SERIKALI imesema ili kukabiliana na tatizo la kuwa na walimu waliofeli
mitihani ya sekondari kuanzia mwaka huu itaanza kuwasomesha bure
wanafunzi waliofaulu, wanaotaka kwenda kusomea shahada ya elimu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Ulimwengu ya Ufuatiliaji wa
Elimu kwa wote iliyoandaliwa na Shirila la Umoja wa Mataifa la Elimu na
Sayansi (Unesco), Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa alisema kuanzia sasa wanafunzi waliopata daraja la nne hawataruhusiwa kusomea ualimu.
Alisema ili kuwa na walimu wenye uwezo mkubwa wa kitaaluma na
kuondokana na dhana kuwa wanaokwenda kusomea kozi hiyo wameshindwa
kupata nafasi sehemu nyingine, wanafunzi waliofaulu watapewa mkopo na
Serikali na hawataulipa.
“Ukipata daraja hilo ni kwamba hakuna
nafasi ya kujifunza ualimu,” alisema na kuongeza kuwa wanafunzi
watakaopata daraja la tatu watapewa mkopo, lakini wao watalazimika
kuulipia.
Pia ripoti hiyo iliyoangalia namna mafunzo ya elimu
yanavyotolewa imebainisha kuwa walimu wa Tanzania wanaongoza kwa utoro
kazini katika Ukanda wa Afrika Mashariki jambo lililochangia wanafunzi
kufanya vibaya kwenye matokeo yao ya mitihani.
Akiwasilisha ripoti
hiyo, Profesa Galabawa alisema kuna upungufu wa walimu wenye sifa za
kufundisha huku taasisi zinazosimamia elimu zikishindwa kukabiliana na
tatizo hilo.
Alisema iwapo Serikali inataka kuwa na walimu wenye
sifa zinazotakiwa, italazimika kuwa na Dola 335 milioni (Sh536 bilioni)
ambazo ni sawa na asilimia 23 ya fedha yote ya bajeti ya wizara ya elimu
mwaka 2011 na kwamba Serikali ibadili utaratibu uliopo sasa wa kutoa
elimu.
No comments:
Post a Comment