https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Thursday, February 07, 2013

Huna haja ya kumvumilia mwenye ‘pepo la ngono’



 MAMBO FULANI MUHIMU
Wapendanao wawili.

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
NIMEKUWA nikijikita zaidi kuandika makala zinazotokana na maswali ya wasomaji wangu wanaoniunga mkono tangu kuanza kwa makala haya.
 
Nashukuru kwa hilo, maana kitendo cha kusomwa tu, kinanipa nguvu ya kuendelea kuwapo katika kona hii inayokujia kila Jumamosi ikichambua mambo mbalimbali ya kimapenzi.

Kwa siku kadhaa, nimekuwa nikiulizwa maswali yanayohusu uaminifu wa wapenzi au wanandoa. Kwa mfano, yupo dada mmoja ambaye jina lake sipo tayari kuliweka katika gazeti la Mtanzania la Dar es Salaam Tanzania, linalochapisha makala haya kila Jumamosi, aliniuliza hivi; mpenzi wangu sio muaminifu, maana kila ninapokwenda kwake nasikia kashfa nyingi za kutoka kimapenzi na watu wengine na nikimuuliza anajibu ndio amefanya nao na kuomba msamaha.


Hili lilikuwa swali lililotanguliwa na maneno mengi kutoka kwa msomaji huyo wa Mambo Fulani muhimu. Jibu langu lilitanguliwa na swali, wakati unasikia maneno hayo kutoka kwa watu, je umefanya uchunguzi wako na kugundua ni kweli?

Nasikitika dada huyu alijibu ni kweli, hivyo mtu huyo si muaminifu. Ana pepo la ngono, akichukulia kitendo cha kuishi mbalimbali na mtu wake, maana wapo mikoa miwili tofauti.

Katika hali ya kawaida, kama mwanamume anakiri ndio tabia yake ya kutoka kimapenzi na wanawake wengine, tena akasema bila woga kwa mwanamke wake, basi ana udhaifu.

Na maneno yake wakati mwingine huyatoa kwa maana mbili; mosi ni kuonyesha uhuni wake, au uanaume wake kama wanavyosema watoto wa mjini.

Pili, anaongea hivyo ili mwanamke huyo achaguwe la kufanya, kuendelea kuwa nae au kuachana nae. Kwanini nasema hivyo? Kama kweli mwanaume anakiri kutembea wanawake mtaani kwao kwa kumwambia mchumba wake, je, akisikia yeye wanaume wanaotoka na mtu wake atachukua hatua gani?

Mara nyingi inapotokea hatua hii, mwanaume kujua wanaotoka na mke, au mchumba wake, huvunja uhusiano wao. Kwa sababu hii basi, jibu ni kwamba hakuna haja ya kumvumilia mwenye pepo la ngono kwa Dunia hii yenye maradhi mengi.

Endapo umegundua mume au mchumba wako si muaminifu, ukamuuliza na kukiri kosa, basi achana nae hasa kama tabia hiyo itaendelea kila siku.

Kwa kawaida, aliyetembea na msichana mwingine zaidi ya Yule wake, kwa bahati mbaya kama wanavyomsingizia shetani kila siku, hakika hawezi kurudia kila wakati. Yani kweli kila 
siku unakosea kwa bahati mbaya? Yani kila siku shetani?

Hapana na kuna haja ya kuangalia uhusiano wetu. Unapaswa kutoa picha kamili ya uhusiano wako. Mwambie wazi, kama bado upo busy na mihemko ya wanawake watu wa nje, basi fanya kwanza na ukichoka utaniambia.

Huo ndio ukweli, maana mwenye mapenzi ya dhati kwa menzake hawezi kufanya uchafu kila siku ya Mungu na kumsingizia shetani na kuomba msamaha.

Wakati mwingine lazima watu waangalie heshima zao, maana inapotokea mpenzi wako, mume au mke wako anakuwa sio muaminifu, hata heshima ya kutembea mtaani inapungua.

Kila unapofika, watu wanakushangaa au kukusindikiza kwa vidole, wakiangalia uzuri wako, heshima yako na bado unayejidanganya kuwa unampenda, yupo ‘busy’ na wapita njia.

Jiweke kando unapoona hakuna mabadiliko kwa mpenzi wako, maana usipokuwa makini, utaambulia maumivu kila wakati, hasa kwa kuwabaini wanaotembea, wanaofanya uchafu na mtu wako, ingawa wewe unajiheshimu.

Hii ipo zaidi kwa wanawake, maana wakati mwingine mfumo dume unasababisha wao wakikutwa na watu wa pembeni kuachika na wao wanapowakuta wezi wao kuombwa msamaha, wakifikiriwa ni wepesi kusahau na maisha kuendelea.

Mapenzi ni matamu lakini yanatesa kama uliyekuwa naye si muaminifu kwako, ukizingatia kwamba atakupa wasiwasi wa kufikiria anachofanya, hivyo kukupa ugonjwa wa moyo bure tu.

Jichunguze wewe na mtu wako kwa faida ya uhusiano wenu, ili mapungufu yaliyojitokeza kuachwa kama kweli mna ndoto za kufunga ndoa kwa wale wapenzi au wachumba.

Kinyume cha hapo, ni mateso na majuto maana uliyekuwa naye anafanya sikukuu ya kutembea na watu wa pembeni kila siku ya Mungu.

Tukutane wiki ijayo.
0712 053949
0753 806087

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...