Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dk. Hamisi Kingwangalla akiwasili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alipofanya ziara ya kushtukiza hospitalini hapo, Januari 4, 2016. Picha zote na Zainul Mzige.
Na Rabi Hume, Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dk. Hamisi Kingwangalla amefanya ziara, Januari 4, 2016 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kutembelea idara mbalimbali za hospitali hiyo kuona jinsi ya ufanyaji kazi. Baadhi ya idara ambazo, Dk. Kingwangalla alitembelea ni pamoja na Kitengo cha dharura, Chumba cha wagonjwa Mahututi (ICU), wodi ya Mwaisela, duka la dawa la MSD na kukagua ufanyaji wa kazi wa mashine ya CT-Scan na MRI. Akizungumzia ziara hiyo mara baada ya kutembelea Hospitalini hapo, Dk. Kigwangalla ameeleza kuwa ili kuweza kuona hali ya utendaji wa kazi iliyopo katika hospitali hiyo ya taifa tangu ambapo Rais, Dkt. John Pombe Magufuli alipofanya ziara ya kushtukiza na kutokuridhishwa na utendaji kazi wa hospitali hiyo hali iliyopelekea kuivunja bodi iliyokuwa ikisimamia hospitali.
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dk. Hamisi Kingwangalla akitoka katika ofisi ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo.
Dk. Kingwangalla alisema amefurahishwa na utoaji wa huduma katika upimaji kwa kutumia mashine ya CT-Scan na MRI ambazo awali wakati wanaingia madarakani hazikuwa katika hali nzuri ya ufanyaji wa kazi na kuwataka watumishi wa hospitali hiyo kufanya kazi kwa bidii na kuifanya hospitali hiyo kuonekana yenye hadhi ya kuwa hospitali ya taifa. Alisema limekuwa jambo ambalo linasikitisha kuona huduma zinazopatikana katika hospitali ya taifa zinashindwa na huduma zinazotolewa katika hospitali za watu binafsi na akilinganisha huduma za kulipia vitanda zinazotolewa Muhimbili kuwa hazina viwango vya juu ambavyo vinaweza kuwashawishi wananchi wenye uwezo kuacha kwenda hospitali binafsi na kwenda hospitalini hapo.