https://tpc.googlesyndication.com/simgad/8045142562622600543


Recent Post

Monday, February 11, 2013

Mdau wa Handeni atoa somo; (Vinohaluse hano chili habuka kwiha)

Adam Malinda, pichani.

Na Adam  Malinda,Dar es salaam.
KUPITIA mtandao wa Handeni kwetu ningependa wale wote wanaoamini kuwa kusaidia ndugu zao na jamii inayosurubika katika wilaya ya Handeni kuhusu njaa na ukame wa muda mrefu, wamesaidia kwa kumuamini mwenyezi mungu kwa imani zao , watakuwa wamefikiri jambo la busara.

Umefikia wakati tukumbushane, tuone umuhimu wa kujenga mapenzi ya kweli na nyumbani kwetu, tusifikiri kuwa wanasiasa tukiwaachia ni wajibu wao kuleta maendeleo, lakini pia wajibu huenda pamoja na haki, nasi ni haki yetu kuguswa na shida mbalimbali za nyumbani hususan sekta za afya, elimu, kilimo na miundombinu.

Nasema haya kwa sababu viongozi tunaowachagua si malaika wa kuweza kufanya kila jambo, muda mwingi tumeutumia kuwalaumu, ni kweli walipoomba nafasi ya kuitumikia jamii walifahamu kuwa hawana uwezo wa kamaliza kila shida za wananchi ,lakini waliahidi, hivyo ni haki yao kualaumiwa, je tangu tuwalaumu tumeongeza tatizo ama tumeweza kupata ufumbuzi kwa kuwalaumu.


Njia pekee ya kujali kero za Handeni ni kujiunganisha na kuwa na nguvu ya pamoja ili  Handeni kwanza madaraka na vyeo baadae, hii itatusaidia kuondoa wingu zito la kasi ndogo ya maendeleo linaloikabili eneo la wilaya yetu.

Haisaidii kumlaumu mbunge, kwa kuwa aliyoyafanya ndipo uwezo wake ulipoishia, tusimlazimishe ng’ombe kuota mapembe kama ya nyati ilhali umbile lake na hulka viliishia hapo, tuone tunaweza kufuga mnyama gani mwenye mapembe tunayoyahitaji, yanayoweza kutoboa mibuyu.

Lakini aina ya mapembe tunayoyataka yatategemea lishe bora tunayompa, maana kiongozi bora ni yule mwenye kuwa na ushiriki wa karibu na wananchi wake,kauli nzuri, ushirikiano, kujuliana hali ya mazingira husika na kuona kinachoweza kusaidia kuondosha tatizo.

Nasema kauli mbiu iwe Handeni kwanza kwa sababu huwezi kuwa unaguswa na kuzorota kwa maendeleo bila kushiriki kuonesha njia ya kufufua maendeleo, njia ya kwanza wana mtandao mjue ni mshikamano wa dhati toka mioyoni, kuendesha makongamano na vikao vya kujadili mustakabali wa Handeni .

Mfano sasakuna njaa katika maeneo mengi ya wilaya hii na majirani zao, lakini jitihada gani zimechukuliwa na mamlaka husika, je sisi kama wana handeni tumejipanga vipi kuunga mkono jitihada hizo, hii ni kudhihirisha tunafuatilia kwa karibu masuala yanayogusa nyumbani.

Aidha tujitathimini wenyewe kwa kujiuliza kila hatua moja unayoifanya ama kuchangia mjadala kuhusu Handeni unafikiri kwa ajili ya kumfurahisha mdau wako, unalinda maslahi ya mtu, ama hulka yako ni unafiki.

Tukubaliane kuwa Handeni tatizo lipo, haliwezi kumalizwa kwa njia ya kujipendekeza, halitafuti nani atakuwa maarufu, bali tuungane kwa pamoja kwa ajili ya kuona kila mmoja anakuwa mchangiaji kwa namna moja ama nyingine kuhakikisha jamii yetu inapambana na tatizo la njaa, ukosefu wa maji safi na salama, afya zikiwemo zahanati, na shule zenye sifa ya kuitwa shule ili ipatikane elimu bora si bora elimu.

Kuwavisha watoto wetu wakafanana, wanapendeza, bila kuwa na majengo bora, walimu wenye sifa na uwezo wa kufundisha, wameandaliwa kisaikolojia na vitendea kazi , hatuwezi  kuwa na elimu bora Handeni.

Ikiwa mama wajawazito wanatembea umbali wa kilometa kumi kupata huduma za uzazi, bado tupo mbali  na dunia ya leo, zahanati zisizokuwa na dawa, wauuguzi wa kutosha vifaa tiba duni, bado tutakuwa na mzigo mbele ya huduma za afya inayostahili.

Kama kilimo cha jembe la mkono ni kipaumbele cha serikali ya wilaya, njaa itakuwa imeweka kambi Handeni, lazima tuhakikishe makundi ya rika la kati na vijana wanakopeshwa matrekta kwa ajili ya kulima mashamba makubwa ya mazao ya chakula na biashara, hali itakayowezesha kilimo kuwa na tija na kuwavutia vijana vijijini , kuwaondoa woga wa kilimo cha jembe la mkono.

Lakini ni vizuri kufanya upembuzi yakinifu katika kuona matrekta hayo yanakuwa ya aina tofauti, kwani maeneo mengi ya Handeni yanahitaji kwanza matrekta ya kung’oa miti na visiki ndipo yaingizwe matrekta ya kulimia.

Sasa Handeni imepewa wawekezaji wa madini, milima yote inayoonekana imekuwa katika himaya ya wawekezaji wazawa na wageni, bila kujipanga Handeni inaweza kuwa shamba la bibi, wazawa wakibaki kuwa masikini wa kutupwa, wageni wakizoa mali kwenda nazo makwao .

Tunasikitika kuwa baadhi ya vigogo waliopo serikalini na vibaraka wao wameanza kampeni za kukomesha kauli za kudai haki kupitia magazeti , ili wana handeni wakose pa kusemea, yaani wanajaribu kutuziba midomo, lakini tunaamini hawataweza, wanajaribu kuziba shimo la panya kwa mkate.

Kwa ujumbe huu naomba wanamtandao mfahamu haki haiwezi kutolewa kirahisi, haki hudaiwa kwa nguvu, muda wa kuwaacha wafanye wanavyotaka umekwisha, kama wanataka amani iwepo Handeni, wakubali kukaa pamoja na kujadiliana matatizo ya Handeni, lakini kama wanaendelea kuwa na makundi yao ya kipambe kwa ajili ya kuididimiza Handeni, hatutakubali kamwe, Cuba ilikombolewa na wanajeshi 7 wakiongozwa na Fildel Castro, wengine wengi walipoteza maisha katika jitihada za kuleta ukombozi wa kweli.

Wana handeni mashariki-magharibi, kusini-kaskazini, kwetu ni bora kuliko kwa mwingine, ukisifia kwa mwenzio ushakuwa mtumwa, ukimpenda baba wa mwenzio umemtukana mama yako, Handeni yetu nzuri inahitaji umoja na mshikamano kupambana na changamoto za kudumaza maendeleo ya Handeni.

Vinohaluse hano chili habuka kwiha,chimwe mizi ,chisumka Handeni, vinochikekala neichilo ntongo zetu hazikwiza vyedi, kukaya kuna gumbo, wantu wagonela maizii, suwe chadya chips na nguku, kindedi ivyo nivyo vikikalwa, hechina mbazi na kukaya, nagaa ivyedi chidugane chifanyanye vikudamana  chongeze ubala ukuleka chikegala nkande wayetu wapate nguvu yo ukulima chani  mwakani mnungu akajalia gumbo disekuchiwia, kukaya kukataa kuna  gumbo hata suwe chimwedigumbo.

Ni miye mwanankwavi samwemzundu a.k.a Samwechengo. 0716 266171/0784 587838.

No comments:

LinkWithin

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...