Msanii mahiri wa maigizo na filamu, Sinta.
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
HALI inazidi kuwa mbaya kwa vurugu na maandamano, baada ya
wasanii kutangaza kufanya maandamano mfululizo, endapo Serikali itaendelea
kuchekea dhuluma na manyanyaso wanayoendelea kufanyiwa wasanii hapa nchini.
Lulu
Haya yalithibitika rasmi mwishoni mwa wiki iliyopita, baada
ya wasanii wa maigizo na filamu kuitisha mkutano wao katika Ukumbi wa Vijana,
Kinondoni, kwa ajili ya kuangalia changamoto zinazowakabili katika tasnia hiyo
ya filamu.
Wema Sepetu na Steve Nyerere
Kila msanii wa filamu na viongozi wao kwa ujumla, malalamiko
yao ni juu ya watendaji wa COSOTA na Bodi ya Filamu, inayoongozwa na Mkurugenzi
wake, Joyce Fisoo.
Mbaya zaidi, wasanii hao wameanza kutishia kufanya
maandamano makubwa kushinikiza serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
kuangalia na kuthamini haki zao.
Tatizo si maandamano ya Wasanii, maana sio kitu kipya, ila
wasiwasi wangu kitatokea nini katika maandamano hayo? Kwanini nasema hivi;
wasanii wana nguvu mno.
Kichwa cha msanii mmoja na nguvu yake katika jamii,
hailingani hata kidogo na vichwa vya wanasiasa 10 katika ardhi hii. Huu ndio
ukweli, hivyo ni wazi tuujadili kwa faida yetu.
Serikali, chini ya Waziri wake wa Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo, Dk Fenella Mukangara na Naibu wake, Amos Makalla, kuna haja ya
kufanyia kazi kero hizo.
Najua wameshafanya vikao kwa ajili hiyo, lakini matokeo yake
bado sio suluhisho, maana wasanii wanaendelea kulia na wakitangaza
kutokubaliana na chochote kutoka COSOTA.
Wasanii hao na viongozi wanalalamikia sheria zilizotungwa
kwa ajili ya kusimamia soko la filamu kutokuwa na mashiko na faida yoyote kwa
upande wao, zaidi ya kunufaisha wafanyabiashara.
Sitaki kusema nani mwenye hoja katika suala hilo, ila ni
kuwataka serikali na wasanii hao kukaa tena kwa ajili ya kujenga suala hilo.
Kwanini malalamiko hayo yanazidi kuwa makubwa? Je, ni kweli
wasanii hao wanawaonea watendaji wa COSOTA na Bodi ya Filamu? Tozo au uhakiki
wa kupitia filamu zao umeangaliwa kuwa ni msingi wa maendeleo ya sanaa yao?
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Tanzania
(TDFAA), Michael Sangu, sheria zilizotungwa kwa ajili ya wasanii haziwezi
kuboresha maisha yao zaidi ya kuwanyonya.
Suala hilo litazidi kuongeza maisha duni kwa wasanii
Tanzania na kuwafanya wafe hoi bila kuwa na kitu chochote cha maana walichovuna
enzi za uhai wao, kama walivyokuwa wengineo wakiwa weupe, ingawa walikuwa na
majina makubwa.
Hatuwezi kwenda hivyo. Hii nchi ili iweze kusonga mbele
lazima kila jamii awe na maelewano na mwenzake, hivyo suala hili la malumbano
baina ya wasanii na serikali haliwezi kufumbiwa macho.
Kwa mfano, nguvu ya wasanii mitaani inaweza kusababisha
mvurugano wa amani pale watakapoamua kweli kuandamana kwa hali yoyote ile.
Pamoja na maandamano hayo, pia wadau na mashabiki wao
wanaweza kuwaunga mkono kwa dhati, bila kusikiliza maneno ya wanasiasa, iwe
waziri, mbunge au diwani.
Hawa wakiachiwa ovyo ovyo hata jamii itapata hasara kubwa,
pale watakapowalisha sumu mbaya ya kile wanachovuna kutoka kwenye serikali yao
ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
Kwa mfano, wasanii wanalalamika kuwa mchakato mzima wa
kanuni za utekelezaji wa sheria ya filamu na michezo ya kuigiza Tanzania Bara
haukuhusisha wasanii kwa ajili ya kuangalia kile wanachokutana katika uandaaji
wa kazi zao.
Kila msanii anayezungumzia sakata hilo, anakuwa mwenye
jazba, huku wengine wakitangaza kuwa kamwe hawatatoa ushirikiano kama sheria
zilizotungwa hazitarekebishwa, ikiwamo ile tozo iliyowekwa, wakisema ni kubwa.
Serikali kwa kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo inapaswa kuliangalia hilo kwa haraka kabla ya kuzidi kuingiza
chokochoko katika vuguvu vugu hizo za wasanii kwa kusikiliza kilio cha wasanii
wao.
Kuna mengi yapo chini ya pazi. Watendaji wa COSOTA na Bodi
ya Filamu hawana ushirikiano mzuri na wasanii pamoja na viongozi wao. Hili
litachelewesha maendeleo kwa ujumla wake.
Huu ndio ukweli, maana kinachoendelea sasa, kinaweza kuibua
hisia mbaya kwa wasanii, jamii na viongozi wa serikali kwa ujumla. Itakuwa ni
nchi ya malalamiko kila siku?
Wasanii wetu watakuwa chini wakigalagazwa kila siku, huku
tukijua umuhimu wao katika kuelimisha jamii, ukizingatia kwamba sanaa imetumika
kuiweka nchi hapa ilipo sasa.
Hakuna njia ya mkato katika hilo, hivyo naamini viongozi
wahusika na wanasiasa wanaweza kuupitia upya sakata la wasanii na maslahi yao,
ili iwe njia ya mafanikio yao kwa ujumla.
0712 053949
0753 806087
No comments:
Post a Comment