https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543

Recent Post

Saturday, April 05, 2014

Migogoro ya ardhi inavyoitafuna wilaya ya HandeniKatibu wa Baraza la Kata ya Kwamatuku, wilayani Handeni, mkoani Tanga, pichani.
Na Kambi Mbwana, Aliyekuwa Handeni
“KATIKA nchi kama yetu, ambayo Waafrika ni masikini na wageni ni matajiri, kuna uwezekano mkubwa kwamba Mwafrika akiruhusiwa kuiuza ardhi, katika miaka themanini au miaka ijayo, ardhi yote ya Tanganyika itamilikiwa na matajiri wageni, na wenyeji watakuwa watwana.

“Lakini hata kama wageni wasingekuwa matajiri, litaibuka tabaka la Watanganyika matajiri wajanja. Tukiruhusu ardhi iuzwe kama kanzu, katika muda mchache, kutakuwa na kundi dogo la Waafrika wakiwa na ardhi na walio wengi watakuwa watwana.” Haya ni maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambare Nyerere.


Mwalimu Nyerere ambaye kwa sasa ni marehemu, aliyasema haya mwaka 1958, kauli ambayo hadi sasa inaendelea kuishi. Mengi yanatokea katika migogoro ya ardhi. Wachache wanamiliki ardhi, huku wananchi wengi wakibaki kama watwana.

Mjumbe wa Baraza la Kata ya Kwamatuku, wilayani Handeni, mkoani Tanga, Mwanahamisi Nyata, pichani.
Nimelazimika kuanza na kauli ya Nyerere baada ya kuona jinsi Tanzania inavyogubikwa na migogoro ya ardhi. Kila kona zinasikika kauli tata au vilio vya wananchi wengi wakionyesha jinsi wanavyotafunwa na kadhia hiyo.Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, pichani.
Katika wilaya ambazo zinasikika kuwa na migogoro mingi ya ardhi, Handeni, mkoani Tanga huwezi kuacha kuitaja. Hii ni kutokana na mfumo mzima wa ardhi unavyofanyika, hasa viongozi wa serikali za vijiji wanaoshiriki kuuza ardhi  bila kufuata sheria.


Mwanakijiji anayelalamikia kuporwa ardhi, Hausi Zuberi.
Hivi karibuni, mwandishi wetu alitembelea katika Kata ya Kwamatuku, wilayani Handeni, mkoani Tanga, ambapo kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, wakilalamika kuporwa ardhi zao.

Katika kijiji cha Komsala, wilayani Handeni, mkoani Tanga, baadhi ya wananchi walionekana kumtaja mwekezaji Amina Singa, kuwa anamiliki shamba lenye heka zaidi ya 120 huku akiingia kwa wakulima wengine kupora maeneo yao.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana katika mgogoro huo, awali mwekezaji huyo aliomba heka 60 miaka 20 iliyopita, ila sasa anamiliki pori kubwa, huku akishindwa kulilima, japokuwa anaonekana kutamani maeneo ya wakulima wengine wenye heka zisizozidi tano.

Mkulima aliyejitambulisha kwa jina la Hausi Zuberi, anasema mtu wanayemlalamikia, amekuwa mkatili kiasi cha kuwanyima raha wakulima wanaopakana naye katika eneo lake, jambo linalomfanya atamani kununua sanda kwa ajili ya kuzikiwa endapo atakufa wakati anatetea ardhi katika shamba linalopakana na mwekezaji huyo.

“Mume wa Amina anayejulikana kwa jina la Singa Singa alikuja katika kijiji hichi miaka ya nyuma kidogo kuomba eneo la kulima, hivyo serikali ya kijiji ikampa heka 60, ingawa haijulikani eneo lake limeongezwa vipi hadi kuwa na shamba kubwa kiasi cha kumfanya ashindwe kulima lote.

“Mbaya zaidi ameanza kuingia katika maeneo ya sisi wakulima wadogo ambao tulipewa heka tano na serikali na tunafamilia kubwa, hivyo ni wazi mwekezaji huyu anataka kutuua njaa nabinafsi siwezi kumuachia adhulumu shamba langu,” alisema Hausi.

Mkulima huyo mdogo anayepatikana katika kijiji hicho, anasema mgogoro huo umefika katika Baraza la Kata, hata hivyo masikini hawezi kupata haki, jambo linalowapa imani mwekezaji huyo amepita njia za panya.

Anasema japo Baraza hilo lilifika katika shamba lao kukagua, lakini uamuzi wao wa kumpa haki mwekezaji umeonyesha namna gani agenda ya dhuluma imeandaliwa kwa ajili ya kuwakomoa wakulima wadogo.

Mkulima mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Paulina Anthon, anasema kuwa mgogoro wao na mwekezaji huyo umekuwa mkubwa kiasi cha kuwaondolea imani ya kupakana na mtu mwenye uwezo kifedha.

Anasema kwamba mwekezaji amepora sehemu ya eneo lao kwa wakulima wengi anaopakana nao kwa kupita jiwe linaonyesha mwanzo na mwisho wa eneo lake.

“Kesi hii ilianzia serikali ya kijiji, lakini kabla haijafikia ukingoni wakatuhamishia katika Baraza la Kata ya Kwamatuku, jambo ambalo matokeo yake yakawa machungu kwetu, maana haki yetu ikanyimwa na kupewa mwenye nazo.

“Tunaomba serikali, chini ya Mkuu wa wilaya akaja kijijini kwetu na kutembelea maeneo haya yenye kero kubwa, maana haiwezekani wakulima tukose maeneo ya kulima hali ya kuwa kuna mtu ana eneo kubwa na halimudu kuliendeleza,” alisema Paulina.

Paulina anasema kwa kawaida hakuna haki inayoweza kupatikana chini ya serikali ya kijiji cha Komsala, wala baadhi ya viongozi wa Kata, ukizingatia kuwa mwekezaji huyo anadharau kupita kiasi, hasa kwa wasiokuwa na kipato kikubwa.

Katibu wa Baraza la Kata ya Kwamatuku, Nassib Bakari, anasema kuwa Kata yao ni miongoni mwa zile zenye changamoto kubwa ya migogoro ya ardhi inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na wananchi kutofahamu sheria na viongozi wa vijiji.

Anasema kuwa kijiji cha Komsala kimechangia kuukuza mgogoro huo, maana viongozi wake wameshindwa kuyapatia ufumbuzi kiasi cha kuhamishia katika ofisi ya Kata, ambapo lengo lao ni kujitoa katika lawama.

“Baraza la Kata lilitembelea katika kijiji cha Komsala na kuzungumza na wakulima hao, lakini kwa bahati mbaya walikuwa na hasira kiasi cha kushindwa kutoa ushirikiano kwa wajumbe waliokwenda kusikiliza kero zao.

“Lakini hapo kabla, mgogoro huu uliletwa na Amina, aliyetoa malalamiko ya kuingiliwa katika eneo lake na wakulima hao, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa lingeweza kupatiwa ufumbuzi na serikali ya kijiji maana ndio wanaolifahamu kwa ufasaha jambo hilo,” alisema.

Katibu huyo anasema endapo serikali za vijiji zingekuwa makini na kufuata sheria za ardhi, migogoro hiyo ingekoma. Lakini kwasababu viongozi hao hawafuatilii sheria za ardhi, wanaamua kuchezea migogoro ya ardhi.

Anasema Baraza lao la Kata kwa kipindi cha mwaka mmoja wamepokea kesi 53 za migogoro ya ardhi, huku 9 zikikatiwa rufaa, huku kesi hizo zikitoka katika vijiji vya Komsala, Kweingoma, Kwamatuku, wakati kijiji cha Nkhale ndio pekee kisichokuwa na migogoro ya aina hiyo, maana wamepeleka shauri moja tu.

“Kule Nkhale hakuna migogoro, lakini vijiji vingine hali ni mbaya na Baraza linakutana na changamoto nyingi kupita kiasi, huku kesi hizo zikihusisha watu wa aina zote, yani masikini, matajiri na wengineo.

“Unapoamua kumnyima haki masikini na kumpa tajiri, hata kama alikuwa na haki, lakini jamii itaona serikali imepewa rushwa kama yanavyoweza kusemwa na watu wengi wanaodhani Baraza linajiendesha kwa hisani ya matajiri,” alisema.

Mwekezaji anayelalamikiwa katika mgogoro huo, Amina, alishindwa kulizungumzia jambo hilo kiundani, kwa madai kuwa yeye ndio mlalamikaji na sio mlalamikiwa kama wanavyosemwa wakulima hao.

Hata hivyo, mwekezaji huyo alishindwa kujibu ni miaka mingapi alianza kulima katika ardhi hiyo ambayo sasa imeingia katika migogoro, huku yeye akionyewa vidole na wananchi wengi katika kijiji hicho.

Mimi ndio nimefikisha suala hilo serikalini kwasababu wananchi hao wamevamia shamba langu na kufanya uharibifu, hivyo nashangaa kwamba mimi nimepora ardhi na wananchi,” alisema Amina.

Alipoulizwa anamiliki heka ngapi kijijini hapo alishindwa kujibu, ingawa alisisitiza kuwa yeye ndio amevamiwa na wananchi hao.

Hata hivyo, migogoro ardhi haipo katika kijiji cha Komsala na Kata ya Kwamatuku tu, isipokuwa maeneo mengi ya Handeni matatizo hayo yameshika kasi. Katika Kata ya Misima, iliyopo katika wilaya hiyo, nako kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, wakisema wanaporwa ardhi zao.

Kwa matokeo haya, ofisi ya Mkuu wa wilaya Muhingo Rweyemamu, ina changamoto kubwa ya kulishughulikia tatizo hili ambalo sasa limefikia hatua ya kuzua zogo kutoka kwa wananchi wenye kipato cha chini na kikubwa.

+255712053949


No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...