Pages

Pages

Monday, January 28, 2013

Tusielekeze macho yetu kwa Simba na Yanga peke yao



SIWEZI KUVUMILIA
Mlinda mlango wa Simba, Juma Kaseja.

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WATANZANIA hatuwezi kuendelea kama hatutakuwa na mapenzi mema na timu zetu zote na sio kuegemea zaidi kwa timu kongwe za Simba na Yanga.

Kauli hii naisema leo ambapo najua ligi hatua ya mzunguuko wa pili imeanza, huku timu 14 zikiwania taji hilo linalodhaminiwa na Kampuni ya Simu za Mikononi ya Vodacom Tanzania.

Ndio ukweli huu, maana nimeshindwa kuvumilia kuona baadhi ya timu zetu zinazoshiriki ligi mara kadhaa kucheza na majukwaa, huku mashabiki wakiangalia zaidi timu kongwe.

Hii sio njia nzuri, maana wakati mwingine zinawakosesha mapato kwakuwa kabla ya mchezo husika, timu hizo hutumia gharama kubwa kuwaandaa wachezaji wao.

Kama hivyo ndivyo, timu hiyo inayotegemea mapato ya milangoni, zitajiendeshaje? Hii ni tofauti na nchi zilizoendelea. Huko kila shabiki anakuwa kama kichaa kwa kuipenda zaidi timu yake sambamba mpira wa miguu kwa ujumla.

Kuna watu ambao wanachoangalia wao ni Yanga na Simba tu. Timu ya African Lyon yenye maskani yake jijini Dar es Salaam, haiwezi kuendelea kwa kutunisha mfuko wao, hadi icheze na Yanga au Simba.

Timu ya Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Azam FC, Coastal Union lazima ziungwe mkono zinapokutana zenyewe kwa kuhakikisha kuwa mashabiki tunajaza viwanja.

Najua hali ni ngumu kwa kila mmoja wetu, lakini si sahihi pia kujidanganya kwamba soka lipo kwa watani wa jadi, Simba na Yanga peke yao.

Huo ndio ukweli wa mambo, maana kadri siku zinavyozidi kwenda mbele, mahitaji ya kuendeleza timu zetu za mpira wa miguu yanazidi kuwa makubwa na magumu.

Michezo ni pesa inayolipa, lakini si kwa mtindo huu unaoendelea wa Watanzania kuona ili nafsi zao zinakuwa na raha zaidi kwa kuwaangalia watani wa jadi.

Sikatai, upenzi wa timu hizo hauwezi kufutika, ila shabiki wa kweli wa soka hawezi kukosa uwanjani kwa namna moja ama nyingine. Watanzania tujenge mapenzi na timu zetu.

Huko kuangalia Simba na Yanga, kumetupambaza kiasi kwamba hatuangalii mafanikio ya Taifa. Katika mzunguuko wa kwanza wa ligi hiyo, kuna timu zimegawana kiasi kisichozidi elfu 50,000 kama mapato ya uwanjani.

Angalia hasara hii. Fedha hizo zinaweza kweli kuwatoa Tanga, kama ni Coastal Union na kuwapeleka Bukoba kucheza na Kagera Sugar, zaidi ya kutafuta nauli kwa njia nyingine?

Tanzania ni yetu wote. Ili isonge mbele tunahitaji kuwa na akili mpya, hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi, kimichezo na kijamii.

Tukiangalia soka la Simba na Yanga pekee hatuwezi kwenda, maana timu hizo zimekuwapo kwa miaka mingi na bado hakuna cha maana zaidi ya kushuhudi migogoro, matusi, kejeli na fitina za kila aina zinaposukwa njama za kila aina, iwe kuupinga uongozi uliokuwapo madarakani na mengineyo.

Tujaribu kuweka karata zetu kwa timu zote za Tanzania ili zione tahamni ya Watanzania katika hali ya kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya mpira wa miguu.

Wakati nasema hayo, nakumbuka kuwa Tanzania mwaka huu katika mashindano ya Kombe la Shirikisho inashiriki timu ya Azam FC, ambayo kwa hakika ina mipango kabambe ya kuweza kutangaza soka la nchi hii kwa waliopiga hatua.

Azam inashiriki mashindano hayo baada ya mwaka jana kushika nafasi ya pili katika ligi ambayo Simba ilinyakua ubingwa huo, hivyo yenyewe kupata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ni Azam hii ambayo baadhi yao wanaiangalia vibaya, wakiona haina cha maana, hata pale wanapoangalia mafanikio yao waliyopata katika kipindi kifupi mno.

Katika hilo, hakika siwezi kuvumilia, hivyo wadau wa michezo, hasa wa mpira wa miguu tuna kila sababu ya kuangalia juhudi zetu katika hali ya kukuza soka letu.

Sitaki kusema kwamba tusipende timu za Simba na Yanga, maana wengineo ndio imani zao, lakini tupende michezo kwa ujumla, kwa kuingia uwanjani kihalali ili mapato yaweze kuendesha timu hizo zinazotegemea mapato.

Vinginevyo, Simba na Yanga zetu, zitazidi kuathiri kiwango cha mpira wa miguu, maana zenyewe zinajiweza kwakuwa na rasilimali fedha na watu, hivyo kuweza kufanya lolote, ikiwamo kununua mechi kwa timu zinazopoteza mwelekeo kwa kukosa bajeti.

0712 053949
0753 806087

No comments:

Post a Comment