Na Kambi
Mbwana, Dar es Salaam
NITAUMIA
kama kuna mtu atashindwa kuipongeza timu ya Azam iliyofanikiwa kutwaa ubingwa
wa Tanzania Bara msimu huu.
Ndio, maana timu
hii imeweza kunyakua ubingwa mbele ya timu za Doto na mwenzake Kulwa zinazoaminika
ni timu vigogo vya soka vya Tanzania Bara. Kwa
wasiojua, timu za Doto na Kulwa, basi ni Simba na Yanga, zilizoanzishwa miaka
ya 1935 kwa Yanga na 1936 kwa mwenzake Simba SC.
Wakati
inanyakua ubingwa wa Tanzania Bara, wapo baadhi ya watu wanaoshikwa na machungu
kiasi cha kufikiria kuwa Azam wameshinda kwa kubebwa, jambo ambalo si kweli
hata kidogo.
Hapa siwezi
kuvumilia kamwe. Siku moja baada ya kushinda mbele ya Mbeya City kwa bao 2-1
jijini Mbeya, Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi aliibuka akisema kuwa Azam
wanabebwa.
Hapa unaweza
kushangaa kauli hii. Tujiulize. Vipi Mbeya City wangefungwa na timu za kina
Doto na Kulwa yani Simba na Yanga?
Vipi timu
hizi zingeendelea kutawala soka la Tanzania kwa kuibuka mabingwa kila mwaka?
Hapana. Hii si njia nzuri.
Kwa timu
kama Azam FC, nathubutu kusema kuwa imestahili kunyakua ubingwa wa Tanzania
Bara. Na inastahili pia kushiriki michuano mikubwa, ikiwamo Ligi ya Mabingwa
Afrika, msimu ujao.
Wasimamizi
wa soka la Tanzania, Shirikisho la Soka nchini (TFF) iwe makini katika hili.
Azam ni miongoni mwa timu zenye wachezaji mahiri mno.
Hata hivyo
haitoshi, pia imewekeza vizuri, hivyo sioni ajabu ikichukua ubingwa wa Tanzania
Bara au hata taji lolote barani Afrika.
Huu ni
wakati wa kujivunia matunda ya uwekezaji mzuri wa soka na kuachwa kubabaishwa
na timu zinazojiita vigogo.
Tangu
kuibuka kwa timu ya Mbeya City, nilipenda aina ya soka lake. Kuna uwezekano
mkubwa soka letu likapanda chati kwa kuzalishwa wachezaji wazuri kutoka katika
timu za kawaida huko mikoani, maana soka halipo Simba na Yanga tu.
Huu ndio
ukweli hivyo ni wakati wetu kujivunia na kuwaunga mkono mabingwa wapya, timu ya
Azam FC, huku nikishindwa kuvumilia kama yupo anayeumizwa na matokeo haya.
Ndio maana
nasema, hizi timu za kina Doto na Kulwa zifikie wakati zithaminiwe kwa ukongwe
wao ila si kwa soka lao. Hazina kitu kabisa hizi.
Zimechoka,
zimeishiwa. Ni Baraka ya majina tu, ila uwanjani ni sifuri.
Tuonane wiki
ijayo.
+255712053949
No comments:
Post a Comment