https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Tuesday, February 19, 2013

Nguvu hizi za urais CCM ni ishara gani?



Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa

Na Rahimu Hemed, Dar es Salaam
INASIKITISHA kuona Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inayumbishwa na makada wake wanaotajwa kuwa na dhamira ya kugombea Urais kwa tiketi ya Chama chao, mwaka 2015.
Waziri wa Mambo ya Nje, Bernald Membe

Wana CCM hawa wamekuwa wakitumia nguvu kubwa katika kuweka sawa mitandao yao kwa ajili ya kujiweka pazuri katika kuelekea ‘ubwana mkubwa’ huo ifikapo mwaka 2015, ambapo mchakato wake umezidi kupamba moto.
Katibu Mkuu wa Chadema, Wilbroad Slaa

Ni kitendo cha kuchanganya kichwa na kinachoweza kumtoa Mtanzania machozi, kuona kumbe wapo watu ambao wanachowaza wao ni kuongoza tu, hata kama hawana jipya.

Mtu hana dhamira wala utu moyoni mwake, lakini inashangaza kuona anafanya kila awezalo kujifagilia yeye na watu wake. Kwa bahati mbaya, baadhi yao, wanachoangalia wao ni mtandao wao kuneemeka hata kama hawana tija.

Kwa mfano, katika Chama Cha Mapinduzi CCM, yapo majina makubwa yanayotajwa kuwa na nia ya kugombea urais mwaka 2015, ambao ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, Samuel Sitta, Edward Lowassa na wengineo.

Ingawa hawajatangaza hadharani ukiacha, Sitta ambaye aliwahi kukaririwa akijitangaza kuwa anafaa kuwa Rais wa Tanzania, lakini dhamira yao inaonekana.

Mtu kama Lowassa, huwezi kuacha kumuona katika vyombo vya habari kila siku, akidaiwa kusema hili au kutoa kile katika shughuli za kidini, hasa kwa Wakristo wanaomualika mara kwa mara katika sherehe zao.

Najua kuwa yoyote anaweza kuwa Rais wa Tanzania, lakini wasiwasi wangu ni hii nguvu kubwa inayotumiwa na baadhi yao katika kuelekea kiti hicho, ambacho sasa kipo chini ya Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika Chaguzi za ndani za CCM mwaka jana, tuliona jinsi makada hao walivyotunishiana misuli, huku baadhi yao pia wakitajwa kumwaga fedha katika kuimarisha makundi yao.

Ni jambo la ajabu mno. Wanachama hao wa CCM, katika kuelekea kwenye mbio hizo, wamesababisha hadi uhasama kwa makundi yao, hasa pale wapowapigia debe kwa njia mbaya na kuleta malumbano ya aina yake na hata kurushiana maneno machafu.

Ni kweli usiopingika kuwa kila chama chenye uhai, ni lazima kuwe na uhasama katika kuelekea jambo moja la maana; lakini si kama inavyofanywa sasa na wafuasi hao wa CCM.

Hawa wameweka mbele tama ya kushika dola na sio kuwaongoza Watanzania wanaosumbuliwa na matatizo lukuki, ikiwamo elimu duni, afya ya kuunga unga, njaa na shida ya maji katika maeneo mengi ya yanayounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ukienda kwenye mitandao ya kijamii utakutana na lugha zenye ukakasi, vijana au wafuasi wa mabwana wakubwa hawa jinsi wanavyoonyeshana umwamba kwa kutukanana.

Utu wa Mtanzania sasa umetoweka kabisa. Nguvu kubwa imewekwa katika kuitaka nafasi hiyo ya Ikulu. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kulikemea jambo hili.

Alisema siku zote mtu anayeng’ang’ania kwenda Ikulu anafaa kuogopewa kama ukoma. Akasema, “Ikulu ni mahali patakatifu.” Kwamba mahala pale hapahitaji mchezo na mzaha.

Yule anayetaka nafasi hii lazima ajipime kama kweli ana uwezo huo kwa kuangalia na kubuni mbinu za kuinua uchumi wa Taifa kwa vitendo na sio porojo, au kuangalia namna ya kuwajaza mapesa, maisha bora kundi lake kwa kuwateua kwenye nafasi zenyemguso.

Hili haliwezi kukubalika hata mara moja. Kwa kuwa Tanzania ni yetu wote, hivyo kila Mtanzania anapaswa kuangalia jinsi baadhi ya wanasiasa wetu, hasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanavyotaka nafasi hiyo ya Urais kwa uroho kupita kiasi.

Nikiwa kama Mtanzania na ninayefuatilia siasa, nimekuwa nikifanya utafiti wangu mara kwa mara na kugundua kuwa baadhi ya wilaya au mikoa, imeathiriwa mno na siasa za Mtandao.

Unaweza kuona Mkuu wa Wilaya hapatani na Mbunge, hasa kwasababu watu hawa wawili wanapingana katika kambi zao. Hili si jambo zuri hata kidogo na hakika linastahili kupingwa vikali kwa ajili ya maisha bora kwa kila Mtanzania.

Kama sio makundi nini kingine? Mkuu wa Wilaya anateuliwa na Rais, yani anakuwa mwakilishi wa Rais. Lakini mbunge yeye anachaguliwa na wananchi, lakini kwa bahati mbaya, wabunge wengi huingia kwenye mtandao kabla na baada ya Urais.

Kwa mfano, katika Uchaguzi wa mwaka 2010 ambao Kikwete alirejea tena madarakani kwa kupewa nafasi na Watanzania wanaompenda na kumheshimu, lakini ukweli ni kwamba wale waliokuwa na dhamira hiyo ya kupokea kijiti chake hawakurudi nyuma zaidi ya kujipanga, wakiamini kuwa miaka mitano sio mingi.

Hivyo basi, waliogombea ubunge na kupata wakiwa kwenye kundi hilo, waliendelea kuwa kwenye mtandao wao na walioshindwa, bado waliungwa mkono kwa kusaidiwa kila kinachostahili.

Katika siasa za Tanzania, wapo watu ambao wanagombea wao lakini bajeti inatoka kwa wengine. Kwa mtindo huu, utaona jinsi mbio hizi zinavyoweza kuitikisa nchi siku za usoni.

Kwanini? Haya yote yanaletwa na dhamira ya kuwatetea Watanzania kutoka kwenye njaa hadi kupata ahueni na maisha bora au wanataka tu kujinufaisha wenyewe?

Fedha hizi zinazomwaga na makada hawa kutoka CCM zitarudi kwa mtindo gani na wapi zinapotoka? Urais si jambo dogo. Kwa wanaokwenda Ikulu kuwaongoza Watanzania hakika Ikulu ni mzigo.

Inashangaza kama wengineo wanakuwa na nia ambayo si nzuri, ndio maana wengineo wameamua kuzalilisha watu wao, jamii yao, ndugu au binadamu wenzao kwasababu za kijinga kabisa.

Serikali ya CCM, chini ya Mwenyekiti wake, JK, inajua jinsi inavyoyumbishwa na makada hawa. Ndio, maana wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema kutendo cha Kikwete kutowapendekeza wanaotajwa kuwania urais mwaka 2015 kwenye Kamati Kuu CC ni dalili za kuwapunguza makali baadhi yao.

Katika Kamati Kuu, majina ya Membe, Lowassa, Sitta hayakuwapo, hivyo kuwanyima nafasi ya kuendeleza makundi yao ndani ya Kamati hiyo yenye umuhimu mkubwa kwa serikali ya CCM.

Pamoja na hayo, bado wataalamu wa mambo wanaendelea kuchambua kuwa, mkakati huu wa Kikwete ulikuwa hatua muhimu kwake kama kiongozi wa chama baada ya kukwama kuzuia makundi kung’ara katika chaguzi zilizopita ambapo wafuasi wa Edward Lowassa waliibuka kidedea kuanzia katika NEC, mikoani na Jumuiya za chama hicho, ambapo kwa siasa za Tanzania, inaweza kuwa chapuo kwa Waziri Mkuu huyo wa zamani, aliyelazimika kujiuzulu.

Kila mmoja alishuhudia baada ya kumalizika Uchaguzi wa wajumbe wa NEC, Kikwete alisita kuunda CC kwa maelezo kuwa waliochaguliwa walikuwa wageni, hivyo binafsi alikuwa hawafamu vizuri.

Kwa jinsi hali ya mambo inavyoendelea, hatua hii ya Kikwete ilitafsiriwa kama mkakati wa kuzima nguvu ya mojawapo ya kambi, bila kutajwa kuwa ni ya Lowassa, Membe au Sitta, ingawa ukaribu wa familia ya Kikwete, ikiongozwa na mtoto wake, Ridhwani na mama yake, Mama Salma Kikwete, watu wanabashiri kuwa wapo kambi ya Membe, ambaye kwa hakika anahitaji nguvu za ziada ili apitishwe na chama chake kuwania urais huo kama ni kweli ana lengo hili.

Inajulijulikana umuhimu wa Kamati Kuu, maana hatua ya Kikwete kutopendekeza majina makubwa na yenye nguvu ndani ya CCM kuwania ujumbe huo, inaweza ikawa ni njia ya kuwafanya wajumbe wa CC kuwa na kazi moja tu ambayo ni kuchuja majina ya wagombea badala ya wao pia kuwa washiriki, hivyo ikawa rahisi kujipigia chapuo, ukizingatia kuwa kila linalojadiliwa nao watakuwapo.

Hayo yote ni muendelezo wa nguvu kubwa ya wanasiasa hawa wanaowania nafasi ya Urais wa Tanzania, ingawa bado wamekuwa kimya, kwasababu wanajua kuwa sio picha nzuri kujitanga mapema kuwa wana lengo la kuwaongoza Watanzania.

Nguvu kubwa hii inaleta picha gani? Ni kweli wanataka kuwaongoza Watanzania au wanataka kujineemesha wenyewe? Maswali kama haya yanahitaji yajikite katika vichwa vyetu, tuwaze na kufikiria mara mbili kwa ajili ya nchi yetu.

Nimejikita zaidi kwenye siasa za CCM kwasababu purukushani zao ni nyingi na pia wao ndio walioshika dola. Ingawa upinzani upo na una nguvu kubwa, ila kwakuwa fedha na nguvu zinazotumiwa na wanasiasa kutoka Chama Tawala, basi ni wajibu wetu kuhoji na kuwabana katika matumizi hayo yasiyokuwa na tija.

Pamoja na matumizi hayo, pia wafuasi hao, makada hao wa chama tawala lazima wajuwe watashindana huko kwa kadri ya uwezo wao, lakini bado karata itabaki kwa wapiga kura, Watanzania ambao kwa hakika wanalingia upinzani kuimarika na kuwa na imani kubwa na viongozi wa vyama vya upinzani kwa namna moja ama nyingine.

Leo hii ambapo Chama Cha Wananchi CUF, Chadema, TLP hakika heshima zao ni kubwa na wanapendwa na Watanzania, hivyo hawa ambao wanaona wamezaliwa ili wawe marais, hakika kazi wanayo.

Mbio hizi, matumizi mabaya ya fedha kwa ajili ya kuneemesha ngome zao, zinazua maswali kede kede kwa watu wenye uelewa wao, dhamira yao na machungu ya kweli ya kuhoji kwanini wanasiasa hawa wanatumia nguvu kubwa kuutaka urais wa Tanzania?

Wanataka nini hawa? Kama swali hili ni la uongo, basi lipo karibu na ukweli, ndio maana pamoja na kusemwa sana, kutajwa katika harakati hizo, wakibanwa hawakanushi, zaidi ya kusema urais sio dhambi.

Mungu ibariki Tanzania.
0766 453862

 

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...