HOTUBA:- HOTUBA
YA MHE. DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
KATIKA UFUNGUZI WA KITUO CHA TIBA, UCHUNGUZI NA MAFUNZO YA MAGONJWA NA SARATANI
ZA MATUMBO NA INI CHA HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI,
TAREHE
30 MEI, 2014
Mhe.
Dkt. Kebwe Steven Kebwe
Naibu
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii;
Dkt.
Gabriel Upunda
Makamu
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Hospitali ya Taifa Muhimbili;
Dkt. Rufaro Chatara
Mwakilishi Mkazi wa
Shirika la Afya Duniani (WHO)
Prof. H.C.
Konrad Meßmer (MESSMER);
Mwakilishi wa Else Kroner – Fresenius Stiftung
ya Ujerumani;
Prof. Meinhard
Classen;
Mwenyekiti, Munich Society of
Gastroenterology;
Waheshimiwa
Mabalozi;
Dkt. Marina
Njelekela
Mkurugenzi Mtendaji
wa Hospitali ya Taifa Muhimbili;
Prof. Ephata Kaaya
Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu cha Afya na Sayansi za Tiba
Muhimbili;
Prof. Msemo Diwani
Mwakilishi wa Mkurugenzi
Mtendaji, Taasisi ya Saratani
Ocean Road;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Napenda kuchukua nafasi hii kutoa shukrani
zangu za dhati kwa uongozi mzima wa Wizara ya afya kwa kunialika kushirikiana
nanyi katika tukio hili. Kwa namna ya pekee nikupongezeni kwa maandalizi mazuri
na kwa kuwa na wazo la kuanzisha kituo hiki ambacho kinaongeza nguvu katika
utoaji huduma za afya hapa Tanzania.
Kituo hiki ni cha kwanza katika nchi za Afrika Mashariki na kitatoa huduma za
tiba, uchunguzi na mafunzo kwa kutumia Hadubini. Ni wazi kuwa kituo
hiki kitasaidia wananchi wetu kupata huduma hapa nchini na kitawapunguzia
gharama zilizotokana na wao kwenda nje kutafuta tiba ya magonjwa haya.
Mabibi
na Mabwana;
Ninafahamu
kuwa
ujenzi wa Kituo hiki umewezekana kutokana na ushirikiano baina ya
Serikali ya Tanzania na Chama cha Magonjwa ya Tumbo cha Munich. Serikali
ya Tanzania imechangia shilingi Milioni Mia Nane na
Chama cha Magonjwa ya Tumbo cha Munich
kupitia msaada kutoka ELSE KRONER FRESENIUS STIFTUNG ya Ujerumani,
imechangia
zaidi ya shilingi za kitanzania Bilioni Moja kwa ajili ya ununuzi wa
vifaa. Huu
ni uwekezaji mkubwa sana
na naomba kutumia nafasi hii kukuombeni wenzetu wa Hospitali ya
Muhimbili
kuhakikisha kuwa mnakitumia kituo hiki ipasavyo huku pia mkivitunza
vifaa
vilivyopo.
Mabibi
na Mabwana;
Magonjwa ya mfumo wa
chakula na ini ni miongoni mwa matatizo makubwa ya kiafya yanayoikabili dunia
nzima kwa sasa. Kumbukumbu za magonjwa ya Saratani duniani zilizotolewa mwaka
2008 zinaonyesha kuwa, jumla ya wagonjwa wapya takribani milioni tatu na laki
tano, waliugua saratani za mfumo wa chakula na ini. Kati ya hao asilimia 65% walitoka katika nchi
maskini, ikiwemo Tanzania.
Saratani ya koo la
chakula na ini, ndizo zinazoongoza katika nchi maskini ukilinganisha na nchi
zilizoendelea, zikifuatiwa na saratani ya tumbo. Hapa kwetu Tanzania, wastani
wa watu 30 hadi 35 kwa kila wananchi 100,000 hufariki dunia kila mwaka kwa
saratani ya koo la chakula.
Sababu kubwa za
maradhi haya ni za mtindo wa maisha kama
unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara. Pia, magonjwa ya kuambukiza kama homa ya ini na bakteria aina ya Helikobakta, ni
sababu mojawapo ya mtu kupata saratani za mfumo wa chakula na ini.
Mabibi
na Mabwana;
Ninaelewa kuwa
hatuna wataalamu wa kutosha katika huduma hii ya afya wakiwemo madaktari,
wauguzi na wataalamu wengine ili kufanikisha kuendesha kituo hiki vizuri.
Mmenitaarifu kuwa kuna Mabingwa wa Hadubini wanane (8) hapa Hospitali ya Taifa
Muhimbili kwa sasa, pamoja na wauguzi watano tu ambao ni wachache sana.
Katika kusaidia
kukabiliana na upungufu huu, serikali yetu itasaidia katika kufanikisha mafunzo
kwa wataalamu zaidi ndani na nje ya nchi katika maeneo haya ili walau tuwe na
idadi inayohitajika.
Nitumie nafasi hii
pia kuwaomba wenzetu wa Taasisi za Hospitali ya Taifa Muhimbili, Chuo Kikuu cha
Afya na Sayanzi za Tiba Muhimbili na Taasisi ya Saratani Ocean Road, kupanua huduma zenu
na kutoa huduma za kitaalamu zaidi kama vile
upandikizaji wa figo na nyinginezo. Pale mnapohitaji msaada kutoka serikalini,
msisite kufanya hivyo kwani suala la afya linagusa maisha ya kila mwananchi
wetu.
Mabibi
na Mabwana;
Pamoja na mikakati
ya kutoa huduma za tiba, nakisihi kituo hiki pamoja na taasisi wadau kufikiria namna
ya kuanzisha kinga ambayo inajumuisha chanjo kwa magonjwa kama
hepatitis B na C ambayo yanachangia kwa kiasi kikubwa magonjwa ya tumbo na ini (hepatology)
ikiwemo saratani ya ini. Ninaelewa kuwa katika mpango wa chanjo (Expanded
Program of Immunisation) chanjo ya Hepatitis B inatolewa kwa watoto.
Hata hivyo, jitihada
zinatakiwa kuendelea ili kujumuisha watu wazima ambao hawajapata chanjo hiyo. Zaidi
ya hayo, tafiti zinazohusu maeneo ya Afrika ni muhimu sana kwani zitatuonesha mwelekeo na
kutusaidia katika kubuni jitihada mbalimbali za kukabiliana na matatizo ya
kiafya yanayokabili nchi zetu.
Ndugu
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili;
Katika hotuba yako
umetaja upungufu mkubwa wa wafanyakazi kama
moja ya changamoto. Ni kweli changamoto hii ipo katika kila sekta, ikiwemo
sekta ya afya. Hata hivyo, serikali yetu inafanya kazi kwa bidii kukabiliana
nayo ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaosomea shahada ya
uzamili katika tiba na uuguzi.
Mabibi
na Mabwana;
Sekta ya afya ni
moja ya sekta zinazoathiriwa sana na tatizo la
wataalamu kuondoka kwa ajili ya kupata maslahi bora zaidi nje ya nchi. Naelewa
kuwa kwa maendeleo ya utandawazi tuliyonayo, mtu yeyote angependa kupata maslahi
bora zaidi. Serikali yetu imekuwa ikijitahidi na inaendelea kujitahidi
kuhakikisha kuwa wataalamu wetu wanapata maslahi bora kadiri ambavyo tunamudu.
Bajeti ni ndogo,
lakini naelewa kuwa Hospitali ya Taifa ina huduma ya wagonjwa binafsi yaani
“Intramural Private Practice (IPPM)” ambayo si kwa wagonjwa binafsi tu bali pia
mifuko mbalimbali ya bima ya afya kama vile Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Afya ya Jamii. Hivyo
mnaweza kabisa kutumia mapato yanayopatikana kutokana na huduma hii katika
kuboresha vipato vya wataalamu wenu. Ninaamini kuwa kama
ikitumika vizuri, maslahi bora yanayosemwa hayatakuwa popote zaidi ya hapa hapa
Hospitali ya Taifa Muhimbili
Mwenyekiti wa Bodi
ya Wadhamini Muhimbili, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi za Tiba Muhimbili
na Wakurugenzi Watendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Saratani
ya Ocean Road,
Kuhusiana na kudumu
kwa kituo hiki, ninafahamu kuwa marafiki zetu wa Gastroenterology Foundation of
Munich na Else
Kroner Fresenius Stiftung hawataendelea kutusaidia milele. Ni wakati muafaka
sasa kwa kituo kupitia Hospitali ya Taifa Muhimbili kuwa na bajeti yake
inayojitegemea kila mwaka ambayo itajumuishwa katika bajeti yote ya mwaka bila
kutegemea bajeti ya jumla ya Hospitali.
Zaidi ya hayo,
kupitia huduma ya IPPM, kituo kifanye kazi kama
kitengo kinachotengeneza mapato yaani kwa lugha ya kigeni “business unit” ili
kutengeneza mapato yake. Mapato hayo
yatumike kununua mahitaji ya kitengo kama vile
vifaa tiba kuepuka kushindwa kutoa huduma kutokana na ukosefu wa vifaa. Hii itakihakikishia
kitengo kufanya kazi vizuri muda wote na huduma zake zitakuwa endelevu.
Mabibi
na Mabwana;
Nitakuwa sijatenda
haki kama sitatoa shukrani za dhati kwa “Gastroenterology
Foundation of Munich” na “Else Kronner Fresenius Stiftung” chini ya usimamizi
wa Prof. Meinhard Classen kwa jitihada zake katika kuanzishwa kwa kituo hiki na
kuifanya siku ya leo kuwa ya kukumbukwa. Ni ukweli usiopingika kuwa, ufadhili wa
fedha uliofanywa na Else Kronner- Fresenius Stiftung ambaye Mwakilishi wake Prof.
Dr. H.C. Konrad Meßmer (MESSMER) ambaye
yupo hapa pamoja na kazi ya usimamizi wa mradi huu uliofanywa na Prof. Classen binafsi
kupitia Gastroenterology Foundation of Munich, haukuwa rahisi wala nafuu.
Hawa ni watu wenye
upendo wa dhati na wenye kujali wagonjwa na zaidi wenye mapenzi na Afrika ndio
wanaweza kufanya kazi kubwa kama hii. Hivyo kwa
niaba ya Serikali ya Tanzania
nasema asante sana kwako Prof. Classen
pamoja na rafiki zako wa Ujerumani ambao wachache wako hapa na wale wote
waliochangia katika kufanikisha kituo hiki.
Mabibi
na Mabwana;
Ningependa kuchukua
nafasi hii kuishukuru Serikali ya Ujerumani kwa misaada mbalimbali iliyokwishatoa
kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa watanzania. Mmekuwa
pamoja nasi mara zote siyo tu katika sekta ya afya bali pia katika sekta
nyingine, ikiwemo uongozi bora. Kama
watanzania, tunathamini ushirikiano huu na tunaamini kuwa utadumu kadiri nchi zetu
mbili zitakavyodumu.
Nashukuru tena kwa
kunikaribisha hapa na sasa natamka kwamba Kituo hiki cha TIBA, UCHUNGUZI NA MAFUNZO YA MAGONJWA NA SARATANI ZA MATUMBO NA INI
CHA HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI kimezinduliwa rasmi.
Asanteni kwa
kunisikiliza
No comments:
Post a Comment