https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Thursday, May 22, 2014

Makamu wa Rais akutana na Watanzania wanaoishi nchini Japan

Na Mwandishi Maalum – Tokyo, Japan
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal pichani aliyesimama, amewatoa wasiwasi Watanzania wanaoishi nchini Japan kuhusu mvutano  uliojitokeza ndani ya Bunge la Katiba na kuwahakikishia kuwa ana imani Bunge hilo litakapokutana  Agosti mwaka huu mambo yatakwenda vizuri .

Dkt. Bilal amewatoa hofu Watanzania hao kufuatia risala yao iliyosomwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo (Tanzanite Society)  David Semiono kueleza masikitiko yao kuhusu kutoridhishwa na mwenendo wa Bunge la Katiba.

Akizungumza na Watanzania hao katika ukumbi wa New Otani Hotel hapa Tokyo, Japan jana Mei 21, 2014 Dkt. Bilal alisema kilichojitokeza katika bunge hilo ni kurekebishana ili nchi iweze kupata Katiba mpya yenye maslahi kwa wananchi na itakayodumu kwa miaka mingi ijayo.

Makamu wa Rais alibainisha kuwa kazi ya kuandika katiba si rahisi kama wengi wanavyofikiria kwani katika nchi zingine, wanafikia uamuzi  huo baada ya kutokea hali ya kutoelewana na hata kupigana jambo ambalo ni tofauti na Tanzania ambapo uamuzi huo umefikiwa  kiungwana kwa kuheshimu mawazo na maoni ya wananchi wake.
 “Sisi kwa salama na amani tumeanza mchakato wa katiba mpya na tumalize kwa salama na amani, tuendelee na sifa tuliyonayo ya umoja na mshikamano,” aliasa Dkt. Bilal

Aliutaka Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kuacha jazba na kurudi bungeni ifikapo Agosti mwaka huu ili waweze kushirikiana na wenzao katika kukamilisha kazi hiyo muhimu waliotumwa na wananchi.

“Tunachoomba waliotoka nje ya mstari, tusiwe wa kwanza kukaidi na kufuata misingi ya jazba. Tutangulize kwanza  Utanzania wetu. Tunawaomba wote waliotoka bungeni, warudi washirikiane na wenzao. Tukimaliza kwa amani mchakato huu, tutakuwa tumeijengea sifa kubwa nchi yetu. Tumeheshimu matakwa ya watu, sote tuheshimu mchakato huu mpaka tuufikishe mwisho kwa amani,” alisema Makamu wa Rais.

Akizungumzia Muungano, Makamu wa Rais aliwataka Watanzania hao kuendelea kuuenzi, kuulinda na kuudumisha kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla, huku akiwakumbusha kuwa muungano huu umekuwa wakupigiwa mfano Afrika na duniani kwa ujumla.

 “Muungano wetu ni wakujivunia na wa aina yake barani Afrika na kote duniani. Kumbukeni miaka ile nchi nyingi za Afrika zilijaribu kuungana lakini zilishindwa. Safari ya miungano yao, ilikuwa fupi na miungano hiyo imesambaratika,” alisema Dkt. Bilal huku akitolea mfano wa muungano wa senego-Gambia na baadhi ya nchi nyingine za Kiafrika.

Akijibu malalamiko ya Watanzania hao waliodai kuwa  Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) haiwatendei haki wafanyabiashara wanaoingiza magari nchini kwa kutoza kodi  zenye utata bila hata kuzingatia taratibu zilizowekwa, Dkt. Bilal  alisema amelipokea tatizo hilo, na kufafanua kwamba Serikali inaendelea kuzifanyia kazi kero mbalimbali ndani ya mamlaka hiyo. 

Aliwataka Watanzania hao kuwa na subra kwani alisema kila jambo huanza kwa hatua moja na halimaliziki kwa siku moja na kuwahakikishia kwamba anaamini kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali kero hizo zitapatiwa ufumbuzi haraka.Kuhusu ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya, Dkt. Bilal aliiasa jamii na viongozi wa dini mbalimbali nchini kushirikiana na serikali kwa kuwapa miongozo ya maadili mema vijana ili kuepukana na janga hilo na hivyo Taifa liweze kupiga hatua ya maendeleo.

“Tusifanye mzaha katika malezi ya watoto wetu, viongozi wa dini zote nchini wana wajibu wa kuwafundisha vijana wetu maadili mema  na sisi wazazi tusichoke kuwakanya vijana wetu kwa ukali kuhusu matumizi ya dawa za kulevya”, alisema Dkt. Bilal. Makamu wa Rais alitumia fursa hiyo pia kuhimiza Watanzania kutumia nafasi yao ughaibuni kushawishi wawekezaji kuja kuwekeza nyumbani kwani Tanzania haiwezi kuendelea bila kuwa na uwekezaji wa kutosha.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...