https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Tuesday, February 26, 2013

TFF sasa yatangaza kikao kujadili uamuzi wa serikali



Rais wa TFF, Leodgar Tenga
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SEKRETARIETI ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imepokea barua ya Serikali ikielezea uamuzi wa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara kutengua uamuzi wa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo nchini kuidhinisha marekebisho ya Katiba ya TFF toleo la 2012.

Baada ya kupokea barua hiyo jana alasiri (Februari 25 mwaka huu), Sekretarieti iliwasiliana na Rais wa TFF, Leodegar Tenga ambaye ameagiza kuitishwa kikao cha dharura cha Kamati ya Utendaji kujadili tamko hilo.


Kikao hicho cha Kamati ya Utendaji ya TFF kitafanyika Jumamosi (Machi 2 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.


Katika hatua nyingine, Mwamuzi msaidizi wa FIFA, Ferdinand Chacha ameondolewa kuchezesha mechi za VPL baada ya kupata alama za chini kwenye mechi kati ya African Lyon na Simba iliyochezwa mwezi uliopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Waamuzi wanaopata alama 6.5 au chini ya hapo kati ya 10 zinazohitajika pia wanaondolewa kwenye mechi za VPL na FDL.

Waamuzi wengine walioondolewa kwa kutomudu mechi walizochezesha za VPL ni Mathew Akrama (Yanga vs Simba), Ephrony Ndissa (Yanga vs Simba), Ronald Swai (Yanga vs Mtibwa Sugar).  

Walioondolewa kwa kupata alama za chini ni Alex Mahagi (Simba vs JKT Ruvu), Methusela Musebula (Toto Africans vs Coastal Union), Lingstone Lwiza (Toto Africans vs Coastal Union), Idd Mikongoti (Toto Africans vs Mtibwa Sugar) na Samson Kobe (Toto Africans vs Mtibwa Sugar).

Masoud Mkelemi aliyekuwa mwamuzi wa mezani katika mechi ya FDL kati ya Moro United na Villa Squad ameondolewa kwa kutofika kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi (Pre-match meeting) na alichelewa kwa dakika tano kufika uwanjani.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...