MAMBO FULANI MUHIMU
Picha inajieleza kabisa. Hawa ni wapenzi wanaofurahia 'love yao'.
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
KATIKA suala zima la mapenzi, kuna baadhi ya vitu ambavyo
ukikutana navyo unaweza kushikwa na bumbuwazi. Ni pale mtu anapotumia muda
mwingi kushindana na mtu wake.
Ni ngumu sana. Ni wakati wa kila mtu kujua kuwa, binadamu
tupo kwa jinia mbili tofauti. Alivyoumbwa mwanamume si sawa na alivyoumbwa
mwanamke.
Katika hilo, viumbe hivi viwili, kila moja ina hulka yake.
Kwa mwanamke, mara kadhaa amezoea kudekezwa hasa katika suala zima la mapenzi,
anapogundua yupo kwa mtu anayempenda.
Mwanamke wa aina yoyote, hata kama awe na umbo gani, lakini
bado atakuwa chini, akijitia madeko kila anavyopenda. Si vibaya, hasa kama
anamdekea mpenzi au mume wake.
Kutokana na hilo, sisi wanaume ni lazima tujuwe namna ya
kuishi na viumbe hawa ili kuwapatia raha zaidi. Si vizuri kuwa wakali muda wote
hadi kufikia kuwaogopesha.
Tukifanya hivyo, hamu ya kuwa na waume zao kila mara
inakwisha, hasa kwasababu ya kero, matatizo ya kushindwa kujua unavyokaa na
mwanaume mwenzako tofauti na mwanamke.
Hata kama uwe na pumzi vipi katika suala zima la mapenzi,
lakini kwasababu huwezi kuwa mbunifu, kujua kudekeza, mpenzi wako, mke wako
hawezi kujisikia raha kuwa na wewe kila wakati.
Zaidi, atakuwa radhi kutumia muda wake mwingi kuzungumza na
marafiki zake, ndugu zake, akisingizia kila anavyoona inafaa, maana wewe sio
mtu wa kumpa raha zaidi ya karaha.
Ingawa madeko yakizidi pia si mazuri, lakini pia lazima mtu
ajuwe hakuna mwanamke ambaye hapendi kudekezwa. Na anapogundua wewe tabia hiyo
huna, hakika atakuwa mnyonge.
Haya si mapenzi ya kuiga. Maana hata kwa wanaume, baadhi yao
nao huona raha kudeka kwa wasichana wao. Haya ndio mapenzi, hasa yanapotokea
watu wote wanapenda kwa dhati.
Endapo mmoja wapo hana upendo wa dhati kwako, hakika hawezi
kukubali umdekee, au akudekee bila sababu za msingi. Huo ndio ukweli, hivyo
ifikie wakati tujuwe namna ya kuishi na watu wetu.
Samahani, kusema mpenzi, sina maana kuwa sizungumzii ndoa
zaidi ya wapenzi tu kama alivyowahi kusema msomaji wangu mmoja, aliyetaka
nizame zaidi kwa watu waliofunga ndoa.
Ni maoni yake, lakini wengi wanaopitia katika uchumba,
upenzi, baadhi yao ndio wanaokuwa wana ndoa. Tuombe Mungu, ila pamoja na hayo
yote, hata wenye ndoa zao, wakati mwingine kudekeana ipo.
Mtu anaweza kujifanya ni mgonjwa sana. Kumbe mwongo tu.
Ukimwambia basi ingia chumbani ukalale, hataki, anataka alale sebuleni tu.
Ila ukiendelea kumliwaza, kumshika hapa na pale, kumpa
maneno matamu ya mahaba, kujikunja kwake kunakwisha na badala yake hisia za
sita kwa sita zinamjia, hivyo kuingia mchezoni.
Hata kama mwanaume hakuwa na hamu ya kufanya tendo la ndoa,
lakini kwakuwa amemkuta mpenzi, au mke wake yupo katika hali ya unyonge, naye
akatumia uanaume wake, anajikuta anataka kulipa deni la kudeka kwa mtu huyo
ambaye mwisho wa siku hujikuta akivuja jasho la furaha.
Lakini kwa bahati mbaya, wenzangu na mimi wanapowakuta
wapenzi wao wamekaa, wakitaka kudeka, nao hukunja uso, maana hawataki kudekewa
hivyo kuwanyong’onyeza zaidi.
“Usitake kunisumbua bwana. Sasa kama unaumwa, au hujielewi
si uende hospitali kuliko kunidekea mimi,” hizi ni kauli za kusikitisha kama
zinatokana katika kinywa cha mwanaume.
Mbaya zaidi, kesho wanaume hao huanza kulalamika kuwa
wananyimwa unyumba, yani tendo la ndoa. Huu ni ujinga kabisa. Ni jambo gumu
mwanamke kutamka kuwa anataka kitu fulani.
Zaidi huonyesha hisia kwa njia mbalimbali, ikiwamo kudeka, hivyo wewe kama hutaki basi
itakula kwako. Nadhani kwa kulijua hilo, tuna kila sababu ya kuangalia mwenendo
wetu.
Lazima tujuwe pia mwanamke ili aweze kutulia ni lazima ajuwe
kwako akideka, atabembelezwa kwa sababu mbalimbali, hivyo ukali hausaidii, hasa
ukijua mwanamke huyo ni chaguo lako sahihi.
Raha ya mapenzi hapo ndipo inapokolea. Vinginevyo, tutayaona
machungu na yenye ukakasi mkubwa.
Tukutane wiki ijayo.
kambimbwana@yahoo.com
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment