Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
CHAMA cha Mpira wa Miguu Ilala (IDFA), kimeandaa kozi ya
waamuzi itakayofanyika Januari 25, katika Shule ya Sekondari ya Benjamin Mkapa.
Pichani ni Kanuti Daudi kushoto aliyeshikana mkono na mmoja watoto kwenye majukumu ya kila siku, IDFA.
Kozi hiyo imeandaliwa kwa ajili ya kutafuta waamuzi wapya
watakaoandaliwa vyema na kutumiwa siku za usoni, hasa kwa wale vijana wadogo,
huku ikipangwa kufanyika siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili kwa muda wa mwezi
mmoja.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Chama
hicho, Kanuti Daudi, alisema kwamba hadi sasa wameshajiandikisha vijana 20
wenye lengo la kushiriki kozi hiyo ya waamuzi.
Alisema bado nafasi zipo kwa wale wanaohitaji kozi hiyo,
huku wakiamini kuwa italeta tija na kuinua michezo kwa kuwa na waamuzi bora.
"Tumeamua kuandaa kozi ya waamuzi kwa ajili ya kutafuta
watu wa kuendeleza zaidi michezo hasa mpira wa miguu, kwa kuhakikisha mambo
yanakwenda sawa.
"Naamini mambo yatakuwa mazuri hasa kwa wale vijana
watakaojitokeza zaidi kwakuwa bado nafasi zipo na tunaamini watashiriki kwa
wingi," alisema.
DRFA ni chama kinachopigania maendeleo ya mpira wa miguu
Ilala, huku timu kongwe na zenye mashabiki wengi, ikiwamo Simba na Yanga
zinazotokea katika eneo hilo.
No comments:
Post a Comment