Na Pendo Fundisha,
Mbeya.
SERIKALI Mkoani Mbeya
imepiga marufuku itikadi za kisiasa katika uendeshaji wa timu ya soka ya Mbeya
City inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ili kulinda uhai wa timu hiyo.
Uamuzi huo
umefikiwa kufuatia baadhi ya wanasiasa kuanza tabia ya kujinadi kuwa
mafanikio ya timu ya Mbeya City inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya
yametokana na juhudi zao na vyama vyao vya siasa.
Katibu Tawala wa
mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja, aliyasema hayo kwenye hafla ya kuwapongeza
wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa timu ya Mbeya City iliyoambatana na
kuivunja rasmi kambi ya timu hiyo baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu ya Soka
Tanzania Bara huku timu hiyo ikifanikiwa kushika nafasi ya tatu.
Mtunguja, alisema tayari
baadhi ya wanasiasa mkoani hapa wameanza kuyahusisha mafanikio ya timu hiyo na
harakati zao za kisiasa za vyama vyao hali ambayo ni hatari kwa uhai wa Mbeya
City katika ulimwengu wa soka nchini.
Alisema, tabia hiyo
inaweza kuwagawa mashabiki wa timu hiyo kutokana na kwamba kila mmoja ana
mapenzi na chama chake cha siasa hivyo kuingiza itikadi kwenye uendeshaji
kutasababisha ubaguzi baina yao.
“Wanasiasa watuache,
wasituvuruge baada ya kuona mafanikio yaliyopatikana sasa wanataka kujiingiza
katika timu, watatuulia timu yetu.” alisema Mtunguja.
Kufuatia mafanikio ya
timu hiyo, Meya wa Jiji la Mbeya, Athanas Kapunga, alisema Halmashauri ya jiji
hilo imeamua kuboresha mishahara ya wachezaji ili kuzuia uwezekano wa
kurubuniwa na timu kubwa kwa kigezo cha maslahi.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa Mbeya City, Musa Mapunda, alisema baada ya kufanikiwa kushika
nafasi ya tatu msimu huu, sasa wanaweka mikakati ya kuhakikisha timu hiyo
inachukua ubingwa wa ligi Kuu ya Soka Tanzania bara msimu ujao.
Naye kocha Mkuu wa timu
hiyo, Juma Mwambusi, alisema katika usajili wao kwa ajili ya msimu ujao wa ligi
hiyo hawatachukua wachezaji wenye majina kutoka timu zinazoshiriki ligi hiyo
bali bali ataangalia zaidi wachezaji chipukizi wasio na majina kutoka ndani ya
mkoa wa Mbeya.
Mbeya City ilianzishwa
Julai mwaka 2011 na huu ni msimu wake wa kwanza kushiriki ligi hiyo na kupata
mafanikio yak upigiwa mfano.
No comments:
Post a Comment