https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Thursday, October 31, 2013

Serikali yatangaza viwango vipya vya ufaulu elimu ya sekondari

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome akifafanua kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya upangaji wa viwango vya alama, matumizi ya alama endelevu  ya mwanafunzi  na ufaulu leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Kamishna wa Elimu Profesa Eustella Bhalasesa.
 Baadhi ya Maafisa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Profesa Sifuni Mchome (hayupo pichani).
Waandishi wa habari na maafisa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wakimsikiliza kwa makini Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome(hayupo pichani). Picha zote na Eliphace Marwa (MAELEZO).

Ukumbi wa mazoezi ya ngumi za ridhaa Tanga kikwazo kwa mchezo huo


Na Oscar Assenga,Tanga.
CHAMA cha Ngumi za Ridhaa mkoa wa Tanga(TBA)kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutokuwa na ukumbi wa kufanya mazoezi kwa mabondia kitendo ambacho kinawapa wakati mgumu mabondia wakati wa kufanya mazoezi. 



Mwenyekiti wa Chama hicho,Mansour Soud Semfyoa aliiambia Tanga Raha kuwa hali hiyo inawafanya mabondia hao kushindwa kutimiza ndoto zao na kuziomba mamlaka husika ikiwemo uongozi wa serikali ya wilaya kuwasaidia ili kuweza kupatikana ukumbi wa mazoezi.

Soud alisema suala lengine ambalo linawapa changamoto ni uhaba wa vifaa vya kufanyia mazoezi kwa mabondia waliopo mkoani hapa hivyo kuwaomba wadau kuwasaidia ili viweze kupatikana.
Mwenyekiti wa Chama Cha Ngumi za Ridhaa mkoani Tanga, Mansour Soud Semfoya
Mwenyekiti huyo alisema chama hicho kimefanya jitihada mbalimbali ili kuweza kupatikana ukumbi wa Tangamano ambapo uongozi wa chama hicho  tayari umeshaandika barua kwenda kwa mkurugenzi wa Jiji lengo likiwa ni kumuomba wautumia ukumbi wa Tangamano.

Alisema majibu ya barua hiyo iliwajibu wamekubaliwa katika ukumbi wa Communite Centre Makorora ambapo wataungana na vikundi vyengine na kuelezwa kuwa wanatakiwa walipie sh.elfu hamsini ili waweze kupewa eneo hilo.

Dunia yampongeza Jamal Malinzi kwa ushindi wa urais TFF

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Rais mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Jamal Malinzi ameendelea kupokea salamu za pongezi baada ya kushinda wadhifa huo katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27 mwaka huu.
Jamal Malinzi, Rais wa Shirikisho la Soka nchini TFF.
Salamu nyingine za zimetoka kwa Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Sepp Blatter ambapo amempongeza Malinzi kwa kuchaguliwa na kumtakia kila la kheri katika majukumu yake ya kuongoza mchezo huo nchini.

Blatter amesema ana uhakika ufahamu wake na uwezo wake katika uongozi ni muhimu katika kuimarisha maendeleo ya mpira wa miguu nchini, na kuongeza kuwa milango ya FIFA iko wazi wakati wowote anapotaka kujadili masuala yanayohusu mchezo huo.

“Nakutakia wewe na kamati mpya ya Utendaji iliyochaguliwa kila la kheri, nguvu, na kila aina ya mafanikio kwa changamoto zilizo mbele yenu,” amesema Rais Blatter katika salamu zake.

Wengine waliomtumia Rais Malinzi salamu za pongezi ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF), Sam Nyamweya, Rais wa Heshima wa Shirikisho la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA), Lawrence Mulindwa, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Arumeru (ADFA), Peter Temu.

January Makamba azipiga tafu shule za sekondari Baga na Tamota


Na Raisa Saidi, Bumbuli,  

Mbunge  wa  jimbo  la  Bumbuli  January Makamba  amekabidhi  msaada  wa  shilingi  milioni mbili  katika  shule  ya  sekondari  ya Baga na  Tamota   kwa  ajili  ya  ujenzi  wa  Maabara   kwa lengo la  kuinua  masomo  ya  sayansi.



Pamoja na msaada huo wa milioni moja moja kwa kila shule pia ametoa  msaada  wa  mabati  mia moja kwa kila shule kwa ajili ya  kuezekea  vyumba  vya  madarasa  na nyumba  za walimu   katika  shule hizo.



Alitoa msaada huo wakati alipokuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya kidato cha nne kwenye shule hizo.

Wednesday, October 30, 2013

Makamu wa Rais Dk Gharib Bilal afungua kongamano la kujadili mtandao wa maji SADC

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akifungua rasmi kongamano la kujadili Mtandao wa maji kwa Nchi Wanachama wa SADC, lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, leoJijini Dar es Salaam.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akifungua rasmi kongamano la kujadili Mtandao wa maji kwa Nchi Wanachama wa SADC, lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, leoJijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa 'local Organizing Commitee', Prof. Mtalo Felix, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano hilo.

Mwidau ataka kasi ya maendeleo mkoani Tanga

Na Mwandishi Wetu, Tanga

MBUNGE wa Viti maalum Mkoa wa Tanga Amina Mwidau (CUF), amewataka wananchi wa Mkoa wa Tanga kubadilika kwa kuwa na ari ya kujiletea maendeleo yao na jamii kwa ujumla.

Mbunge Amina Mwidau, akihutubia wanannchi wa Wilaya ya Pangani katika ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo Mkoa wa Tanga.

Kauli hiyo ameitoa mjini hapa alipokuwa akizungumza na vionozi wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Tanga (Tanga Press Club).

Alisema kuwa ili maendeleo ya haraka yaweze kupatikana katika mkoa huo ni lazima jamii kubadili kwa kuwa na mawazo chanya.


“Maendeleo ni jambo muhimu sana na katika hili ni lazima tushirikiane kwa dhati. Binafsi ninapenda kupongeza juhudi za chama cha Waandishi wa habari Mkoa wa Tanga kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya katika kutangaza mkoa wetu.


“Nilikuwa nasoma na sasa kila wakati tutakuwa pamoja na wanahabari pamoja na wananchi wa mkoa wetu ili kuweza kuungana kwa pamoja katika juhudi za maendeleo za mkoa,” alisema Mwidau

MGODI UNAOTEMBEA: Sakata la Mwigamba na ishara mbaya Chadema



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
BAADA ya Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali nchini (PAC), Zitto Kabwe, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, alipotoa hoja juu ya vyama vya siasa kutokaguliwa, mengi yalisikika.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, pichani.
Hasa ni pale viongozi wa vyama vya siasa nchini kutumia muda mwingi katika vyombo vya habari kukanusha na wengine kufika mbali kusema kuwa Zitto anapenda kujenga matukio ili kuweka juu jina lake.


Mwenyekiti wa Chadema Arusha aliyesimamishwa, Samson Mwigamba, pichani.
Kwa wale tunaomfuatilia Zitto kwa karibu tukagundua kuwa kuna kitu ndani yake na kingetokea mapema iwezekanavyo. Ikumbukwe kuwa, Zitto mbali na kuwa mwenyekiti wa PAC, pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kama kweli vyama siasa havijakaguliwa hususan Chadema, yeye pia yupo ndani ya chama hicho. Je, hoja yake zaidi ilitokakana na kutaka kuinyuka Chadema?

Najikuta najiuliza maswali hayo baada ya Chadema kumsimamisha Mwenyekiti wa mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kwa madai kuwa ametoa siri za chama chao hadharani.
Siri? Ni siri gani hizo zinazofichwa kiasi cha kuwataka watu wengine wa nje wasijuwe? 

Inashangaza mno. Ukijaribu kufuatilia suala hilo na kauli ya Zitto juu ya mahesabu ya vyama vya siasa yanafanana.
Mwigamba amemtuhumu Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na Katibu Mkuu wake Dk Willbroad Slaa juu ya mahesabu na matumizi yote ndani ya chama hicho.

Tuesday, October 29, 2013

Mkuu wa Mkoa Tanga Chiku Gallawa atembelea kiwanda cha Rhino Cement jijini Tanga

Mkuu wa Mkoa Tanga, Luteni Mstaafu, Chiku Gallawa katikati akipewa maelekezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Kiwanda cha Rhino Cement  akiwa sambamba na Mkuu wa Wilaya Tanga, Halima Dendego.
Baadhi ya mitambo mipya inayojengwa kiwandani hapo.
Kiwandani cha Rhino Cement alipotembea Mkuu wa Mkoa Tanga leo.
Hapa wanazungumza moja baada ya jingine kiwandani hapo.

Kongamano la kujadili ujangili duniani lafanyika mkoani Kilimanjaro

Kaimu Mkuu wa Chuo cha uhifadhi na usimamizi wa Wanyama Pori mkoani Kilimanjaro (MWEKA), Dkt. Freddy Manongi akitoa maelezo katika kongamano la kujadili changamoto na mbinu za kukabili ujangili duniani, iliyofanyika katika ukumbi wa chuo hicho leo kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya chuo cha Mweka.
Wadau wa Uhifadhi wa Wanyapori kutoka katika nchi 20 duniani, wakifuatilia mafunzo katika Kongamano la kujadili changamoto na mbinu za kukabili ujangili duniani, iliyofanyika katika ukumbi wa chuo hicho leo kama sehemu ya Maadhimisho ya miaka 50 ya chuo cha Mweka.
Wadau wa Uhifadhi wa Wanyapori kutoka katika nchi 20 duniani, wakifuatilia mafunzo katika Kongamano la kujadili changamoto na mbinu za kukabili ujangili duniani, iliyofanyika katika ukumbi wa chuo hicho leo kama sehemu ya Maadhimisho ya miaka 50 ya chuo cha Mweka.

Pendo Njau atangaza mahaba kwa masumbwi


Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

BONDIA Pendo Njau, amesema kwamba hakuna mchezo mwingine anaopenda zaidi ya masumbwi, jambo linalomfanya aendelee kuwa busy katika kuuweka sawa mwili wake.

PENDO NJAU
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Pendo alisema kuwa jambo hilo linatokana na kuwa na dhamira ya kulinda makali yake katika mchezo wa masumbwi nchini.


Alisema tangu akiwa na umri mdogo aliupenda sana mchezo huo, hivyo anaamini kuwa ndio njia ya kumpatia mafanikio katika masumbwi na kupiga hatua Kimataifa.


“Mchezo wa ngumi ndio niupendao, hivyo ninachofanya kwa sasa ni kuhakikisha kuwa naendelea kufanya mazoezi makali kwa ajili ya kunifikisha hatua ya juu ya zaidi.

NAIBU WAZIRI WA KATIBA AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA IRELAND NCHINI TANZANIA

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria,Mhe. Angellah Kairuki akifafanua jambo
kwa Mgeni wake ambaye ni Balozi wa Ireland Nchini,Mhe. Fionnula Gislen wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika leo Ofisini kwa Mhe. Kairuki,jijini Dar es Salaam.

Monday, October 28, 2013

Coastal Union yainyunyizia vitatu Mtibwa Sugar jijini Tanga leo

Na Oscar Assenga,Tanga.

TIMU ya Coastal Union ya Tanga leo wakiwa chini ya Kocha Joseph Lazaro wamefanikiwa kuibamiza Mtibwa Sugar mabao 3-0,katika mchezo wa ligi kuu Tanzania bara uliochezwa uwanja w a Mkwakwani mjini hapa.

Kikosi cha Coastal Union kilichoichapa Mtibwa Sugar mabao 3-0.
Wachezaji wakisalimiana kabla ya mchezo huo kuanza.
Wachezaji wakiingia uwanjani.
Katika mchezo huo ambao ulikuwa mkali na wenye upinzani mkubwa ambapo Coastal Union waliweza kuandika bao lao la kwanza kwenye dakika ya 20 kupitia Crispian Odulla aliyemalizia kazi nzuri iliyofanywa na Haruna Moshi “Boban’



Baada ya kuingia bao hilo,Coastal Union waliweza kuendeleza wimbi la mashambulizi langoni mwa Mtibwa Sugar na kufanikiwa kuongeza bao la pili lililofungwa dakika ya 38 kupitia Jerry Santo kwa njia ya penati iliyotokana na Keneth Masumbuko wa Coastal Union kuangushwa katika eneo la hatari na Yusuph Nguya wa Mtibwa Sugar na mwamuzi wa mchezo huo Hashim Abdallah kuamuru ipigwe penati.

Jamal ndio Rais wa TFF, atangaza msamaha kwa waliofungiwa na TFF



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
Jamal Emil Malinzi ndiye Rais mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), huku akishinda wadhifa huo katika uchaguzi uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Rais wa Shirikisho la Soka nchini TFF, Jamal Malinzi.
Aliibuka na ushindi wa kura 73 dhidi ya mpinzani wake pekee Athuman Jumanne Nyamlani aliyepata kura 52. Nafasi ya Makamu wa Rais imetwaliwa na Wallace Peter Karia aliyepata kura 67 na kuwashinda Ramadhan Omari Nassib kura 52 huku Imani Omari Madega akipata kura sita.



Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa, Rais Malinzi ametaka ushirikiano kutoka kwa wadau wote akiwemo mpinzani wake Nyamlani katika kuhakikisha mpira wa miguu nchini unasonga mbele.



Pia ametoa msamaha kwa watu wote waliokuwa wamefungiwa kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa na TFF. Msamaha huo hauwahusu wale waliofungiwa kwa makosa ya rushwa au kupanga matokeo. Vilevile msamaha huo hauhusu adhabu zilizotolewa katika ngazi ya klabu.



Rais Malinzi pia amevunja kamati zote za TFF ambapo ataziunda upya kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji.



Kwa upande wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji walioshinda ni Kalilo Samson (Kanda namba 1- Geita na Kagera) aliyepata kura 102 za ndiyo na 17 za hapana. Kanda namba 2- Mara na Mwanza, mshindi ni Vedastus Lufano aliyepata kura 51 dhidi ya Jumbe Odessa Magati (11), Mugisha Galibona (24), na Samwel Nyalla (39).

Kesi ya Mfanyabiashara wa madini Erasto Msuya yaahirishwa hadi Desemba 11

Washitakiwa Joseph Damian "Chusa" na mwenzake Shaibu Jumanne Saidi "Mredi", wakimsaidia Mshitakiwa mwenzao kupanda katika Gari la Polisi muda mfupi baada ya kesi inayowakabili ya mauaji ya Bilionea wa Madini ya Tanzanite, Erasto Msuya kuahirishwa hadi Desemba 11, mwaka huu.
Ndugu wa Marehemu ERasto Msuya waliofika Mahakamani wakimuondoa Mdogo wa Marehemu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi kumuwaisha Hospitali baada ya Kupoteza Fahamu muda mfupi tu baada ya Mahaka ya Hakimu Mkazi Moshi, kuahirisha Kesi hiyo hadi Desemba 11.


Mwandishi Wetu, Moshi

MAHAKAMA ya Hakimu mkazi Moshi, Leo imeahirisha Kesi ya Mauaji ya Bilionea wa Madini ya Tanzanite Jijini Arusha, Erasto Msuya (43), hadi Desemba 11 mwaka huu.  

Kesi hiyo iliyotajwa katika Mahakama hiyo kwa mara kwanza, Agosti 21, mwaka huu, mbele ya Hakimu Mkazi, Munga Sabuni, inawakabili watuhumiwa 8 wanaodaiwa kuuwa kwa kukusudia kinyume cha Sheria ya Makosa ya jinai, Kanuni ya 16, Kifungu cha 196.

Pamoja na idadi ya Watuhumiwa wanaodaiwa kuhusika na Mauaji hayo ya kikatili, yaliyotokea Agosti 7, katika maeneo ya Mjohoroni, wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, kukamilika, Upande wa Mashtaka, ukiongozwa na Wakili, Janet Sekule, uliwasilisha Maombi ya kutaka Kesi hiyo ipangiwe Tarehe mpya ili kupisha Upepelezi kukamilika.

Wakili Sekule, alisema kuwa kutokana na uzito wa Kesi hiyo, Jamhuri ingependa kupatiwa muda wa kukusanya ushahidi wa kutosha ambao utawasaidia katika kesi hiyo, ombi ambalo halikupata pingamizi lolote kutoka upande wa Washtakiwa.

SIWEZI KUVUMILIA:Tutadanganyana tu, kwani nani anajali?



Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam

SITAKI kusikia nani ameshinda nafasi za Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), kwakuwa kuna uwezekano mkubwa uwapo wa mabwana wakubwa hao ukawa kazi bure.
Kikosi cha Twiga Stars
Siku zote wamekuwa wakitogotea pale pale. Mawazo au juhudi za kuokoa soka letu huwa zinaishia hewani. Ingawa kwa siku za hivi karibuni soka linaonekana kufika mbali, ila upande wa wanawake hakuna kitu.


Kila siku ya Mungu kilio kinakuwa kile kile. Wasichana ambao ndio wahusika wakuu wanaocheza mpira huo, wanaishia kulalama wakiangalia jinsi wanavyosuswa.


Kama hivyo ndivyo, kwanini nibabaike na majina ya wagombea wa TFF, katika Uchaguzi uliofanyika jana Jumapili? Nasema hivyo kwasababu juhudi nyingi zinaishia njiani.


Tumebakia watu wa siasa. Tunapenda sana kuzungumza mdomoni wakati vitendo vyetu vina matege. Ndio maana naona tunadanganyana tu,kwani nani anajali kuona soka letu linaanguka?


Nimefanikiwa kuzungumza na wachezaji mpira wa miguu wanawake kwa nyakati kadhaa na kuona jinsi wanavyolalamika. Hata maisha yao ya baadaye hawajui wataishi vipi.

Sunday, October 27, 2013

Mamia wamzika James Kombe nyumbani kwao Msae, Moshi, mkoani Kilimanjaro

Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT, kanda ya Kaskazini, Dkt. Martin Shao akiendesha Ibada ya Maziko ya  aliyekuwa Mkuu wa kitengo cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, James Kombe, aliyefariki dunia Oktoba 21 mwaka huu, Jijini Dar es salaam na Kuzikwa Jana Nyumbani kwake, kijiji cha Msae, Kata ya Mwika, wilaya ya Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama akitoa heshima za mwisho katika Jeneza la aliyekuwa Mkuu wa kitengo cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, James Kombe, aliyezikwa Jana Nyumbani kwake, kijiji cha Msae, Kata ya Mwika, wilaya ya Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro.
Mkuu wa wilaya ya Hai, Novatus Makunga (wakwanza) na Mkuu waWilaya ya Moshi, Dkt. Ibrahimu Msengi (wa pili) wakitoa heshima zao za mwisho katika Jeneza la aliyekuwa Mkuu wa kitengo cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, James Kombe, aliyezikwa Jana Nyumbani kwake, kijiji cha Msae, Kata ya Mwika, wilaya ya Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro.

Baba yake Wema Sepetu afariki Dunia leo Hospitali ya TMJ

Balozi Abraham Isaac Sepetu amefariki Dunia mapema leo akiwa katika Hospitali ya TMJ alikokuwa amelazwa akitibiwa ugonjwa wa Kisukari na kiharusi alioupata hivi karibuni mjini Zanzibar. 

Balozi Sepetu, ambaye pia ni baba mzazi wa Miss Tanzania 2006, Wema Isaac Sepetu, hadi anapatwa na ugonjwa na hatimaye mauti, alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Uwekezaji wa Vitega Uchumi Zanzibar.

Taarifa zaidi za msiba huo zitaendelea kukujia kadri zitakavyofika katika meza yetu, huku tukiamini kuwa msiba huo utakuwa umegusa hisia za wengi, wakiwamo mashabiki wa sanaa wa mwanadada Wema Sepetu.

 

Yanga waitangazia hatari Mgambo JKT

NaKambi Mbwana, Dar es Salaam
TIMU ya Yanga, imeitangazia hali ya hatari Mgambo JKT, ikisema itahakikisha inaibuka na ushindi mnono katika mchezo huo uliopangwa kufanyika Jumanne ya Oktoba 29 katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Kocha msaidizi wa Yanga, Fredy Minziro.
Mechio hiyo inachezwa huku Yanga wakiwa na shauku ya kuibuka na ushindi huo ili iweze kujiweka pazuri katika patashika ya Ligi ya Tanzania Bara, ambapo katika mechi iliyopita, mabingwa hao watetezi waliibuka na ushindi wa bao 3-0 dhidi ya Rhino Rangers ya mjini Tabora.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Fredy Minziro, alisema kwamba timu yao imeanza mazoezi kwa ajili ya kujiwinda na Mgambo huku wakiwa na hamu ya kushinda dhidi ya Mgambo JKT.

Alisema kuwa kikosi chao chote kimeanza mazoezi makali kwa ajili ya mechi hiyo itakayokuwa na ushindani wa aina yake, kutokana na timu zote mbili kutaka kushinda  dhidi ya mwenzake, jambo ambalo kwa upande wa Yanga wanakabiliana nalo.

Papii Kocha na baba yake wataka Watanzania wawaombee

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWANAMUZIKI Papii Kocha, anayetumikia adhabu ya kifungo cha maisha jela, amewataka Watanzania wamuombee ili aweze kutoka na kurudi katika maisha yake ya uraiani.

Papii aliyasema hayo jana alipotembelewa na wadau mbalimbali wa muziki wa dansi, wakiwamo wale wanaounda muungano wa kundi la Bongo Dansi, linalopatikana katika mtandao wa kijamii facebook.
Wanamuziki Papii kocha kushoto na baba yake Nguza Viking wakiwa na nyuso za huzuni katika picha za matukio yao ya kuhukumiwa kifungo cha Maisha Jela. Wanamuziki hao sasa wanamatumaini kidogo baada ya Mahakama ya Rufaa kukubali kupitia vifungu vya sheria iliyowatia hatiani.
Akizungumza kwa masikitiko makubwa, alisema dua ndio zinazoweza kumrudisha uraiani yeye na baba yake Nguza Viking, maarufu kama Babu Seya, baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na makosa ya ubakaji.

Papii aliyasema hayo baada ya kupata maatumaini kutokana na Mahakama ya Rufaa kukubali kufanya marejeo (review) ya jinsi walivyotuhumiwa na kukutwa na makosa hayo kiasi cha kupewa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani.

Mwidau CUP yarindima Wilayani Pangani mkoani Tanga, huku ikitarajia kutumika zaidi ya mili 20


Na Mwandishi Wetu,Tanga

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga, Amina Mwidau kupitia Chama cha Wananchi(CUF),  amezindua rasmi ligi ya Mwidau Cup inayoshirikisha timu 45 za Wilaya ya Pangani yenye kata 13 huku zaidi ya sh.milioni 20 zikitarajiwa kutumika hadi kumalika kwa ligi hiyo.
 Mbunge Amina Mwidau, akikagua timu huku akiwa na viongozi wa timu ya Black burn kabla ya mchezo kuanza.

Kwa mujibu wa Mwidau lengo la mashindano hayo si kupata tu mshindi kwa ajili ya kuchukua zawadi, bali anataka kuona vipaji vya soka vinaibuliwa kwa kuwa soka ni ajira na wakati huo huohuwaunganisha wananchi pamoja na hiyo ndio dhamira yake kwa Wilaya ya Pangani na Tanga kwa ujumla.
 Mbunge Amina Mwidau, akikagua timu huku akiwa na viongozi wa timu ya Black burn kabla ya mchezo kuanza.

Akizungumza katika Uwanja wa Kumba Wilayani Pangani wakati akizindua ligi hiyo, Mwidau alisisitiza umuhimu kwa timu ambazo zinashiriki kuonesha uwezo wao wa kusakata soka na  anatamani kuona Wilaya ya Pangani inakuwa chachu katika maendeleo ya soka kwa mkoa wa Tanga.
Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Tanga, Amina Mwidau (CUF), akifutiliana kwa makini pambano la soko kati ya timu ya Black burn na Nondo (kulia), ni Katibu Msaidizi wa Chama cha Soko Wilaya ya Pangani, Mohamed Swazi, katika pambano hilo timu ya Black burn iliibuka na ushindi wa bao 4-1.


“Malengo yangu ni kuona tunapata vipaji vya soka kwa vijana wetu maana uwezo wanao. Hivyo nimeamua kuanza na Wilaya ya Pangani kwa kudhamini ligi hii nikiwa na maana ya kupata sehemu ya kuanzia katika kuhakikisha Mkoa wa Tanga unakuwa na ligi ya aina hii,”alisema.

Saturday, October 26, 2013

Rais Kikwete aagana na Balozi wa Pakistan nchini Tanzania

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na Balozi wa Pakistan nchini Mhe Tajammul Altac aliyefika Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 26, 2013 kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kufanya kazi.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika mazungumzo na Balozi wa  Pakistan nchini Mhe Tajammul Altac aliyefika Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 26, 2013 kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kufanya kazi. PICHA NA IKULU

Ikiwa ni kweli, bundi anaunguruma juu ya paa la Chadema, pitia walaka wa Samson Mwigamba, Mwenyekiti wa Chadema aliyesimamishwa jijini Arusha

 Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson Mwigamba, aliyesimamishwa, ambaye ndio aliyotoa walaka huu.
"Wito kwa wana CHADEMA wote!

Kufuatia malumbano yanayoendelea kwenye vyombo vya habari na madhaifu mengi ambayo tumeshayashuhudia kwenye chama kwa sasa, natoa wito kwa wana CHADEMA wote nchini kwamba wakati umefika tubadilishe uongozi wa juu wa chama.

Kihistoria, CHADEMA kati ya mwaka 2005 na 2010, agenda zetu kwa wananchi zilikuwa mbili. Kupiga vita ufisadi, iliyosukumwa sana na Dr. Slaa na ile ya utetezi wa raslimali zetu iliyobebwa na Zitto. Lakini sasa hivi chama kinaenda kwa matukio.

Naandika nikiwa mwana CHADEMA safi na nataka kila mwanachama atakayesoma atulie na kutafakari. Hili siyo jambo la ushabiki. Ni mawasiliano baina yetu wana CHADEMA na tunahitaji tutulie na kutafakari.

Nimekuwa mwanachama wa siku nyingi na nimebahatika pia kuwa kiongozi ndani ya chama kwa nyakati tofauti kwahiyo naelewa ninachokiandika. Nadriki kusema kwamba kwa sasa chama kinakwenda kwa matukio na ni bahati tu kwamba CCM inaendelea kutupatia matukio lakini CCM na serikali yake wakitunyima matukio, CHADEMA chini ya Mkt Mbowe, Katibu mkuu Slaa na Naibu Zitto utakuwa ndo mwisho wake.

CHADEMA iliyopiga kelele sana dhidi ya ufisadi, CHADEMA iliyopiga kelele mpaka sheria ya vyama vya siasa ikabadilishwa na vyama kutakiwa kukaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), eti leo inaungana na CCM kumshambulia mwenyekiti wa kamati ya bunge ya hesabu za serikali (PAC) kwa kutamka kwamba vyama havijawasilisha ripoti zake za fedha zilizokaguliwa. Kwa nini? Muungano huu wa CHADEMA na CCM maana yake nini? Kama chama kinajiamini ni kisafi kwenye hesabu zake hofu ni ya nini? Si wasubiri kikao na kamati ya bunge katibu mkuu aende na hizo ripoti na nyaraka zinazoonyesha kweli wamewasilisha hesabu hizo?

Napenda kabla sijaendelea mbele kuwapongeza wenyeviti wetu wawili wa kwanza ambao kimsingi waliweka msingi mzuri sana wakutong’ang’ania madaraka na badala yake kuachia mapema na kumwachia mwinginekidemokrasia bila vurugu. Hawakuwa madikteta na nawapongeza sana. Walijitahidi sana kutokuwa wapenda madaraka na kimsingi walituwekea utamaduni ambao walitaka wote tuufuate na kujenga taasisi imara inayojali demokrasia na haki ya kilamwanachama.

Makamu wa Rais Dkt Bilal aweka jiwe la msingi mradi wa hifadhi ya mazingira mkoani Kigoma



 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiangalia na kusikiliza maelezo kuhusu maandalizi ya jinsi ya kukamua mafuta ya Mawese kutoka kwa Meneja wa mradi wa Hifadhi ya Mazingira ya Ziwa Tanganyika, Seleboni John Mushi, wakati Makamu alipozindua mradi huo jana Igalula, Wilaya ya Uvinza Mkoa wa Kigoma. Dkt. Bilal, alitembelea na kukagua mradi huo unaosimamiwa na Ofisi yake na kujionea jinsi mafuta hayo yanavyopatikana. 
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiweka Jiwe la Msingi katika Mradi wa Hifadhi ya Mazingira wa Vikundi vidogo vya Uchakataji Mawese Igalula Mkoa wa Kigoma, wakati wa hafla hiyo iliyofanyika jana Wilayani Uvinza. Kulia ni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Sazi Salula. Mradi huo unasimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza maelezo kuhusu ukamuaji wa mafuta ya Mawese Kaimu Meneja wa kutoka kwa Meneja Sido Mkoa wa Kigoma, Gervas Ntahamba, wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi huo iliyofanyika jana Igalula, Wilaya ya Uvinza Mkoa wa Kigoma. Dkt. Bilal, alitembelea na kukagua mradi huo unaosimamiwa na Ofisi yake na kujionea jinsi mafuta hayo yanavyopatikana.Picha na OMR

Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa akoleza moto wa urais TFF

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, amewataka wajumbe wa Mkutano wa Mkuu wa Shgirikisho la Soka nchini (TFF), kufanya uamuzi sahihi kwa kuchagua viongozi makini katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Jumapili, katika Ukumbi wa Golden Tower, jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, pichani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa katika vyombo vya habari na Lowassa, wajumbe kufanya uamuzi mzuri katika uchaguzi huo ni hatua ya kukuza soka la Tanzania.


Alisema kuwa hatua hiyo inatokana na rais wa sasa, Leodgar Tenga kumaliza muda wake na kuanza mchakato wa kupatikana mrithi wake katika uchaguzi ulioandaliwa na Shirikisho hilo, huku nafasi ya urais ikiwaniwa na Athuman Nyamlani na Jamal Malinzi.


“Nikiwa Kama mmoja wa wadau wa mchezo wa soka, nimekuwa nikifuatilia harakati za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa TFF siku ya jumapili, ambapo ni
siku muhimu kwa soka la Tanzania.


“Ni siku ambayo wajumbe watatuchagulia viongozi wa kuliongoza soka letu na kuendeleza juhudi za Rais wetu Dk. Jakaya Kikwete katika kusaidia mpira wa miguu hapa nchini,” ilisema taarifa hiyo.


Lowassaa
liwaomba wajumbe wachaguwe watu watakao endeleza juhudi hizo zenye kuhakikisha kuwa mpira wa miguu unasonga mbele na kulitangaza Taifa katika Nyanja za Kimataifa.


Aidha, Lowassa pia alimpongeza Tenga kwa kuweka msingi imara kuliongoza soka la Tanzania, akiamini ndio mchezo unaopendwa na watu wengi, hivyo kutaka sheria zifuatwe, huku tukilazimika kuingia kwenye mfumo wa utendaji unaolazimisha kupatikana kwa maalum za soka.

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...