Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MSEMAJI wa klabu ya Coastal Union
yenye maskani yake jijini Tanga Tanzania, Hafidh Kido, ameachia ngazi kutokana
na migogoro mizito inayoendelea kuitafuna timu hiyo iliyomaliza ligi katika
nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi.
Msemaji wa zamani wa Coastal Union, Hafidh Kido pichani.
Akizungumza leo asubuhi jijini Dar
es Salaam, Kido alisema kuwa amelazimika kujiuzuru ili kulinda hadhi yake
katika sekta ya habari kutokana na mikanganyiko ndani ya timu hiyo.
Msemaji wa zamani wa Coastal Union, Hafidh Kido, akiwa katika majukumu yake.
Alisema awali uongozi wa klabu hiyo
haukumpa ushirikiano katika majukumu yake, hali iliyolazimika kusaidiwa kwa
kiasi kikubwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo na Mfadhili wao, Nassor
Bin Slum.
“Mimi Hafidh Athumani Kido, nikiwa
na akili timamu natangaza kutojihusisha na shughuli zote za Coastal Union, hasa
usemaji wa klabu, huku miongoni mwa sababu nyingi zilizonifanya kutangaza
uamuzi huo ni sintofahamu iliyozuka ndani ya klabu yetu.
“Kwa taaluma yangu ya uandishi wa habari lazima niwe na
msimamo juu ya mambo yanayoendelea kwenye jamii ili niendelee kufanya kazi na
klabu hii kwa wakati huu wa misuguano, lazima niwe na upande; kwa maana upande
unaounga mkono uongozi ama upande usiokuwa na Imani na uongozi,” alisema Kido.
Kwa mujibu wa Kido, yeye ameamua
kutounga mkono upande wowote, akiamini atakuwa katika mstari sahihi na kukaa
pembeni ili afanye shughuli zake za uanahabari kwa furaha na amani, huku
akisema kuwa ataendelea kuwa mwanachama halali wa Coastal Union Sports Club
mwenye kadi 0013.
No comments:
Post a Comment