Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
WIKI
iliyoisha jana nimeimaliza vibaya baada ya kupata habari zilizonipasua kichwa
kupita kiasi. Kiukweli sijapendezwa na habari hizo. Ni kuhusu
mgogoro mkubwa uliokuwa ndani ya klabu ya Coastal Union, yenye maskani yake
jijini Tanga. Awali mgogoro huo ulikuwa siri ya viongozi wao kwa wao.
Sisi wadau
wa soka hususan katika timu hiyo, tuling’amua jambo hilo tangu mapema, hasa
pale Mkurugenzi wa Ufundi na aliyekuwa mfadhili wao, Nassor Bin Slum, kujitoa
pole pole katika majukumu ya klabu hiyo. Kadhia hiyo
niliamini ingetoweka. Kumbe nilijidanganya, maana Msemaji wa klabu hiyo, Hafidh
Kido, naye akatangaza kujiuzuru kwa kuchoshwa na migogoro.
Hapa ndipo
nisipoweza kuvumilia. Siwezi kuvumilia kwasababu
kujiuzuru kwa Kido ni mwendelezo mbaya kwa timu hii iliyoanza kupoteza tena
thamani yake. Coastal imemaliza ligi ikiambulia nafasi ya tisa, yani chupu
chupu kushuka daraja. Kwa timu hii iliyoandaliwa vizuri kiasi cha kuweka kambi
ya wiki mbili nchini Oman, inashangaza kwanini imeangukia pua.
Hata hivyo, sisi wadau hatuwezi kushangaa, maana hakuna
nyumba yenye migogoro kusha malaika wa kheri akawa ndani yake hata kidogo. Ndio hapo ninapoibuka na kuwataka viongozi wa klabu hii na
mashabiki wote kuwa makini. Kama msimu huu imeambulia nafasi ya tisa, basi kuna
hatari msimu ujao ikashuka daraja, maana bado haijatulia.
Tanga ilikua tishio kwa kupitia timu hii ikiwa na wachezaji
kadhaa wenye ubora, akiwamo Juma Mgunda, Razak Yusuf Kareka, Ally Maumba, Abuu
Yasin, Ally Jangalu, Douglass Muhani, Kassa Mussa na wengineo kibao walioweza
kuipa hadhi timu hii.
Viongozi
waache ubabaishaji na kurudia enzi za mwaka
1988 kwa kuishuhudia mkoa wa Tanga ukichanua, maana timu zake ziliwika kupita
kiasi. Taji la Ligi ya Tanzania Bara
lilichukuliwa na Coastal union, wakati Kombe la Muungano lilijumuisha timu za Bara
za Zanzibar lilichukuliwa na African Sports, wakati Kombe la Taifa
linalojumuisha mikoa yote ya Tanzania likichukuliwa na timu ya Mkoa wa Tanga (Tanga Star).
Haya ndio mambo tunayohitaji kwa
manufaa ya soka la Tanzania, hususan mkoa wa Tanga kwa kuona timu hii ambayo ni
kioo cha soka mkoani humo kuacha ujinga na kurudia enzi zao. Wakazi na wananchi wa Tanga pamoja
na mashabiki wa kandanda watawalaani vikali viongozi wa soka wa Coastal Union
wanaoleta urasimu kiasi cha kuwafanya wadau waikimbie timu hiyo.
Mgogoro huo umechagizwa vikali na
wanaojifanya miungu watu kiasi cha kuwakimbiza wadau wachanagiaji, akiwamo Bin
Slum, hali iliyozidisha chuki na uhasama ndani ya timu hiyo. Naumiza kichwa kuhusu usajiri wa
klabu hii msimu ujao na mipango yao kwa ujumla. Nani anaweza kuingiza fedha
zake kwa klabu yenye migogoro?
Coastal kuingiza migogoro hali ya
kuwa wamemaliza ligi wakiwa nafasi ya tisa? Hii ni aibu na lazima wadau tuhoji
uhalali huu. Hakika Siwezi Kuvumilia. Ndio maana
nasema wiki yangu ilimalizika vibaya na pengine itazidi kuwa mbaya kwasababu ya
ubabaishaji huu wa viongozi wa Coastal Union na pengine inaweza kuwa ishara
mbaya kwa klabu hii kongwe jijini Tanga.
Nafahamu
soka linaendeshwa kwa fedha. Fedha hizo zingeweza kutoka kwa wadau mbalimbali,
kwa bahati mbaya gogoro zito linaibuka katika kipindi cha kuweka mikakati
kabambe ya usajiri.
Chonde,
chonde Ahmed Aurora, Mwenyekiti wa Coastal Union unapaswa kuliangalia kwa
umakini jambo hili maana jahazi linazama wakati wakazi na wananchi wa Tanga
walikuamini kuwa utakuwa na maslahi na soka lao, ukizingatia kuwa uso wa soka
la mkoani humo lipo kwa timu hii.
Tukutane wiki
ijayo.
+255712053949
No comments:
Post a Comment