Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UONGOZI wa klabu ya Yanga, umesema kwamba hawana presha na
mechi yao ya Aprili 19 dhidi ya Simba SC, badala yake wanaelekeza nguvu kwa
mechi nyingi kabla ya kuvaana na mtani wao wa jadi katika Uwanja wa Taifa,
jijini Dar es Salaam.
Yanga kwa sasa imeweka kambi yao mjini Bagamoyo, ambapo
Jumapili wataingia uwanjani kumenyana na timu ya JKT Ruvu ya mkoani Pwani, huku
wakiwa na mipango kabambe ya kuhakikisha kuwa wanaibuka na ushindi mnono.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Afisa Habari wa Yanga,
Baraka Kizuguto, alisema kuwa ingawa watu wamekuwa wakiangalia zaidi mechi ya
Simba, lakini timu yao inakabiriwa na michezo migumu mno, hivyo hawaoni sababu
ya kuwekeza katika mechi moja ya watani.
Alisema mipango yao ni kunyakua ubingwa wa Bara na sio
kumfunga mtani wa jadi, huku wakishindwa kutetea taji lao ambalo kwa sasa
linaelekea kuchukuliwa na timu ya Azam baada ya kufikisha pointi 53, huku Yanga
wao wakishika nafasi ya pili wakiwa na pointi 46.
“Hatuwezi kuwekeza zaidi mechi ya Simba wakati tuna mechi
nyingine ngumu, ikiwamo ya JKT Ruvu, hivyo tunakwenda hatua kwa hatua kwa ajili
ya kuiweka timu yetu katika mazingira mazuri ya kutetea taji letu la Ligi ya
Tanzania Bara.
“Tusipokuwa makini tunaweza kuifunga Simba lakini tukapoteza
mechi nyingine, hivyo kusababisha kuuweka rehani ubingwa wetu wakati ndio
mipango tunayoiweka kuhakikisha kuwa kila kitu kinakwenda vizuri kwa kufanya
maandalizi ya kila mechi na si ile ya watani wa jadi tu,” alisema.
Ligi ya Tanzania Bara imezidi kukolea joto huku timu ya
Yanga na Azam zikionekana kukabana koo kuwania taji hilo, ambapo kwa mtani wake
wa jadi Simba, msimu huu ameonekana hana chake baada ya kupata matokeo mabaya
kwenye mechi zake.
No comments:
Post a Comment