WANAMUZIKI NA WADAU WA MUZIKI KUKUTANA
VIJANA SOCIAL HALL KINONDONI ALHAMISI ASUBUHI KUJADILI MAZISHI YA AMINA NGALUMA
WANAMUZIKI na wadau wa
muziki watakutana Alhamisi hii saa 5 asubuhi kujadili namna ya kusaidia na
kushiriki mazishi ya mwimbaji Amina Ngaluma.
Marehemu Amina Ngaluma, pichani, enzi za uhai wake.
Hilo litafanyika ndani
ya ukumbi wa Vijana Social Hall (jirani na Mango Garden), Kinondoni jijini Dar
es ambapo itaangaliwa namna nzuri ya kushirikiana na familia ya marehemu
kuanzia hatua ya kuupokea mwili hadi mazishi.
Mwili wa Amina Ngaluma
aliyefariki nchini Thailand Alhamisi iliyopita, utawasili jijini Dar es Salaam
Ijumaa hii saa 3.30 usiku kwa ndege ya
KLM. Mazishi yatafanyika siku inayofuata (Jumamosi) mchana.
Mmoja wa waratibu wa
kikao hicho cha Alhamisi kinachoshirikisha pia Shirikisho la Muziki Tanzania,
Mwinjuma Muumin, amesema msiba huu umechukua muda mrefu, familia imeingia
gharama kubwa katika kipindi chote hiki na hivyo ni wakati muafaka sasa kwa wanamuziki
na wadau wa muziki kukutana na kuangalia
namna ya kuipunguzia mzigo familia ya marehemu.
Muumin amesema kuna
mambo mengi ya msingi ya kujadiliana katika kikao hicho na kwamba taarifa zote
muhimu za mazishi ya Amina Ngaluma zitatolewa hapo.
Mwanamuziki Rashid
Sumuni ambaye ni mume wa marehemu
anatarajiwa kuhudhuria kikako hicho.
Naye Rais wa Shirikisho
la Muziki Tanzania, Addo November amesema kikao hicho ni muhimu na kitafungua
njia ya umoja na mshikamano miongoni mwa wasanii hususan wanamuziki wa dansi.
No comments:
Post a Comment