https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Tuesday, February 12, 2013

TFF yawapigia magoti mashabiki wa soka Tanzania



Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah

Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linawataka washabiki wa mpira wa miguu kujitokeza kwa wingi wikiendi hii kuzishangilia timu za Azam na Simba zitakazocheza mechi za mashindano ya Afrika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo mchana, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kwamba Nguvu ya washabiki ni muhimu katika kuziweza timu hizo kufanya vizuri katika mechi hizo za nyumbani dhidi ya Al Nasir Juba ya Sudan Kusini na Club Libolo ya Angola.

Azam itacheza Jumamosi (Februari 16 mwaka huu) dhidi ya Al Nasir katika mechi ya Kombe la Shirikisho wakati Simba itaikabili Club Libolo kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayofanyika Jumapili. Mechi zote zitachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Aidha, Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inamaliza raundi ya 16 kesho (Februari 13 mwaka huu) kwa mechi kati ya wenyeji African Lyon dhidi ya Yanga itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi hiyo itakayochezshwa na mwamuzi Martin Saanya kutoka Morogoro inakutanisha timu zenye mazingira tofauti. Wakati Yanga wakiwa ndiyo vinara wa ligi hiyo kwa pointi 33, African Lyon ambayo sasa inanolewa na Salum Bausi inakamata mkia ikiwa na pointi tisa tu.

Nayo Toto Africans itaikaribisha Polisi ya Morogoro kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Jacob Adongo kutoka Musoma. Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 20,000 utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mgambo Shooting na Oljoro JKT.

Nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Maxime ambaye sasa ni kocha wa Mtibwa Sugar ataiongoza timu yake hiyo katika mechi dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani, Morogoro. Ni kwenye uwanja huo huo ambapo Mtibwa Sugar katika mechi yao iliyopita walichapwa mabao 4-1 na Azam.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...