https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Tuesday, January 01, 2013

Mjasiriamali anayelia na masharti ya mikopo



Mama Kipande akiandaa kuku
 
Na Kambi Mbwana, Aliyekuwa Korogwe 
KADRI siku zinavyozidi kusonga mbele, akina mama wengi wanaendelea kuchangamkia kazi mbalimbali zinazoweza kuinua maisha yao na familia zao kwa ujumla.

Wakati wengine wanashiriki kazi zinazotumia akili na nguvu, wapo wengine wanaomenyeka kwenye ujasiriamali kwa kumiliki migahawa, cafe na hoteli katika sehemu mbalimbali za Tanzania, ukiwa ni mpango wa kuboresha maisha yao. 

Kutokana na hilo, familia nyingi zimekuwa zikiishi vyema hasa kwa wale ambao wazazi wao wamekuwa wakishiriki kufanya kazi kwa namna moja ama nyingine. 
Mama Kipande kushoto akiandaa kuku mgahawani kwake

Sio katika majiji tu yenye mchanganyiko wa watu wengi, bali hata kwenye miji inayoendelea, ukiwamo wilaya ya Korogwe watu hufanya bidii mno katika kazi zao kwa ajili ya kuinua uchumi wao na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza na Handeni Kwetu, Mama Kipande anasema akiwa kwenye mgahawa wake huo uliopo Manudu, wilayani Korogwe, mkoani Tanga kuwa biashara yake hiyo inampa ahueni nyingi za kimaisha kutokana na watu wengi kuchagua kupata chakula kwake.
Kwa jinsi watu walivyokuwa wakipata chakula huku wakizungumzia hili na lile, lilinifanya niulize kuwa wingi wao ni wa kila siku au la.
Kwa jinsi mji wa Korogwe unavyozidi kupanuka, hata suala la biashara kwa wajasiriamali linazidi kufanya vyema, huku bidhaa kama vile unga, mchele, mafuta ya kula, maharage na bidhaa nyingine zikiuzwa kupita kiasi.
Mama Kipande anasema biashara yake hiyo ni ya zamani na kila mmoja anamjua kutokana na kuifanya kwa muda mrefu.
Anasema watu mbalimbali wamekuwa wakienda kwenye mgahawa wake kupata chain a chakula cha mchana, huku yeye akihakikisha kuwa huduma nzuri na chakula safi kinapatikana katika mgahawa wake huo.
“Hii ni biashara niliyodumu nayo kwa miaka zaidi ya 20 sasa, huku nikishukuru kwakuwa watu wananiunga mkono na nafanya biashara nzuri na kuimudu familia yangu.
“Vyakula vya kila aina vinapatikana katika mgahawa wangu, huku nikipokea watu kutoka kada mbalimbali, ukizingatia kwamba chakula changu ni kizuri na kinapendwa na watu wengi,” alisema Mama Kipande.
Kwa siku anauza kuku wasiopungua 10 katika mgahawa wake, wakati mchele anapika kilo nane hadi 10 kulingana na biashara kwa siku inavyochanganya na watu wanavyokwenda kupata chakula.
Mjasiriamali huyo anasema kwamba mgahawa wake unatumia unga wa sembe kilo 25 kwa siku tatu, huku unga wa ngano kiloba cha kilo 25 ukitumika kwa siku mbili tu, huku mafuta ya kula dumu moja la lita 18 likitumika kwa siku moja.
Kutokana na biashara hiyo kwenda vizuri, wakati mwingine hukutana na vikwazo vya hapa na pale, vikiwapo vya kuondoshwa katika nyumba anazofanyia biashara yake kwasababu zisizoeleweka.
Hata hivyo, wateja wake wengi wamekuwa wakimuelewa na kumfuata popote anapokuwa, jambo linalompa mwangaza kuwa biashara yake imeshajijenga yenyewe na watu wanapenda huduma yake kila siku ya Mungu.
Awali biashara yake alikuwa akiifanya Old Korogwe, lakini aliamua kuondoka baada ya kuona mwingiliano wa watu wengi ulikuwa ukihamia katika mji wa Manundu, hivyo kufuata mazingira.
Baaada ya kufika Manundu, wapo waliokuwa wakitoka Old Korogwe kwenda kupata chakula Manundu, hivyo kuona kuwa biashara anayofanya ni muhimu na anapaswa kuwa makini kwenye utendaji wake wa kazi.
Licha ya kufanya biashara hiyo kwa muda mrefu na kuelewa mazingira yote ya biashara, lakini mjasiriamali huyo anasema kwamba hafahamu lolote juu ya mambo ya kukopa, akiogopa kufilisiwa mali zake kutoka kwa wakopeshaji hao.
Anasema woga huo ameupata kwa kuwa na udhoefu wa watu wengine kusumbuliwa na kulazimika kukimbia maeneo yao kwasababu ya kukwepa madeni yao, hivyo jambo hilo linamfanya aone hana sababu ya kujenga tabia ya kukopa bila mpango.
“Huwa naogopa sana kukopa kwakujua naweza kuiacha familia yangu kwenye tabu, huku mama yao nikikimbia kwasababu ya kukwepa madeni, ukizingatia kwamba najua kuwa aina hiyo ya maisha ni ngumu na lazima nikubali hali yangu.
 “Sitaki kukopa bila sababu za msingi, maana mpaka sasa naweza kufanya biashara mwenyewe bila tatizo lolote, hivyo ili nikope napaswa kufanya biashara kubwa zaidi na lakini sio nifanye ili mradi kuna hela zipo zinahitaji wakopaji,” alisema Mama Kipande.
Aidha Mama Kipande anasema kwamba kingine kinachomfanya ashindwe kukopa ni kutokana na masharti magumu yanayowekwa kwa ajili ya kuwakopesha watu, hasa ardhi, nyumba na vitu vingine vya thamani.
Suala hili linasababisha akina mama wengi washindwe kuitumia vyema fursa ya mikopo maana hawana vitu vya thamani, jambo linalowafanya walowee kwenye dimbwi la ufukara, ingawa njia za kuwakomboa zipo.
Anasema serikali kwa kushirikiana na taasisi na benki za biashara zinatakiwa kuweka sera nzuri ya kuwakopesha watu kwa vikundi bila kuwapa masharti magumu ili kuwainua akina mama ambao mara nyingi ndio walinzi wa familia.
“Akina mama wakiendelea familia kwa pamoja imeendelea, maana mama hawezi kumuacha mtoto wake anatembea bila nguo wakati ana senti yake ndani, lakini baba hilo anaweza kuliona na akalifumbia macho.
“Katika hili ipo haja sasa ya kuangalia upya mwendo wetu kwa ajili ya kujenga uchumi imara kwa watu wote, wakiwamo akina mama,” alisema.
Mama Kipande pia anaitaka serikali kuangalia kwa kina upandaji wa gharama za maisha kwa kuhakikisha kuwa bei za vyakula hazipandi bila sababu ya msingi ili wao wasiwakandamize zaidi wateja wao.
Kuhusu usafi na mgambo wa jiji; mama Kipande anasema kwamba katika mgahawa wake suala la usafi ni jambo la muhimu, hasa kwa kuhakikisha kuwa wateja wake wananawa kwa sabuni na maji ya moto kabla na baada ya kula.
Hali hii inawafanya watu wengi kuingia katika mgahawa wake kwa kuona kuwa wanazingatia chakula kizuri na usafi katika eneo lote.
Kuhusu mgambo wa jiji, mama Kipande anasema usumbufu upo endapo biashara inafanywa bila kufuata sheria au wale wasioangalia suala zima la usafi wa mazingira na kwenye maeneo yao ya kazi.
Kwa sababu hiyo, kuna kila sababu ya serikali kutoa elimu zaidi kwa wajasiriliamali ili kuwafanya wamudu na kuitaka fursa ya ukopaji ili wapanuwe biashara zao kwa kupitia wataalamu wa fedha na biashara katika kila wilaya.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...