Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI ya Jamhuri ya Watu wa China, imeridhia na kukubali
kugharamia ujenzi wa Kiwanja cha michezo kilichopewa jina na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar la Mau Tse Tung, kilichopo miperani Kikwajuni Mjini
Zanzibar.
Kauli hiyo imetolewa na Balozi Mdogo wa Jamuhuri ya Watu wa
China aliyepo Zanzibar Bw. Xie Yunliang wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika Ofisi yake iliyomo ndani ya
Jengo la Msekwa Bungeni Mjini Dodoma.
Balozi Xie Junliang alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar kwamba Timu ya wataalamu wa China inatarajiwa kukifanyia utafiti na
uchunguzi kiwanja hicho baadaye mwaka huu sambamba na utiwaji saini makubaliano
ya ujenzi wa kiwanja hicho unaotarajiwa kufanyika mapema mwaka ujao.
Alisema ujenzi wa uwanja huo uliopewa heshima ya jina la kiongozi muasisi wa Taifa la China marehemu Mao Tse Tung utajumuisha kiwanja
cha mchezo wa soka pamoja na michezo mengine ya ndani mfano mchezo wa Table
Tennis.
“Tunatarajia ujeni wa kiwanja cha Mao utakapokamilika
utakuwa na uwezo wa kuhudumia wanamichezo wa michezo tofauti ukiwemo ule
unaopendwa zaidi wa soka “. Alisema Bwana Xie Junliang.
Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar alimueleza Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba uhusiano wa kidugu uliopo kati ya Zanzibar na
Tanzania kwa ujumla pamoja na China unastahiki kuenziwa zaidi.
No comments:
Post a Comment