https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Friday, April 25, 2014

Pitia mchango wa kimaandishi wa Maria Sarungi Tsehai kwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba

Mh. Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii nichangie kwa maandishi mjadala unaoendelea bungeni kuhusu sura ya 1 na ya 6 na kuhusu mwenendo mzima wa Bunge lako tukufu.
Mh Mwenyekiti, tokea tumefika Dodoma zaidi ya siku 70 tumeweza kushuhudia mengi, katika huu mchakato wa kujadili rasimu ya pili ya Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunamaliza siku rasmi tulizopangiwa bila kufanya maamuzi yoyote kuhusiana na Rasimu na bila muafaka.
Maria Sarungi pichani.
Mh. Mwenyekiti, tunamaliza siku hizi 70, tukiwa tumegawanyika na kuparanganyika katika makundi, na kilichobaki ni kurushiana vijembe, kutukanana, kususiana na kununiana. Bunge lako tukufu lilitakiwa kuwa kioo cha muafaka wa kitaifa ila sasa tumegeuka na kuwa chanzo kinachosababisha mpasuko ndani ya jamii.  Na ikiwa hali hii ya mpasuko ndani ya Bunge itaendelea kuwepo, kuna hatari kubwa ya kuhatarisha amani na utulivu tunaojivunia ndani ya nchi yetu – naomba jambo hili tulisichukulie kama mzaha. 

Mh. Mwenyekiti, kama utakumbuka nilichangia awali kabisa chini ya uenyekiti wa muda wa Mh. Pandu Kificho na nilizungumzia ubabe wa walio wengi (Tyranny of Majority) na jinsi inavyoweza kupelekea mchakato huu kuharibika. Leo maneno haya yametimia. Ieleweke kuwa mi si nabii bali ni mwanafunzi mzuri wa historia. Na siku zote maridhiano na ushirikishwaji wa pande zote ni sehemu muhimu ya mchakato kama huu wa kuandika Katiba.
Mh Mwenyekiti, Tanzania tunasifika duniani kwa kuwa mstari wa mbele kukomboa nchi za kiafrika na kupatanisha mataifa.  Baba wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Nyerere aliongoza michakato mingi na mojawapo kubwa ni mapambano ya watu weusi dhidi ya utawala dhalimu na wa kibaguzi wa makaburu huko Afrika Kusini. Nilifarijika sana kumsikia aliyekuwa Rais wa Pili wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki katika video akizungumzia juhudi za Mwalimu Nyerere hata katika mchakato wa kuandika katiba yao ya Afrika Kusini. Katiba ambayo inasemekana ni moja ya katiba bora barani Afrika.


Mh. Mwenyekiti katika video hii inayopatikana Youtube, aliyekuwa rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki alieleza ni jinsi gani Mwalimu Nyerere aliwashauri ANC,   pamoja na kuwa ingeweza kutumia nafasi ya kidemokrasia na kuchagua wajumbe wa Bunge lao la Katiba, Mwalimu alisema ilikuwa muhimu kukaa na ‘adui’. Na alishauri kuwa ANC wakae na wahasimu wao yaani makaburu kabla ya Bunge lao la Katiba kuanza na kukubaliana katika misingi mikuu itakayowaongoza vyama vya siasa - “set of guiding principles”. Na Thabo Mbeki alieleza kuwa ndicho walichofanya na walifanikiwa kuandika Katiba mpya ambayo iliridhiwa na vyama vyote na makundi yote nchini Afrika Kusini. Pamoja na wingi wao, ANC walifuata ushauri wa Mwalimu Nyerere kuwa katika masuala ya kutunga Katiba, ni muhimu sana kuwa na maridhiano na upande mwingine, na sio tu wengi wape.  Hii iliwafanya ANC wafanye majadiliano na maridhiano na makaburu pamoja na kuwa walikuwa na historia ya uonevu, ubaguzi na umwagaji damu.

Mh. Mwenyekiti, lengo la kutoa mfano huu ni kujaribu kuonyesha kuwa mchakato huu tokea tumeuanza hapa Dodoma, tulianza bila maridhiano juu ya misingi mikuu ya kutuongoza. Na mpaka sasa bado muafaka huu haujapatikana. Maridhiano ni lazima na yanahitajika kabla sisi wajumbe wote 629 hatujaendelea na vikao. Maridhiano haya yanatakiwa yahusishe pande zote yaani vyama vya siasa lakini hata sisi wawakilishi wa vikundi ambao hatufungwi na maslahi ya kisiasa.

Mh. Mwenyekiti, maridhiano haya lazima yahusishe suala la muungano na muundo wa serikali kwani inaonekana ndo chanzo kikuu cha mpasuko hivi sasa. Ushauri wa Mwalimu Nyerere uzingatiwe kwani si suala la kuwa na idadi kisheria ya kupitisha ibara za rasimu, au kuwa na uhalali au akidi ya kufanya vikao. Bali ni suala la kuandika katiba yenye maslahi kwa wananchi WOTE wa Tanzania na itakayodumu kwa miongo kama si karne zijazo.

Mh. Mwenyekiti, kwa kumalizia ningependa kukuomba kwamba kama mwenyekiti wetu ambaye wengi wetu hata mimi binafsi tulikuamini sana, sasa uonyeshe uongozi wako shupavu na uhakikishe unarudisha hadhi na heshima ya Bunge lako tukufu kwa kukemea na kuadhibu vitendo vinavyokinzana na kanuni ikiwa ni pamoja na matumizi ya lugha ya kuudhi, matusi na kebehi. Nafahamu fika kuwa wewe binafsi unapenda midahalo na mijadala yenye tija, tuongoze tuweze kujadili hoja na kukubali kutokubaliana kwa ustaarabu.
Asante
Maria Sarungi Tsehai

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...