Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
JUHUDI za kukuza kiwango cha elimu kinachagizwa na vitu mbalimbali, bila
kusahau taasisi zilizoundwa kwa ajili ya kufanya kazi kwa ushirikiano kwa
maendeleo ya Taifa.
Juhudi hizo zinakwenda sanjari na será zenye tija, ukizingatia kuwa ndio
mfumo bora kwa sekta hiyo nyeti. Hapa Tanzania, miongoni mwa será na mikakati kabambe ni pamoja na ile ya uchangiaji
wa elimu ya juu. Sera hiyo imekuwa ikitekelezwa nchini kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya
juu tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Katika mazungumzo
yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa
HESLB, Cosmas Mwaisobwa (pichani), anasema kuwa será
hiyo imezidi kushika kasi, ingawa ilikuwapo tangu wakati wa ukoloni na baada ya
uhuru hasa baada ya kuanzishwa kwa Azimio la Musoma mwaka 1974.
Anasema kuwa katika
mfumo mpya ulioanza miaka ya 1990, mwanafunzi alitakiwa kuchangia sehemu
ya gharama za elimu tofauti na ilivyokuwa mwanzo ambapo alikuwa akipata bure
elimu ya juu. Kabla ya kuanza kwa mfumo wa uchangiaji, serikali ilikuwa ikitoa kila kitu
kwa wanafunzi waliopata fursa ya kujiunga na elimu ya juu.
“Hata hivyo, kuanzishwa
kwa mfumo huo, kulitokana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii, hivyo kuwezesha
kuanzishwa kwa mfumo wa wananchi kuchangia gharama mbalimbali badala ya
serikali kugharimia kila kitu katika elimu, afya na huduma nyingine.
“Awamu ya kwanza ya kuanzishwa kwa mfumo
huo mwaka 1992, wanafunzi walianza kugharamia nauli za kwenda na kurudi kutoka
chuoni, ada za maombi ya kujiunga na vyuo, ada za
kuandikishwa chuoni na fedha za tahadhari,” alisema.
Aidha, wanafunzi walilipia ada za serikali za wanafunzi vyuoni. Awamu ya pili ya
uchangiaji katika elimu ya juu ilitekelezwa kuanzia Julai, 1994. Pamoja
na gharama zilizohamishiwa kwa wanafunzi na wazazi katika awamu ya kwanza,
wanafunzi waligharamia mahitaji ya chakula na malazi.
Hata hivyo, gharama
hizo zilionekana kuwa kubwa na serikali kuanzisha utaratibu wa utoaji mikopo
kwa wanafunzi kwa ajili ya gharama za chakula na malazi, huku utaratibu huo
ukianzishwa rasmi awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin William Mkapa, mwaka
2005. Ndio hapo ilipoanzishwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB), ambayo ilianza shughuli zake rasmi shughuli zake Julai, 2005.
Katika awamu hiyo ya utekelezaji wa sera ya uchangiaji, wanafunzi
wanatakiwa kuchangia katika maeneo yote yaliyobaki ya gharama za elimu ya juu,
yakiwemo ada za mafunzo, utafiti, mahitaji maalumu ya vitivo na mafunzo kwa
vitendo.
Sheria iliyounda bodi ya mikopo, ilianisha majukumu ya bodi ambayo ni
kusimamia uendeshaji wa mfuko wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu na kuweka
utaratibu wa kuwatambua wahitaji wa mikopo; kupokea, kuchambua maombi yote na
kutoa mikopo kwa waombaji wahitaji, na Kuweka kumbukumbu za wanafunzi
wanaokopeshwa.
Majukumu mengine ni kukusanya marejesho ya mikopo yote iliyotolewa tangu
mwaka 1994; kuweka mtandao wa ushirikiano baina ya bodi, taasisi za elimu
ya juu, waajiri na wakopaji; na kuishauri serikali kuhusu masuala ya utoaji na
urejeshwaji wa mikopo. Mkurugenzi huyo Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Mwaisobwa
anasema tangu mwaka 2005, HESLB imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika
utekelezaji wa majukumu yake.
Anasema katika miaka minane na nusu tangu kuanzishwa kwake, bodi
imeimarisha utendaji kazi na kuweka mifumo na vitendea kazi ili kusimamia
ongezeko kubwa la mikopo. “Hivi sasa bodi inatoa mikopo kwa kutumia mifumo ya kielectroniki
(mtandao) katika uchambuzi wa mikopo, utoaji mikopo na urejeshwaji wa mikopo. “Vile vile waombaji wa mikopo yanatuma maombi yao kwa njia ya mtandao,
tukiamini ni njia nzuri inayoweza kurahisisha utaratibu huo wa kutafuta nafasi
ya kupatiwa mahitaji yao,” alisema.
Mwaisobwa anasema
kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi tangu mwaka 1994/1995 ambapo
wakati huo kulikuwa na wanafunzi 6,061 waliojiunga na vyuo mbalimbali vya za
elimu ya juu. Anasema kwa sasa wamefikia wanafunzi 233,000, huku wanafunzi
98,371 wakipata mikopo. Mkurugenzi huyo pia alisema mikopo
itolewayo na Bodi imekuwa sababu ya ongezeko la vyuo vya elimu ya juu
kutoka 25 vilivyokuwepo mwaka 2004/2005 hadi vyuo 63 mwaka wa sasa wa masomo wa
2013/2014.
“Tangu wakati huo hadi Sedemba, mwaka jana, alisema mikopo yenye thamani
ya sh. 1,843,483,926,686.58. Alisema katika mikopo hiyo, sh. 51,103,685,914
zilitolewa na iliyokuwa Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia na sh.
1,792,380,240,772.58 zimetolewa na bodi yenyewe kuanzia Julai, 2005 na
wanafunzi walionufaika ni 260,150.
“Pamoja na uchangiaji huo, dhana hii nigeni katika historia ya
Tanzania kwa kuwa mfumo huo ulikuwepo hata kabla ya uhuru. Mwaka 1956, serikali ya kikoloni ilianzisha mfuko uliojulikana kama
Tanganyika Education Trust Fund, ambao ulitoa mikopo kwa wanafunzi kutoka
familia masikini. Utaratibu huu uliendelea hata baada ya uhuru hadi mwaka 1964
lilipoanzishwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT),” Alisema.
Anasema kuwa mwaka
1964 hadi 1974, wanafunzi walitumikia katika Jeshi la Kujenga Taifa kwa miezi
sita na baada ya hapo walihakikishiwa kupata kazi serikalini. Kwa kipindi cha miezi 18 walilipwa asilimia 40 ya mishahara yao na asilimia
60 iliyobaki ililipwa serikali, kama uchangiaji katika elimu ya juu kwa
mwanafunzi husika.
Kupitishwa kwa
Azimio la Musoma mwaka 1974, kulileta mabadiliko katika taratibu za ugharamiaji
wa elimu wa juu. Muda wa kutumikia Jeshi la Kujenga Taifa uliongezwa kutoka
miezi sita hadi mwaka mmoja. Wanafunzi waliokuwa
wakijiandaa kujiunga na elimu ya juu walitakiwa kufanya kazi angalau kwa miaka
miwili kabla ya kuanza masomo yao.
Anasema kutokana na
utaratibu huo, wanafunzi walitia saini mikataba ya miaka mitano na serikali ili
kufanya kazi serikalini baada ya kumaliza masomo kabla ya kuruhusiwa kufanya
kazi sehemu zingine. Hiyo ilikuwa njia nyingine ya urejeshaji wa gharama za
elimu ya juu. Kwa ujumla, mfumo
wa uchangiaji elimu na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu,
umesaidia vijana wengi wa Kitanzania kupata fursa ya elimu katika vyuo vya
elimu ya juu nchini.
Pamoja na mafanikio
hayo, changamoto kubwa iliyopo ni namna ya kurejesha mikopo hiyo kwa kuwa baada
ya kuhitimu, wengi wamekuwa wakishindwa kuheshimu makubaliano au kuwa wagumu
katika ulipaji.+255712053949
kambimbwana@yahoo.com
No comments:
Post a Comment