NIANZE kwa kukushukuru wewe uliyepata nafasi ya kusoma kazi zangu, ikiwamo hii inayoelezea mambo ya uhusiano na maisha, yanayogusa hisia za wengi duniani.
Nasema hivyo maana suala la uhusiano ni zito kuliko inavyochukuliwa na baadhi ya watu. Baadhi yao wanafikiri kuwa wakiachana na waume zao leo, basi kesho atapata mwingine.
Sawa, ila sio jambo zuri. Sio njia nzuri katika maisha yako. Ni tabia mbaya inayotakiwa ipingwe na wote. Utajisikiaje ukiwa na umati wa watu ambao uliwahi kuwa na uhusiano nao?
Sio ajabu unaweza kuonekana wewe ni muhuni, maana kwanini uachwe na waume zaidi ya watano? Kwanini? Kuna nini hapo? Je, wewe ndio tatizo au mwenzako?
Haya ni maswali tunayotakiwa kujiuliza wote kwa pamoja ili kulinda ndoa zetu au uhusiano sisi wote. Msomaji wangu mpendwa, binadamu wengi tabia zao hufanana japo sio sana .
Japo kuwa kuna tabia mbaya na nzuri, ila mwisho wa siku, kwako wewe zinaweza kuwa kero. Hivyo, ukiona mwenzako anakwenda njia tofauti, unaweza kumuweka chini.
Lakini sio sababu ya kuvunja uhusiano wako haraka, maana umekutana na mtu njiani amekuvutia zaidi ya yule uliyekuwa naye. Ukifanya hivyo, ni kujiweka matatani.
Nasema hivyo maana unaweza kuondoka na kwenda kwa mwingine, ila ukakuta kasumba kubwa mno. Hapo hutafurahia zaidi ya kulia na kusaga meno. Ni baada ya kujidanganya mwenyewe.
Utashangaa kwanini ulifanya hivyo? Siku zote majuto ni mjukuu. Huna haja ya kulia. Ni wakati wako wa kuangalia mwenzako anakwendaje kwa kumuweka chini.
Ndio anaweza kuwa mnywaji sana wa pombe. Kwa bahati mbaya tabia yake ya ulevi wewe huitaki. Nadhani kwa kupitia wewe mwenyewe anaweza kuacha.
Ni baada ya kumwambia kistaarabu na kumuelezea jinsi gani anatakiwa awe ili aweze kuwa na wewe. Endapo yupo kwenye msingi wa kujenga nyumba yenu ya upendo anaweza kupunguza kama sio kuacha.
Nadhani hiyo ni tabia nzuri mno inayotakiwa ifanywe na wote, maana mapenzi mazuri siku zote ni kusikilizana. Hakuna njia ya mkato katika hilo . Ndio maana nasema pigania uhusiano wako.
Na kwa yule aliyejaliwa kufunga ndoa, basi ahakikishe kuwa analinda ndoa yake kwa kuzima zile dosari zinazoweza kuhatarisha usalama wa ndoa yake kwa sababu moja ama nyingine.
Wapo watu ambao kosa kidogo tayari wamedai talaka. Kwao wao ni bora wakimbilie talaka maana wameona mitaani wapo watu wanaoweza kuishi naye na kuendelea kujaza idadi ya wapenzi.
Inakera mno. Inatia aibu kama mtaa mzima umeumaliza kwa njia hiyo hiyo. Tabia ambazo baadhi yao zinaepukika endapo kwa mikono yako, mdomo wako na miguu yako itapigania kwa dhati suala hilo .
Watu watakucheka. Mwanamke kubadilisha wanaume zaidi ya watano kwa kipindi kifupi huo ni uhuni. Unajipakaza matope na kuonekana kituko mtaani na kuitwa majina mengi ya karaha.
Hutaweza kuwakataza watu kukuita wewe ni cha wote, jamvi la wageni na mengine lukuki. Kwanini uwakataze wakati ni kweli? Ajabu, utakapoitwa hivyo, watu watakusikia na kukuonea huruma.
Sio wote wanaweza kuwapenda wasichana wenye sifa mbaya kama hizo, hivyo ni wakati wako kujifunza kutokana na makosa. Muweke chini mtu wako kwa ajili yako.
Mfundishe tabia nzuri na upiganie kikweli uhusiano wako kwa faida yako na sio kukimbilia talaka au kuvunja mkataba wenu, maana sio vizuri na hakuna haja ya kujaza wanaume.
KUJADILI vitu vya maendeleo kwa Tanzania kunahitaji moyo wa chuma kama alivyowahi kusema muasisi wa Taifa hili, Hayati, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere juu ya masuala nyeti ya Azimio la Arusha.
Dayna Nyange, msanii
Mwalimu, mmoja wa viongozi wanaopendwa barani Afrika, Oktoba 14, ilikuwa ni kumbukumbu ya kifo chake, baada ya kumaliza siku zake za kuishi duniani, akitumika kama mkombozi kwa Taifa hili, linaloongozwa na Rais wake, Jakaya Mrisho Kikwete.
Nasema moyo wa chuma, maana hata kama uwe mjuzi wa kujadili mambo hayo kwa kiasi gani, hao wanaojadiliwa kubadilika kwao ni kazi ngumu. Katu hawataki kusikia au kuona yale wanayofanya kwa faida ya nchi yao .
Hata hivyo, sio jambo la busara kubaki kimya. Taifa linazidi kutumbukia kwenye shimo baya la umasikini na wachache wao wakizidi kuneemeka. Utajiri ni wa kwao, wakati wenzao wanazidi kuwa masikini wa kutupwa.
Tanzania ya leo, ni kazi ngumu kupata ajira kama huna fedha. Suala kama hilo , linaonyesha ni jinsi gani mambo yanavyotakiwa kubadilika kwa faida ya wananchi wake. Tuache hayo turudi kwenye lengo la makala haya.
Wakati Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo akiteua safu mpya ya uongozi ya baraza la Michezo Tanzania , nadhani ipo haja pia ya kuangalia upya mwenendo wa uongozi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Baraza hili muhimu kwa Tanzania naweza kusema limekufa. Viongozi wake wengi hawaonyeshi jitihada zao za dhati kwa maendeleo ya sanaa ya Tanzania . Wasanii waliokuwapo bado kazi zao hazina jipya, huku wengineo tungo zao zikikosa sifa.
Ni hao wanaoacha kutunga nyimbo za kukosoa madawa ya kulevya, kubweteka majumbani au kwenye vijiwe vya kahawa, huzama zaidi kwenye tungo za kidunia. Hapa lazima niwe muwazi na bila ya kuweka woga wowote kwa ajili ya Tanzania .
Sitaki kusema viongozi wa BASATA wote wameshindwa kazi, ila Serikali lazima iwapige jicho ama kuwaelekeza vitu vizuri kwa ajili ya maendeleo ya Taifa. Nimepata nafasi ya kuchunguza utendaji kazi wa BASATA na kubaki mdomo wazi.
Mengi wanayofanya, si maendeleo kwa sanaa ya Tanzania . Uchunguzi wangu unaonyesha kila msanii wa nje anayekuja hapa nchini hutakiwa alipe fedha nyingi kama gharama za kuja kufanya kazi Tanzania , zisizopungua milioni moja.
Kwa mfano, wapo wanaotozwa hadi kiasi cha shilingi miliona moja, huku wakitakiwa walipe fedha za faini, kama mtu huyo ameanza kutoa habari kwa wanahabari kwa ajili ya kuwajulisha Watanzania.
Sawa, ila wakati mwingine wadau hao huonewa kwa makosa ambayo sio yao . Nasema hivyo huku nikiangalia upekuzi wa waandishi kujua habari hata zile wasizotakiwa wazifahamu kwa wakati huo.
Pamoja na hayo, kama ndivyo hivyo, fedha hizo za faini kiasi cha milioni moja hupelekwa wapi? Je, nchi hii inafanya juhudi gani kutangaza sanaa ya Tanzania ? Wasanii wetu wa ndani wanafanyiwa vitu gani kwa mafanikio yao ?
Msanii wa ndani kubaki kuimba peke yake ni jambo linaloweza kuangamiza kipaji chake. Inatakiwa apate ushindani, ama kusoma kutoka kwa wenzake. Hivyo basi, kitendo cha BASATA wao kujifanyia mambo kienyeji ni kuharibu mfumo mzima wa sanaa.
BASATA wao huku wakiweka mbele fedha, lazima utendaji kazi wao uwe mzuri, maana uliopo sasa ni kubuluzana na uliojaa maslahi binafsi. BASATA iliyopo sasa ni kuwakomoa wadau wenye uwezo wa kukuza sanaa kwa manufaa yao .
Sitaki nionekane tofauti juu ya hili, ndio maana hapo mwanzo wa makala haya nikatahadharisha maana wanaopewa ukweli hupayuka wakisema wanayojua wenyewe. Inatia aibu, kama kila mtu anahifanyia anavyojua mwenyewe.
Huku wadau tukipigania utendaji mbovu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), bado kuna vitengo nyeti vinaachwa tu bila kukosolewa. Nisema tu, nitakuwa mkweli kusema kila ninalojua kwa maendeleo ya Taifa langu, hata kama nitachukuliwa tofauti.
Kuna mambo mabaya mno yasiyofaa kufanywa na viongozi wetu, iwe ni kwenye michezo ama sanaa inayofaa kuheshimiwa Dunia nzima. Angalia Barani Ulaya, wengi wanafanikiwa. Muangalie mwanadada Rihannah, Jay Z na mke wake Beyonce, utakubali kuwa sanaa inalipa.
Sio huyo tu, bado wapo wakali wengine wanaovuna fedha lukuki, kutokana na kukuta mfumo mzuri katika nchi zao, ikiwamo hakimiliki. Siamini kama wasanii wetu wa ndani wataendelea kuachwa tu, hali ya kuwa wana utajiri wa vipaji.
Ni wakati wao Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuangalia upya sera zao na sera za mabaraza yake, likiwamo hilo la BASATA. Sioni juhudi na harakati za kukuza sanaa ya Tanzania zaidi ya kuidumaza.
Je, ni wasanii wote wanatakiwa walipe fedha hizo zikiwamo faini au ni wachache? Ushahidi unaonyesha kuwa, kama ni kweli, basi BASATA wanavuna fedha nyingi, maana wengi wanakiuka masharti hayo. Yani kupata kibali, kabla ya kuvuja kwa ujio wao.
Hivi kweli, mwandishi kuandika ujio wa msanii fulani ni kitendo kibaya kiasi cha kuwafanya BASATA walazimike kutoza faini hizo? Jamani, kwanini Tanzania tunakwenda ovyo namna hiyo?
Kwanini tamaa ya kujaza matumbo yetu ipo mbele kuliko kusudio la kweli la kuwakomboa Watanzania kwenye vita hii ngumu ya maradhi, ujinga na umasikini? Sikatai, msanii alipe gharama za kuishi nchini, ila nyingine ni wizi tu.
BASATA unaweza kufuatilia kibali kwa muda mrefu bila hata kukupatia. Nia yao ni mdau huyo avunje amri yao ya kuzungumzia ujio huo hata kwa marafiki zake, ili wapate hiyo shilingi laki tano au milioni moja.
Yuko wapi Emmanuel Nchimbi, waziri wa Wizara hiyo? Hivi kweli ndivyo BASATA wanavyotakiwa wajiendeshe? Sina nia mbaya, ila kusudio ni kujiendesha vema kwa manufaa ya Tanzania na sio kwenda ndivyo sivyo.
BASATA wanatakiwa wasome alama za nyakati. Wanatakiwa wawe na fikra pevu juu ya sanaa ya Tanzania , inayozidi kuyumba. Wengi kazi zao ni mbaya na zinakosa maudhui na maana halisi ya sanaa ya Tanzania , hata kwenye matamshi.
Bado sanaa nyingine zinakosa mwamko, ikiwamo ya nyimbo za asili, zile za makabila tofauti, zilizokuwa zikivuma wakati huo. Sanaa kama ususi, uchongaji, uchoraji sasa zimeadimika kabisa katika Taifa hili.
Wanaotamba ni Bongo Fleva, tena kwa kazi ambazo nyepesi, zimekosa soko na mvuto linapokuja soko la Kimataifa. Wengi wao mavazi yao ni karaha tupu. Bado wabunifu ni mavazi wapo wapo tu. Ukienda nchi za wenzetu wamefanikiwa, kiasi cha sasa kuangalia mazuri yao .
Sisi tuna wasanii wengi tu, lakini bado Makhirikhiri wamekuja kuteka soko la Tanzania, bila kusahau ndugu zao Dikakapa Traditional Dance, ambao hadi sasa wapo mikoani huko wakitangaza muziki wao wa asili.
Sawa, waje tu, maana najua ni somo kwa wadau, viongozi na wasanii wa ndani. Lakini kuwekewa ngumu, au wadau kutozwa fedha nyingi ni kuwadhulumu wao na kuibananga sanaa ya Tanzania , inayotakiwa itangazwe na kila mmoja wetu.
Kiu yangu ni kuona sanaa inapiga hatua kwa kuwa na viongozi wenye uelewa, mipango na uthubutu katika kazi zao, sio wale wanaotamani zaidi kumiliki vitu vya thamani katika utawala wao, huku wanavyoviongoza vikijikongoja.
Ndio maana naitaka Serikali, kuangalia zaidi mfumo mzima wa BASATA na ndugu zao COSOTA, maana ni muhimu na wameshika funguo za mafanikio kisanaa ya wasanii wa Tanzania , wanaoshi kama njiwa, kula chini kulala juu.
WAKATI mwingine kusema ukweli ni jambo jema japokuwa hao wanaosemwa au kupewa ushauri huo, watajisikia tofauti kwa namna moja ama nyingine.
Inawezekana sisi ni watu wa karibu kabisa katika ufanyaji kazi huo, ila linapokuja suala la ukweli hakuna jinsi. Tuambiane tu kwa nia ya kufika pale tunapohitaji.
Jamani, kwenye ukweli siku uongo hujitenga. Hivyo hakuna haja ya kuogopana. Ni kutokana na hilo, acha niseme kuwa Shirikisho la Soka nchini (TFF), chini ya Rais wake, Leodgar Tenga, tujiandaye kulia zaidi.
Katu tusijidanganye kupiga hatua kamwe. Wala tusitarajie kupanda viwango vya soka vya juu zaidi au kucheza michuano mikubwa duniani, ikiwamo Kombe la Dunia.
Tunachotakiwa sisi ni kujiandaa kulia zaidi kwa kuporomoka kwenye michezo, maana viongozi wengi wanafanya kazi zao kisiasa zaidi wakiwa na nia ya kulindana hata pale watu hao wanapoharibu na kuwakera watu.
Nikiwa kama mdau wa michezo, nitamlaumu Tenga kwakuwa ndiyo Rais, ila zaidi wa kubeba lawama hizo ni Katibu Mkuu wake, Angetile Osiah.
Tenga kulia na Sunday Kayuni
Ndio, maana yeye ndio mtendaji mkuu wa yote japo kuwa amekuwa mwepesi mno kujitetea au kumtetea yule anayeonekana tofauti kwenye utendaji kazi wake.
Angalia mwenendo wa timu ya taifa, Taifa Stars. Ni utumbo mtupu. Kila mara kumekuwa na kasumba za hapa na pale. Klabu zinakwenda ndivyo sivyo.
Osiah bila kujua analofanya, anajichanganya zaidi kwa kumuondolea majukumu yake, Mkurugenzi wa Ufundi, Sunday Kayuni. Eti kuboronga kote huko hakusababishwi na yeye, wakati anajua fika ufundi wote upo chini yake.
Kwa madai yake, wa kulaumiwa ni watu wengine wakiwamo wakuu wa mashindano. Jamani, kabla ya kufika huko kwenye mashindano, lazima ufundi utangulie.
Ni yeye wa kuangalia ratiba zinakwendaje ili mambo yaende vizuri. Kubadilishwa ovyo kwa mechi za ligi kuu au vitu kuingiliana kumesababishwa nay eye.
Wala sina haja ya kutoana kafara hapa, kama walivyomtoa kafara Ofisa Habari wao wa zamani, Florian Kaiajage kwenye tukio la kugoma CD ya wimbo wa Taifa, ila ukweli lazima usemwe maana baadhi ya Watanzania, hawajui wajibu wao.
Hakuna mipango kabisa TFF. Hawasimamii michakato ya kupiga hatua katika sekta ya michezo, ukiwamo mpira wa miguu, zaidi ya kukalia vyeo wasivyoviweza.
Kwa bahati mbaya au nzuri, wanaojitolea kusema ukweli huonekana tofauti katika nyuso zao na kusemwa kupita kiasi, wakijifanya wao ni miungu watu wasioweza kukosea.
Eti, ndio tatizo na watapekelekea wadhamini wawatose kwa namna moja ama nyingine. Jamani, hakuna malaika hapo. Hakuna aliyekamilika. Kukoselewa kuna maana ya kujipanga ili Taifa lipige hatua kutoka hapa lilipo.
TFF wamekosa changamoto na ari kwa wadau na wachezaji wote, kuanzia Taifa Stars na wale wanaocheza ligi. Ndio maana ligi inakosa mvuto kwa ratiba mbovu.
Mara kadhaa timu ya taifa, Taifa Stars, inakosa mechi za kujipima nguvu, kitu kinachoifanya ishindwe kupiga hatua kutokana na maandalizi yao hafifu.
Ni matatizo makubwa. Kwa timu kama hiyo isiyokuwa na jipya, inahitaji maandalizi ya uhakika na wala sio kuzima moto kama wanavyofanya sasa na kufuja fedha za walalahoi.
Ona, hawa wameanza kulinganisha uwepo wa Osiah na ule wa Fredrick Mwakalebela. Mwakalebela ni Katibu Mkuu wa zamani, aliyemaliza muda wake na kuhamia kwenye siasa.
Huko alishindwa kuingia bungeni kwa sababu anazojua mwenyewe na chama chake. Sitaki kuingia huko kwenye siasa, maana ndizo zinazoharibu mfumo wetu wa maendeleo ya michezo.
Wakati wa Mwakalebela, hakujatokea hayo yanayotokea sasa. Na hata kama yaliyotokea, basi si kwa kiwango kikubwa kama inavyokuwa sasa kiasi cha kukosa kusafiri kwa timu ya Taifa, huku klabu ikifanikiwa kwenda Sudan.
wachezaji wa Tanzania wanayecheza soka la kulipwa nje walikuwa wakiwasili kwa wakati tofauti na sasa. Hakuna mawasiliano mazuri wao na Mashirikisho mengine duniani.
Kulikuwa na mawasiliano ya uhakika. Mechi za kujipima nguvu zilikuwa za kutosha. Hali hiyo ilimfanya hata kocha wa wakati huo, Mbrazil, Marcio Maximo, afanye kazi yake vizuri.
Leo hii baadhi ya wadau wameanza kumtupia lawama kocha wa sasa wa Stars, Mdenmark, Jan Borge Poulsen. Hoja wanayo, ila pia wasisahu na ubabaishaji huu wa TFF.
Nadhani wanafanya hivyo kwasababu kocha ndiyo mwenye jukumu hilo, lakini wakati mwingine tunaweza kumuonea na kumtupia mzigo wa bure, wakati anashindwa kusimamiwa na viongozi hao wa TFF wanaojaribu kukwepa majukumu yao.
Hasaidiwi huyu. Hata akisaidiwa, wakubwa hao huangalia namna ya kupambana na wezi wa milangoni na kusahau mengine, maana nia yao ni kuingiza mapato ya kutosha.
Kwanini viongozi wasikubali kushindwa na kuweka mipango mingine? Hatuna ligi nzuri yenye ushindani.
Hatuna msingi imara wa kuendeleza vijana wadogo, bado tunaota ndoto ya kuwa na kiwango imara. TFF wa leo, wakiulizwa vijana wanaopatikana kwenye michuano ya Copa Coca-cola leo wanafanya nini hawatakuwa na jibu hilo.
Uwapi umuhimu wa kuwa na ligi hiyo? Huko wilayani kwenye vijana wengi kuna endelea na nini? Mkurugenzi wa Ufundi, Kayuni kazi zake ni zipi pale TFF?
Ziwekwe wazi ili wadau wazijuwe. Ni hapo ndipo ninapojikuta nikishindwa kuwaelewa TFF.
Najua ni kazi ngumu kusema ukweli, ila kwa hali ilivyo, Watanzania wajiandaye kulia zaidi, maana mafanikio kwetu ni ngumu na tusijidanganyane kwa hilo.
Hatuwezi kufanikiwa wakati tunafanya kazi midomoni. Ni ngumu kupiga hatua wakati sisi tunachojua ni kusawazisha kauli zinazopingwa na wadau, ili waonekane viongozi wazuri kwa jamii wakati ni uongo mtupu.
Osiah ambaye ndio mtendaji mkuu wa TFF, kazi yake imekuwa ngumu mno. Ameshindwa kuwa na ushawishi kwa wadau na upo uwezekano wa kuwapoteza hata wadhamini waliokuwapo sasa kwenye timu zetu.
Najua Osiah ni ndugu yetu ila kumuangalia anavyokwenda ni kumuharibia. Watu wanamuona. Sifa yake inazidi kupotea kwa ubabaishaji wake.
Binafsi napenda kuona anakwenda vizuri na ndio maana nakuwa muwazi kwa ufanyaji wake wa kazi. Hana jipya. Ajaribu kuangalia namna anavyoweza kujiendesha.
Kama ni mpole awe mkali zaidi. Zipo tetesi zinazodai kuwa Osiah licha ya kuwa na cheo hicho, lakini wapo watu wa chini yake wanamuendesha.
Sitaki kuliamini hilo japokuwa najua lisemwalo lipo, maana nia ni kuwekana sawa ili Tanzania ipige hatua katika sekta ya michezo, ukiwamo huo mpira wa miguu.
Kwanini? Hivi kweli sisi tunakuwa watu wa kuchekelea mafanikio ya wenzetu, wakati tuna idadi kubwa ya wanamichezo waliozagaa katika wilaya mbambali.
Fanya uchunguzi utakubaliana na mimi. Huko Handeni mkoani Tanga, Iringa, Mtwara, Tarime, Morogoro na kwengineko kumejaa vipaji vya hali ya juu ila hawaendelezwi wala hawaibuliwi kutokana na mipango yenye tija na Tanzania.
Vijana hao wanakosa walau jezi za kuvaa wakati tuna TFF inayoungwa mkono na wadau wakubwa tu. Sitaki kuamini kama muda umekwisha, maana wanaweza kujirekebisha na kusonga mbele wakiacha kasumba zao.
Kwa sasa TFF hawana jipya. Viongozi wapo wapo tu kwenye viti vyao vya kuzuunguka. Kusua sua huku kukiendelea, lawama hizi ni zenu, maana wadau wanawaunga mkono.
Tatizo lipo wapi? Siasa? Ubinafsi ama ni kuogopana? Kila mtu lazima afanye kazi yake kama inavyotakiwa. Tenga, lazima awe mkali kwa vijana wake ili mambo yaende.
Osiah lazima akubali kukosolewa na watu wakiwamo wanahabari ambao kifani ni ndugu zake kabisa. Naye ni mwanahabari hivyo uwepo wake TFF ni mafanikio kwa waandishi wote nchini wakiona mwenzao anakwenda vema.
Malalamiko mengi yamekuwa kwa vyama vingine vya michezo miaka nenda rudi maana ufanyaji kazi wao ni wa midomoni.
Faida yao wanaijua, ndio maana kila siku malalamiko yao ni fedha za maandalizi na hakuna anaewasikiliza.
Wakati huo TFF wao walitulia lakini kwa bahati mbaya sasa kibao kinaanza kuwaugeukia wao. Zindukeni nyie? Kumbushaneni wajibu wenu. Punda hawezi kwenda bila mchapo.
Binafsi nipo tayari kwa lawama maana najua siku zote sio mzigo ili mradi ujumbe wangu umewafikia.
Kwa mwendo huu wa TFF, kikweli maendeleo ya soka ni ndoto ya kuku kutamani kunyonyesha watoto wake.
MENEJA wa msanii wa filamu aliyewahi kutamba mno miaka ya nyuma, Christina Manongi, Richard Methew, amesema filamu itakayowakutanisha mwanadada huyo na Juma Kassim maarufu kama ‘Juma Nature’, itakuwa moto wa kuotea mbali, endapo makubaliano yao yatafikiwa na wawili hao.
Kwa siku kadhaa sasa wawili hao wamekuwa wakikutanishwa kwa nia ya kupatanishwa ili wacheze filamu hiyo, baada ya kuingia kwenye malumbano, yaliyosababisha Juma Nature atunge vibao viwili vya ‘Sitaki Demu’ na ‘Inaniuma Sana’.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Methew alisema hadi sasa Sinta bado hajakuwa tayari, licha ya kuonekana kuelekea kwenye makubaliano hayo.
Alisema mara baada ya kufikia makubaliano yao, wawili hao watacheza filamu hiyo na kutangazwa kwa wadau kwa nia ya kuona kazi yao inakuwa nzuri.
“Nimejaribu kuangalia vipi Sinta anaweza kurudi kwenye sanaa yake, huku nikiamini kuwa akicheza na Nature inaweza kuwa kazi nzuri zaidi na kumrudisha kileleni.
“Najivunia kuwa na msanii kama Sinta, hivyo naamini akifikia makubaliano kwa kusahau yote yaliyopita, mambo yanaweza kuwa mazuri zaidi,” alisema Mathew.
Hata hivyo, Sinta alipozungumza na Gazeti hili jana, alisema hana nia ya kurudi kwenye uhusiano wa kimapenzi na Juma Nature, hivyo wadau wanapaswa kuelewa katika hilo.
Juma Nature chini na Sinta juu.
Mwanadada huyo ni miongoni mwa wasanii wa kike mahiri na wanaosubiriwa kwa hamu kubwa katika ulingo wa filamu, huku umbo na sura yake likichanganya wengi, tangu wakati huo anashiriki katika michezo ya kundi la Kaole Sanaa Group.
WAKATI klabu ya Simba, ikitarajiwa kuanza mazoezi leo kwa ajili ya kujiandaa zaidi na mechi za ligi kuu, mshambuliaji wa Kimataifa, Gervas Kago, ameombwa na nchi yake kwenda kujiunga na timu yake ya Taifa.
Hiyo ni baada ya Afrika ya Kati, kuwasilisha barua yao jana, wakati tayari alishajua kuwa ataanza mazoezi na wenzake, licha ya nyota wanne wa Simba, kuitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars, kinachonolewa na Mdenmark, Jan Poulsen.
Wachezaji hao wa Simba walioingia kambini wakijiandaa na safari yao ya Morocco, ni Juma Kaseja, Juma Nyoso, Victor Costa na Amir Mafta.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kuwa kupokea barua hiyo kunaonyesha kuwa naye hatajiunga na wenzake kwa ajili ya kujiandaa na patashika ya ligi ya Vodacom.
Simba wanaendelea na mikakati yao wakati Yanga wao wamesimama mazoezi kwa ajili ya kupisha maandalizi ya Stars, kitu kilichomfanya kocha wao, Mganda, Sam Timbe, kurudi kwao kwa muda.
Gervas Kago
“Tunashughulikia usafiri wao kuanzia sasa, nadhani naye hatakuwapo kwenye timu yetu kwa ajili ya kuwakilisha Taifa lake, Afrika ya Kati.
“Ni jambo zuri mchezaji kuwamo kwenye kikosi cha timu ya Taifa, hivyo wale wote ambao hawapo kwenye timu zao za Taifa, kesho (leo) wataanza mazoezi,” alisema Kamwaga.
Simba inaongoza ligi ikiwa na pointi 18, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 15, wakati Yanga wao wana pointi 12, wakizinduka katika mechi mbili zilizopita na kuonyesha kiu ya kutaka kutetea ubingwa wao huo.