Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NI kawaida
ya wadau wa mpira wa miguu kulaumu viongozi pale zinaposhindwa kuonyesha soka
safi uwanjani na kupatikana ushindi. Mengi
yatasemwa zikiwamo lugha za matusi ili kuhalalisha maneno yao dhidi ya uongozi
husika.
Ni haki yao,
maana wanachojua wao ni ushindi hata kama kiongozi wanayemlaumu hachezi yeye
zaidi ya wachezaji wanaosajiliwa kwa ufundi au kuchaguliwa katika timu ya Taifa
(Taifa Stars).
Katika
kusema hayo, naamini kwa sasa kila mtu anaangalia uongozi wa rais wa Shirikisho
la Soka nchini, TFF, Jamal Malinzi kutokana na mwenendo wa soka letu.
Kwa matokeo
mabaya hasa ya Taifa Stars na Burundi, mechi iliyopigwa juzi katika Uwanja wa
Taifa, jijini Dar es Salaam na Stars kulala kwa bao 3-0, maneno makali
yataelekezwa kwake, wakiamini uongozi wake unasua sua.
Ni mapema kumsakama
Malinzi, isipokuwa wadau wa soka wampe moyo kama kweli wana lengo la kukuza
sekta ya mpira wa miguu nchini.
Kabla ya
kucheza na Burundi, TFF ilifanya tukio kubwa la kuwatafuta vijana ili
kuwaunganisha kwenye Taifa Stars.
Waliofanikiwa
kuitwa katika timu hiyo ya maboresho ni Benedict Tinoko, Emma Namwondo, Joram
Nason Mgeveja, Omari Ally, Edward Peter, Shirazy Abdallah, Yusufu Suleiman,
Said Juma Ally kutoka Mjini Magharibi.
Wengine ni
Abubakar Ally Mohamed, Hashimu Ramadhani, Omari Athumani, Chunga Said, Mohammed
Seif Said, Ayubu Kassim, Abdurahman Othman, Paul Michael, Mbwana Mshindo na
Bayaga Atanas.
Hichi ni
kikosi ambacho kiliweza kuungana na wachezaji kama vile Frank Domayo, Simon Msuva, Ramadhani
Singano, Aggrey Morris na Said Morad, ambao baadhi yao waliweza kucheza katika
mechi iliyomalizika kwa kufungwa bao 3-0 dhidi ya Burundi.
Kama nilivyosema hapo juu, kwa timu kufungwa, kushinda au kutoka sare ni
jambo la kawaida katika mpira wa miguu duniani kote.
Hivyo kinachotakiwa ni kuendeleza ushirikiano na kuwaunga mkono wachezaji
wa Stars walioitwa kwenye kikosi hicho au watakaoitwa siku nyingine na Kocha
Mkuu Mholanzi Martinus Ignatius, maarufu kama 'Mart' Nooij, aliyetambulishwa
mwishoni mwa wiki.
Badala ya wadau na mashabiki wa soka kushutumu TFF na viongozi wake, wahamasishe
maendeleo ya mpira wa miguu.
Napenda kuona Stars au timu nyingine yoyote ndani ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania inafanya vizuri, ila mwisho wa siku lawama zisibaki kwa viongozi,
hasa tunapoona juhudi na mikakati ya kimaendeleo.
Hii ni TFF mpya baada ya uongozi wa rais Leodgar Tenga kumaliza muda wake.
Bado kunahitajika sera nzuri za kufanikisha ushindi.
Lawama pekee sio njia ya kutuvusha hapa tulipo, maana soka letu lilianza
kutumbukia shimoni miaka mingi.
Uvumilivu, ushirikiano na mawazo sahihi yataweza kutufanya tutembee kifua
mbele kwa kuona si Stars tu inashinda, bali hata klabu zetu zinazinduka na kuwa
vinyozi kwa timu nyingine za nje ya nchi, hasa michuano ya Kimataifa.
Kwa miaka kadhaa sasa timu za Simba, Yanga na nyingine zinazopata nafasi
ya kushiriki michuano ya Kimataifa, kama vile Kombe la Shirikisho na Ligi ya
Mabingwa Afrika hazipati kitu zaidi ya aibu na kuangukia pua.
Hizi ni changamoto tunazopaswa kuzifanyia kazi kama wadau wa michezo na
si kumshushia zigo la lawama rais wa TFF, ambaye ndio kwanza ameingia
madarakani.
Tumpe muda na ushirikiano kwasababu kwa mipango aliyoitangaza, nchi yetu
ina uwezo wa kusonga mbele, hasa kwa kuboresha timu za vijana.
Mungu Ibariki Tanzania.
+255712053949
No comments:
Post a Comment