Wakati viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wakiweka
kambi Zanzibar, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta jana
naye alitumia siku nzima visiwani humo akikutana na baadhi ya viongozi
wa Serikali, katika kile kinachotafsiriwa kuwa kulinusuru Bunge hilo.
Habari
zilizolifikia gazeti hili kutoka Zanzibar zinasema Sitta alikutana na
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim
Seif Sharif Hamad, Rais Mstaafu, Aman Karume na mwanasiasa wa siku
nyingi wa CCM, Mzee Hassan Nassor Moyo.
Zanzibar
kwa sasa ndiyo moyo wa upatikanaji wa Katiba Mpya kutokana na wajumbe
wake katika Bunge kutegemewa ama kuipitisha au kuikwamisha kwa kuwa kila
upande kati ya mbili zinazovutana, hauna uhakika wa kupata theluthi
mbili za kura.
Baada ya
kuondoka bungeni na kutangaza kususia vikao vya Bunge hilo Aprili 16,
mwaka huu, siku mbili baadaye viongozi wa Ukawa waliingia Zanzibar
wakitaka kufanya mikutano ya hadhara kuwaeleza wananchi sababu za
kufanya hivyo, lakini wakazuiwa na polisi na hadi jana walikuwa
wanasubiri kibali.
Safari ya Sitta.
Katibu wa
Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad pamoja na kuthibitisha ziara ya Sitta
Zanzibar kuwa alikuwa akutane na Dk Shein, alisema hafahamu lolote
kuhusu mkutano wake na Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF.
“Sifahamu
malengo ya safari wala walichokwenda kuzungumza, ila ni kweli kwamba
alifika Zanzibar leo (jana) na alitarajiwa kuondoka jioni kurejea
Dodoma,” alisema Hamad na kuongeza:
“Hilo la
kuonana na Maalim Seif silifahamu ila ninachojua aliniambia nimfanyie
miadi ya kuonana na Dk Shein na nikaifanya kama alivyoelekeza.”
Mapema
habari zilizolifikia gazeti hili kutoka Zanzibar zilisema, Sitta baada
ya kukutana na Karume, Shein na Mzee Moyo alitarajiwa kukutana na Maalim
Seif saa 9:00 alasiri. Katibu wa Maalim
Seif, Issa Kheri Hussein alithibitisha kwamba Sitta alikutana na
kiongozi huyo nyumbani kwake, Mbweni saa 9:30 alasiri jana, lakini
alidai kutokuwa na taarifa za mazungumzo hayo.
“Hilo
naweza kulithibitisha kwamba mkutano huo umefanyika lakini mazungumzo
yenyewe yalikuwa ya faragha na mimi baada ya Sitta kufika niliondoka,
hivyo sikuweza kufahamu kilichozungumzwa kwa undani, pengine mpaka
nizungumze na Maalim mwenyewe,” alisema Hussein.
No comments:
Post a Comment