Na Kambi Mbwana, Morogoro
WAKATI mwili wa
Albert Mangwea ukitarajiwa kuzikwa leo hapa mkoani Morogoro, jana katika kuaga
viwanja vya Leaders Club, mashabiki wa muziki wa kizazi kipya, walitoa kali
baada ya kuacha msiba wa msanii Ngwair na kuanza kumkimbilia nyota mwingine wa
muziki huo, Nassib Abdulmalilck, maarufu kama Diamond.
Ngwair enzi za uhai wakeNgwair alivyoletwa juzi
Ngwair alivyoagwa jana.
Hiyo ilitokea jana
katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni, kulipofanyika tukio la kumuaga
msanii Mangwea, aliyefariki nchini Afrika Kusini Jumanne ya wiki iliyopita na
kuzua huzuni kubwa katika tasnia hiyo.
Mwili wa Mangwea
uliwasili viwanjani hapo saa 2:00 ukitokea Hospitali ya Taifa, Muhimbili,
alipohifadhiwa juzi, mara baada ya kuletwa ukitokea nchini Afrika Kusini
alipofia.
Hali ya utata katika
shughuli hiyo ilianza kuonekana tangu mapema, baada ya wadau na mashabiki
kuanza kuzengea katika sehemu waliyokaa wasanii, ikionyesha kuwa walikuwa na
shauku ya kuwashika wasanii waliokuwapo uwanjani hapo kwa ajili ya kumuaga
mwenzao.
Vurugu za Diamond
zilianza baada ya kumaliza shughuliza kumuaga msanii mwenzake, hivyo kuamua
kuondoka uwanjani hapo, jambo lililosababisha umati wa watu kuanza kumkimbilia.
Hata hivyo jeshi la
Polisi na vijana wa ulinzi wa usalama waliingilia kati, kwa ajili ya kudhibiti mwingiliano
na haja ya mashabiki hao ambao kwa kawaida walianza kutishia usalama wao na
tukio zima la kumuaga marehemu Ngwair.
Hata hivyo, hii si
mara ya kwanza kwa Diamond, maana vurugu kama hizo ziliwahi kuibuka alipokwenda
kwenye msiba wa msanii wa maigizo na filamu, marehemu Steven Kanumba na
kujikuta idadi kubwa ya watu kutaka kumuona kwa ukaribu au hata kumshika mkono.
Awali, Diamond
alimuelezea marehemu Ngwea kama moja ya wasanii wenye uwezo mkubwa wa kuimba,
huku akiweza kuishi kwa upendo na wasanii wote, tangu alipojiingiza kwenye
muziki.
“Nimeguswa sana na
msiba wa Ngwair, naamini pengo lake haliwezi kuzibika, maana jamaa alikuwa na
uwezo mkubwa mno katika tasnia hii, akitamba na nyimbo nyingi zilizowafurahisha
watu wote,” alisema Diamond.
Naye Mbunge wa
Kinondoni, Idd Azzan, alimuelezea Ngwea kama mhimili kwenye sanaa ya muziki wa
kizazi kipya, huku akisema wadau, akiwamo yeye hataweza kuusahau mchango Ngwair.
“Ni mmoja wa wasanii
mahiri mno katika tasnia nzima ya Bongo Fleva, hivyo naamini tutaendelea
kumuenzi na kuhakikisha kuwa mchango unakuwa tunu katika soko la muziki huu,”
alisema Azzan.
Watu wengi walijitokeza
katika kumkuaga Ngwair, wakiwamo wanasiasa, viongozi wa serikali na vyama vya
siasa, hasa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), waliowakilishwa na
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa (BAVICHA), John Heche, Msemaji wao Tumaini
Makene na viongozi wengine ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani kwa sasa.
Heche aliwahakikishia
wasanii kuwa chama chao kitaendelea kupambana vikali kuibana serikali juu ya
maslahi ya wasanii kwenye kazi zao, akiamini kuwa viongo wao, akiwamo mbunge wa
Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Zitto Kabwe, John Mnyika na wengineo
wanaendelea kuipigania sanaa nzima kwa kuwapo kwenye mijadala mikubwa ya
kitaifa.
“Sisi kama Chadema
tumekuwa hodari mno kupigania sanaa ya Tanzania, ndio maana tunasema tutafanya
juhudi kubwa kuhakikisha kuwa wasanii wananufaika, ukizingatia kama msanii
amefanya kazi nyingi na anakosa maendeleo, anaweza kupata matatizo hata
kisaikolojia,” alisema Heche.
Kwa hakika, kila
aliyepata nafasi ya kumuelezea marehemu Ngwea, aliitumia nafasi hiyo kumuombea
dua njema marehemu Ngwair, sambamba na kuwataka wasanii watumie muda huo
kumuombea dua njema.
Idadi kubwa ya
wasanii walilimika katika viwanja vya Leaders Club, akiwamo Mrisho Mpoto, Ommy
Dimpozi, Madee, Fid Q, Profesa Jay, AY, Mwana FA, Lady Jay Dee, Barnabas,
Keisha, Dogo Dito, Q-Chillah, Kassim Mganga, Feroos, Joti na wakali kibao
waliojitoa kwa hali na mali kwa ajili ya kumuaga marehemu Ngwea katika viwanja
vya Leaders Club.
Marehemu Ngwair anatarajiwa
kuzikwa leo katika makaburi ya Kihonda, mkoani Morogoro, huku idadi kubwa ya
watu, wakiwamo wadau, mashabiki na viongozi mbalimbali wa Mkoa wakitajwa
kushiriki katika msiba huu.
Kamati ya Mazishi iliyosaidiwa
kwa kiasi kikubwa na Shirikisho la Muziki Tanzania, chini ya Rais wao, Addo
Novemba, waliweka utaratibu mzuri, japo kasoro za hapa na pale hazikosekani
katika matukio ya kuaga marehemu ambaye alikuwa na jina kubwa katika jamii
yake.
Eneo alililozwa
marehemu Ngwea, kuliwekwa uzio ambao ilibakizwa njia tu ya kupita watu
waliokwenda kumuaga marehemu, huku nyuma ya mwili wa marehemu kukiwa na maeneo
yaliyotengwa kwa ajili ya viongozi mbalimbali, ndugu wa marehemu, Kamati ya
Mazishi na wasanii wote, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha kuwa shughuli za uagaji
zinafanyika bila kuleta hatari yoyote kwa waliokwenda Leaders Club.
Wakati wanamuaga
marehemu Ngwea, kila mmoja alikuwa akitoa ishara anayojua mwenyewe, ikiwamo
saluti, dua kwa Wakristo na Waislamu, wakiwa na haja ya kumuombea marehemu Ngwair.
Hapa mkoani Morogoro,
hali ya utulivu imeonekana kuonekana, huku mashabiki mmoja baada ya mwingine
wasikika wakizungumzia msiba huu ulioletwa kwa ajili ya maziko.
No comments:
Post a Comment