Bendera ya Taifa ya Tanzania, wakifuatiwa na kupiga wimbo wa Taifa.

Wakati wanakatisha kuimba wimbo huo, Dayna alipanda jukwaani, akisababisha shangwe kwa mashabiki wengi uwanjani hapo, wakifurahia alivyojipanga katika shoo yake kwenye tamasha hilo.

Alipomaliza kuimba nyimbo zake, ukiwamo ule wa Mafungu ya Nyanya, Nivute Kwako na nyinginezo, mwanadada huyo alishuka na kupanda jukwaani kwa msichana kutoka Tanzania House of Talents (THT), Reyker, akifuatiwa na Rehema Sundi pamoja na Recho, anayetamba na wimbo wake wa Kizunguzungu, Upepo na huu wa Nashukuru Umerudi unaofanya vizuri kwa sasa.

Recho anatamba katika chati za muziki kutokana na umahiri wake wa kushambulia jukwaa, huku akitokea kwenye taasisi hiyo ya kulea na kukuza muziki ya THT, iliyoibua wasanii wengi wenye uwezo wa kutisha.

Mara baada ya mwanadada huyo kumaliza kuimba, alimuachia Ommy Dimpozi kuendelea kushusha burudani. Hata hivyo, Ommy ni kama alipanda kwa mkosi, maana umeme ulisumbua kwa dakika kadhaa.

Cha kushangaza ni kwamba, licha ya umeme kusumbua uwanjani hapo kwa dakika kadhaa, lakini Ommy aliendelea kushangiliwa na wadau kuimba kama kawaida, hivyo kuonyesha kuwa msanii huyo anakubalika kupita kiasi.

Kitendo cha kumaliza kuimba kwa mkali huyo aliyeacha historia mkoani Dodoma, alipanda jukwaani Rich Mavoco, akifuatiwa na Stamina, msanii aliyetingisha uwanja mzima kwenye shoo hiyo.

Wasanii wengine waliofuata kutoa burudani katika tamasha hilo ni Shetta, Ben Pol, Linah, Mwana FA, aliyesindikizwa na AY, ambaye hata hivyo hakuwa kwenye ratiba ya kupanda jukwaani kutoa burudani.

Msanii ambaye pia atakumbukwa ni AT aliyepanda jukwaani mara baada ya kushuka wakali wa Hip Hop na R&B Ben Poli, yeye alipanda jukwaani na kuwashawishi mashabiki wamsikilize na kucheza nyimbo zake.

Wengi katika shoo kubwa kama hizo hushindwa kuwafanya watu wacheze, hasa hawa wa mduara kama AT, anayetokea mjini Zanzibar.

Shoo ya Dodoma ilimalizwa na Juma Nature usiku wa manane, baada ya kumaliza wakali wote, akiwamo Godzilla, mkali mwenye maskani yake mitaa ya Salasala.

Utaratibu kama huo ulionekana pia katika mji wa Morogoro, ambapo mashabiki wengi walionekana kupagawa kabla ya shoo hiyo wakiwachekea wasanii na kujipanga kwa ajili ya kuingia kwenye shoo hiyo.

Hata hivyo, mashabiki walipoingia kwenye uwanja huo wa Jamhuri mjini Morogoro, walikuwa wazito sana kucheza na kupagawa kama ilivyokuwa kwa wakazi na mashabiki wa mkoani Dodoma.

Fiesta inaandaaliwa na Kampuni ya Prime Time Promotion pamoja na Clouds Media Group, likifanyika kila mwaka. Kwa mwaka huu, Fiesta ilianza kutimua vumbi katika mji wa Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Katika kila mkoa wanapofanya shoo hiyo, kunatanguliwa na kazi za kijamii, ikiwamo kutembelea vituo vya watoto yatima na kuwapa misaada ya aina mbalimbali pamoja na kupata fursa ya kubadilishana nao mawazo.

Kwa mkoa wa Dodoma, wasanii na waandaaji wa tamasha hilo walitembelea kituo cha watoto yatima kinachojulikana kama Kijiji Cha Matumaini, kilichoanzishwa rasmi mwaka 2002.

Usiku wa shoo hiyo ulifunguliwa na Mkuu wa Mkoa, Rehema Nchimbi, wakati ile ya Morogoro ilihudhuliwa pia na Mkuu wa Mkoa wake, Joel Bendera, ambapo pia wakuu hao husisitiza suala la amani kwa tamasha hilo.

Mikoa iliyofuata kwa burudani hiyo ni pamoja na Tanga, Musoma mkoani Mara, Shinyanga, Mwanza, Dodoma, Morogoro, huku wiki hii likipangwa kufanyika jana Ijumaa katika mkoa wa Mbeya, wakati kesho Jumapili tamasha hilo pia litafanyika mkoani Iringa, Uwanja wa Samora.

0712 053949
0753 806087

Mwisho




Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
HALI ndani ya Chama cha Mapinduzi CCM, inazidi kuwa mbaya, kutokana na baadhi ya wanachama na viongozi wake, kushindwa kuwekana sawa katika kipindi hiki kigumu. Wapo wapo tu. Kila mmoja anajifanya yeye ni zaidi ya mwenzake.

Wenaonyeshana nani ana sauti zaidi ya mwenzake. Hali hii ni mbaya mno. Maana, wakati wao wakiendelea kulumbana, wapinzani wao wanaitumia nafasi hiyo kujinufaisha, maana siku zote adui yako muombee njaa.

Ndio maana nasema CCM inauliwa na mengi, hivyo ipo haja ya kila mfuasi wa chama hicho, hasa vijana kukaa na kuliangalia hilo kwa mapana. Hatuwezi kuwa na maisha bora kama chama kinachoongoza nchi kinakuwa legelege, ama kinachotawaliwa na migogoro ya kimaslahi kila siku ya Mungu.


Mambo ya aina hiyo, yanasababisha msuaguano hata kwenye baraza la Mawaziri, kwenye ofisi mbalimbali kuwa chungu. Mfano, malumbano ya kimaslahi ya baadhi ya mawaziri wetu, hayawezi kutegua kitendawili cha maisha bora kwa kila Mtanzania. Hali hii ni mbaya mno. Angalia.
Licha ya Waziri Mkuu wa zamani aliyejiuzulu, Edward Lowassa, kutoa wazo la kujenga shule za Kata, lakini leo shule hizo ni kama mtu aliyevaa shati huku sehemu zake za siri zikiwa wazi. Unategemea nini hapo? Mtu gani anaweza kusifia shati zuri lililovaliwa, zaidi ya kucheka kila anapotupa macho yake na kugundua kwamba anayemuangalia hajajistiri?

Hakuna wa kuziendelesha shule hizo, maana anajua fika ni mtaji mkubwa wa kisiasa wa waziri huyo, ambaye kwa hakika bado yupo kwenye kikaango na makundi hasimu ndani ya CCM. Wenyewe wanasema vita ya Urais 2015. Kila mmoja anamsurubu mwenzake kwa faida yake. Pamoja na hayo, Watanzania, hawawezi kukosoa hata yale wenye faida nayo.

Hili la shule za kata, ni kubwa linaloweza kuboresha maisha ya Watanzania, kwa kuhakikisha kwamba watoto wao wanakwenda shule. Ni kwenye shule za kata tu. Nasema hivyo maana wengi wao hawawezi kumudu gharama za shule za binafsi zinazohitaji fedha nyingi.

Wakati hayo yakiendelea, shule za kata zinakabiriwa na changamoto nyingi, ikiwamo uhaba wa walimu, maabara na hata vifaa vingine vya kufundishia watoto wetu. Hapo huwezi kutarajia matokeo mazuri katika shule za kata, zenye maana kubwa na kizazi cha Tanzania, yenye kasumba za kila aina.

Tembelea katika kata, wilaya na mikoa mbalimbali ya Tanzania uone mambo. Hawana upendo. Ubinafsi, umimi ni matokeo ambayo hakika yananiweka CCM mahali pagumu. Haya lazima yasemwe kama kweli tunahitaji kujifanyia marekebisho kwa ajili ya kujiandaa na uchaguzi Mkuu ujao.


Kadri miaka inavyozidi kwenda mbele, ndivyo uchaguzi unavyozidi kuwa mgumu. Idadi kubwa ya vijana wanaona CCM tena sio mahali pao ndio maana wameingia zaidi kwenye vyama vya upinzani. Tena wamevaa upinzani kiasi cha kuwaona wenzao kinyaa, kisa wamebaki kwenye chama tawala.

Hutoa maneno ya kejeli na dharau za aina nyingi, wakiamini chama hicho sio sehemu sahihi na mkombozi wa wanyonge. Tuwaache na mtazamo wao. Lakini, kama wana CCM wenyewe hawatakuwa tayari kwa mabadiliko ama maono ya mbali, hakika hawawezi kufanya lolote katika mabadiliko haya.

Chama kitaanguka, maana wao wenyewe wamekubali kife. Tena wapo watakaotembea kifua mbele, wakijisifia kukiangusha kabla ya kuhamia upande mwingine wakipokelewa kwa shangwe kwa kukamilisha kazi waliyotumwa.

Huo ndio ukweli wa mambo. Kama sio ukweli, basi upo mbali na uongo. Upo wapi ukweli halisi wa muanzilishi wa Chama cha Kijamii (CCJ)? Je, sio kweli kama wengi waliokuwa ndani ya CCM ndio waanzilishi wake? Kama ni kweli, hao unategemea wana mapenzi mema na chama chao, kiasi cha kukiombea mema?


Unafiki wa aina hiyo ndio sumu. Niliwahi kusema katika makala zangu huko nyuma, hasa lile la mfanyabiashara maarufu, Mustafa Sabodo, kumwaga fedha zake kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), huku akijifanya ni mwana CCM damu.

Wapo walioniunga mkono na walionitukana ama kuniparua kadri walivyoweza wao hawakukosena. Nakubali kukosolewa kama name ninavyowakosoa wenzangu, maana huo ndio uungwana unaotakiwa katika Dunia ya leo. Yale makundi yasiyokuwa na tija ndani ya chama yakomeshwe, ili kama ni kulia tulie wote.

Na wale ambao wamekosa mapenzi mema na chama chao, ni wakati wao kuondoka, ili wachache wanaobakia wakijenge chama chao. Waswahili wamesema akheri ya ndege mmoja mkonono kuliko ndege kumi mtini.

Kujisifia una wanachama wengi, wakati ni wanafiki, ni wafitina, wazandiki, huko ni kutwanga maji kwenye kinu. Mengi yanasemwa, ila yanamezewa tu. Wapo ambao wametembea kwa furaha mara baada ya Sioi Sumari kukosa

Ubunge katika Uchaguzi Mdogo wa Arumeru Mashariki. Bado hao utawaita ni wana CCM? Kwalipi? Mapenzi yao kwa chama yapo vipi? Hao hao ndio wanaofanya mambo kinyume, wakitoa siri ya chama hadharani kwa ajili ya kujenga mtandao kwa watu, bado nao ni wana CCM?

Inauma sana. Chama sasa kimebaki kama mti mkavu ambao umeliwa ndani na kubaki magome tu. Ni dahiri utaanguka. Kama sio leo basi kesho. Kitu gani cha kuufanya usianguke? Mbona umeshakwisha kwa kuliwa na mchwa watu, usiku na mchana?

Kulisema ama kuliona hili bado kunahitaji elimu ya Chuo Kikuu? Nani anayefurahishwa na hali inayoendelea ndani ya chama? CCM leo imebaki kidogo tu kuanguka. Na wale wenye mapenzi mema ndio watakaoumia, maana wenzao, wale wanafiki watahamia kwenye vyama vyao walivyoanzisha, ama vilivyoanzishwa na wale wanaofanana nao.

Wamebaki wana CCM usoni wakivaa skafu na kofia, wakati mioyoni mwao ni wapinzani wa kutupwa, ndio maana hawapendi kuona wanapatana, wanafanya kazi pamoja. Ni roho ngumu tu, ila hata leo hii, Mwenyekiti wao, Jakaya Kikwete, ambaye pia ni Rais wa Jamhuli ya Muungano wa Tanzania, angeinua mikono juu na kusema ameshindwa.

Anashindwa kufanya hivyo, akikumbuka imani kubwa kwa Watanzania juu yake, hivyo anajipa moyo wa kuendelea na mapambano. Hii ndio Tanzania ya leo. Hii ndiyo CCM ya Muasisi wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kizazi kipya cha leo.

Mbele za watu wanasema kidumu chama cha Mapinduzi, wakati vichochoroni wanasema watajuta kutufahamu. Katika hili, waungwana wamekubali kuiua CCM, wakiona kupo watakapokimbilia. Tukutane wiki ijayo.

kambimbwana@yahoo.com

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...