Mkuu wa Wilaya Handeni, Muhingo Rweyemamu
Na Rahimu Kambi, Handeni
SERIKALI imeleta tani 150 za mahindi
ambazo zimeanza kusagwa kwa ajili ya kuwauzia wananchi kwa bei nafuu isiyozidi
Sh 900 kwa kilo moja, kitendo kitakachoweza kupunguza tatizo la njaa wilayani hapa.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya
Handeni, Muhingo Rweyemamu, alipozungumza na Handeni Kwetu juu ya kupambana na
njaa wilayani kwake.
Akizungumza zaidi, Muhingo alisema
kwamba chakula hicho kitauzwa zaidi kwa kata na vijiji vilivyoathiriwa sana na
tatizo la njaa wilayani humo.
Alisema kwa kufikishiwa chakula
hicho, wananchi wake watapata unafuu wa kiasi fulani, hasa kwa kununua kwa bei
nafuu tifautisha na bei ya sasa.
"Chakula kimeshafika na sasa
kimeanza kusagwa ili unga uuzwe kwa bei nafuu kwa ajili ya kuwapa unafuu
wananchi katika baadhi ya kata zilizoathiriwa zaidi na tatizo la njaa.
"Naamini sehemu kama vile
Sindeni, Kwamsisi, Kwedikabu, Kwasunga na kwingineko kulikokumbwa na tatizo
hilo chakula hicho kitafika, ikiwa ni mipango mizuri ya serikali juu ya
kukabiriana na tatizo la njaa," alisema Rweyemamu.
Wilaya ya Handeni ni miongoni mwa
maeneo yanayotajwa kuwa na njaa inayosababisha baadhi ya wananchi wake kukosa
chakula, hivyo kuhangaika hasa kwa kula mboga mboga na matunda mengine,
yakiwamo maembe.
No comments:
Post a Comment